NA DIRAMAKINI
MWENYEKITI wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Babati Mjini mkoani Manyara,ndugu Magdalena Urono amehitimisha mafunzo ya Mradi wa Kukuza Ajira na Ujuzi kwa Maendeleo ya Afrika (E4D) kwa awamu ya tatu na kuwatunuku vyeti vijana wapatao 189 katika Chuo cha VETA Manyara.
Ndugu Magdalena amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kutengeneza mazingira rafiki ili vijana waweze kujiajiri.
Aidha ameyashukuru, mashirika ya kimataifa Shirika la Misaada la Ujerumani (GIZ),Shirika la Maendeleo la Norway (NORAD), Shirika la Maendeleo la Korea (KOIKA) na Umoja wa Ulaya (EU) kwa kufadhili mradi huo kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.Amewaasa vijana kutumia vyema fursa ya ujuzi walioupata katika kujikwamua kiuchumi.
Amewataka wale vijana ambao hawatapata ajira katika sekta rasmi kutengeneza vikundi ili waweze kuaminika hatimaye kupata mikopo kutoka katika sekta mbalimbali za kifedha.