Mama Mariam Mwinyi aitaka jamii kuzingatia usalama wa chakula

NA DIRAMAKINI

MWENYEKITI wa Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF) ambaye ni Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mama Mariam Mwinyi ametoa wito kwa jamii kuzingatia suala la usalama wa chakula ili kujikinga na maradhi yatokanayo na chakula kisicho salama.
Mke wa Rais wa Zanzibar, Mama Mariam Mwinyi akihutubia baada ya kumalizika kwa matembezi ya kilomita tano ya kuadhimisha Siku ya Usalama wa Chakula Duniani yaliyoanzia Mombasa hadi Mapinduzi Square (Kisonge) jijini Zanzibar ambapo vikundi vya mazoezi vimeshiriki matembezi hayo yaliyofanyika leo Juni 7, 2023. (Picha na Ikulu). 

Mama Mariam Mwinyi ameyasema hayo kwenye Maadhimisho ya Siku ya Kimtaifa ya Usalama wa chakuka yaliyofanyika viwanja vya Mwembekisonge, Wilaya ya Mjini.

Amesema, kumekuwa na ongezeko la maradhi yanayosabishwa na usalama mdogo wa chakula, jambo alilolieleza kuathiri afya kwenye jamii.
Aliiasa jamii, kula vyakula vilivyo salama kwa kufuata mtindo mzuri wa kula pamoja na kufanya mazoezi ili kuipunguzia Serikali mzigo mkubwa wa matibabu.

Mwenyekiti huyo wa ZMBF ameeleza moja ya lengo la kuanzishwa kwa taasisi ya hiyo ni kuona namna bora ya kuunga mkono jitihada za Kitaifa na Kimataifa kwenye suala zima la kuimarisha lishe, afya na ustawi wa Wazanzibari ili kukuza maendeleo ya kiuchumi hususani kwa wanawake, watoto na vijana.

Pia, amesema Siku ya Usalama wa Chakula Duniani ni jambo jema linaloleta uelewa mpana juu ya mambo yanayohusu usafi na usalama wa chakula katika kupunguza maradhi na kuimarisha uchumi wa Zanzibar.
Hivyo, aliwasihi watunga sera, Mamlaka ya Usalama wa Chakula, wanasayansi, wakulima, wauzaji wa chakula, wapishi, walimu, wanafunzi na watumiaji mbalimbali, kuongeza bidii za pamoja ili kuhakikisha mwamko wa Usalama wa Chakula unaongezeka Zanzibar.

Mama Mariam amewataka watunga sera na waratibu kuhakikisha wanazingatia sera za udhibiti wa mifumo kwa usalama wa chakula na kuimarisha ushirikiano wao kwa wadau wote na kuhakikisha wanaifahamu miongozo na kuitumia mifumo iliopo katika juhudi za kumlinda mlaji.
Aidha, aliwaasa wafanyabiashara za chakula kwamba wana jukumu la kufuata maelekezo ya viwango vilivyotolewa na mamlaka na kuwaeleza kuwa jukumu la kumlinda mlaji limo mikononi mwao.

Aliisisitiza jamii suala la usalama wa chakula ni pamoja na kuzingatia kula mlo uliotimia ili kupata lishe bora zaidi kwa watoto, wazee na wajawazito kwa kuimarisha mfumo wa kinga ulio imara na makuzi mazuri kwa watoto.

“Tujitahidi kula chakula kilicho safi kwa kuzingatia virutubisho na wingi unaofaa au unaohitajika,"amesisitiza Mama Mariam.
Wakati huo huo, Mama Mariam Mwinyi ameupongeza uongozi wa Wizara ya Afya na wa Wakala wa Chakula na Dawa kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya kwa kudhibiti vyakula vinavyoingia na vile vinavyozalishwa nchini kwa kuhakikisha kuwa salama kwa matumizi ya binadamu.

“Kwa hakika, ukaguzi mnaoufanya kwenye maeneo yanayouzwa vyakula na kuwepo kwa Maabara za kisasa za ZFDA hufanya tujiamini juu ya bidhaa za vyakula zilizopo kwenye soko la Zanzibar kuwa ni salama kwa matumizi ya binadamu,”amebainisha Mama Mariam.

Awali akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Afya, Nassor Ahmed Mazurui amesema,wizara kupitia taasisi zake wanaweka taratibu bora za kudhibiti vyakula vibovu visiingie nchini.

“Tuhakikishe tunakula vyakula bora, usafi wa mazingira na uzalishaji wake, kwa bidhaa zote za mashambani na kwenye mifugo,"amesisitiza Waziri Mazurui.

Pia, ameitaka jamii kufuata taratibu za kuvuna mara baada ya umwagiliaji na kupigwa dawa kwa mazao na wanyama.
Naye Mkurugenzi Mtendaji kutoka Wakala wa Chakula, Dawa na Vipodozi (ZFDA), Dkt.Burhan Othman Simai amesema, jukumu kubwa la taasisi hiyo ni kulinda afya ya jamii katika kuhakikisha bidhaa za chakula, dawa, vipondozi, vifaa tiba na vitendanishi vina ubora, usalama na ufanisi unaotakiwa kwa mujibu wa viwango vya kitaifa na kimataifa.

ZFDA ilianzishwa mwaka 2006 na kufanya kazi rasmi mwaka 2007 kwa mujibu wa Sheria ya Chakula Dawa na Vipodozi Na. 2/2006 na marekebisho yake,Sheria Na.3/2007.

Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Usalama wa Chakuka yenye kauli mbiu, “Usalama wa chakula ni jukumu la kila mmoja wetu”awali yaliambatana na mtembezi ya kilomita tano yaliyoongozwa na Mwenyekiti wa Zanzibar Maisha Bora Foundation, Mama Mariam Mwinyi, kutoka soko la mbogamboga Mombasa hadi viwanja vya Mwembe kisonge.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news