Mandoga atangaza ngumi mpya mbele ya RC Senyamule inayofuta kumbukumbu kichwani

NA DIRAMAKINI

MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Mheshimiwa Rosemary Senyamule amewakaribisha Watanzania wote kutoka ndani na nje ya mkoa huo katika tamasha la masumbwi ambalo linatarajiwa kumkutanisha Mtanzania, Bondia Karim Khalid Saidi maarufu kama Mandonga Mtu Kazi na raia wa Malawi litakalofanyika jijini Dodoma.

RC Senyamule ametoa wito huo baada ya kutembelewa na Bondia Mandonga ofisini kwake kuomba baraka ambapo tamasha hilo litafanyika Juni 24, 2023 majira ya jioni Chinangali Park jijini Dodoma.

"Nimefurahi sana leo kupata mgeni maarufu katika nchi yetu ya Tanzania katika mchezo wa ngumi, ndugu yetu Mandonga Mtu kazi, leo yupo katika Mkoa wa Dodoma akijiandaa kwa ajili ya shindano muhimu ambalo litafanyika tarehe 24, hapa katika Mkoa wa Dodoma eneo la Chinangali.

"Ndugu yangu Madonga nimefurahi sana, karibu sana Dodoma, tunaposema Dodoma fahari ya Tanzania, utakwenda kuifaharisha Dodoma kwa kiwango kikubwa sana, karibu sana Dodoma na ninajua kutakua kuna staili mpya ya ngumi ambayo utakuwa umekuja nayo hapa ambayo ni tofauti ninajua kila unapokwenda mambo yako ni tofauti."

Kwa upande wake,Bondia Mandonga mbali na kumshukuru Mheshimiwa RC Senyamule kwa mapokezi mazuri, pia ameahidi kufanya vema kwa heshima ya Mkoa wa Dodoma na Taifa kwa ujumla.

"Asante sana, ninamshukuru Mwenyenzi Mungu kwa kunikutanisha na mkuu wa mkoa wa makao makuu ya (nchi) Dodoma na hapa nimefika Dodoma, Karim Mandonga Mtu kazi katika fahari ya Watanzania, e bwana wee..ninasema hivi, Mwenyenzi Mungu akipenda yaani siyo tu kwamba nimekuja hapa kwa mama ni bure, tunachukua baraka kwa bibi mkubwa na tunakwenda kufanya majukumu yetu, lakini wakae wakijua wakazi wa Tanzania.

"E bwana wee...makao makuu imekuja ngumi mpya, hii ngumi inaitwa Kitimbwi Yaya ni ngumi yenye masakata mazito sana.

"Unaweza ukapigwa ngumi halafu ukasahau, profile ikafuta ukasahau familia,na ukasahau umetokea wapi unakwenda wapi, hii ngumi inaitwa Kitimbwi Yaya tumeileta kwa niaba ya Mheshimiwa, tuko na mama yetu, lazima niwakilishe ndani ya Mkoa wa Dodoma."

Wakati huo huo, Mheshimiwa RC Senyamule ameongeza kuwa, "Niwakaribishe sana wana-Dodoma na wengine wa mikoa ya karibu kuja kushangilia kwa sababu anashindana Mandonga na mwenzake kutoka nchini Malawi, kwa hiyo tumuunge mkono katika siku hiyo ya tarehe 24 jioni katika eneo la Chinangali Park."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news