MAYELE, NTIBAZONKIZA, NDIO WANAOCHUANA

NA LWAGA MWAMBANDE

LICHA ya bingwa wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara kujulikana kuwa ni Klabu ya Yanga ya jijini Dar es Salaam kwa msimu huu wa 2022/23,sasa macho na masikio yanaelekezwa kwa kiungo mshambuliaji wa Klabu ya Simba, Saido Ntibazonkiza dhidi ya straika wa Klabu ya Yanga, Fiston Mayele ambao wanawania kiatu cha dhahabu.

Awali, Mayele ambaye alikuwa ametupia mabao 16 hakuwa na shaka yoyote ya kutwaa tuzo hiyo, lakini mabao 15 ya Ntibazonkiza, ambaye alipachika mabao matano huku Simba ikiibuka na ushindi mnono wa mabao 6-1 dhidi ya Polisi Tanzania, huenda yakadhoofisha furaha ya Mayele.

Kwa kuliona hilo, uongozi wa klabu ya Yanga ulilazimika kumpeleka Mayele ambaye aliachwa awali jijini Mbeya ili kwenda kupambania tuzo hiyo, katika mchezo wa mwisho wa ligi hiyo dhidi ya Tanzania Prisons ambayo itachezwa Uwanja wa Sokoine.

Ingawa huu ni ubingwa wa pili mfululizo kwa Yanga na wa 29 jumla ambao unawafanya watanue rekodi yao ya kutwaa mara nyingi zaidi hadi mara saba zaidi ya watani Simba SC, bado kila mmoja anatamani klabu yake ionekane bora zaidi.

Aidha, Simba SC ambayo ipo nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo bora zaidi nchini itamaliza msimu huu kwa kuwakaribisha Coastal Union kutoka jijini Tanga.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema matokeo yatafahamika baada ya mechi ya mwisho ili kumpata mfungaji bora. Endelea;

1.Ligi inakwenda mwisho, bingwa amejulikana,
Lakini kuna muwasho, kwa asiyejulikana,
Ni hadi mechi ya mwisho, mfungaji kumjua,
Mayele Ntibazonkiza, ndio wanaochuana.

2.Kabla tarehe sita, mmoja lijulikana,
Magoli kumi na sita, Mayele aliyaona,
Ntiba wote kawapita, sasa wanatazamana,
Mayele Ntibazonkiza, ndio wanaochuana.

3.Kwa hiyo mechi ya mwisho, kwa kweli kitaumana,
Tungoje la damu jasho, wafungaji kupambana,
Sisi wengine korosho, tutakuwa twatafuna,
Mayele Ntibazonkiza, ndio wanaochuana.

4.Mayele ana usongo, alikosa mwaka jana,
Mwaka huu ni mpango, wa kiatu kukiona,
Barani kafika lengo, Bongo bado washindana,
Mayele Ntibazonkiza, ndio wanaochuana.

5.Kila la heri twatoa, wazidishe kupambana,
Kila mtu ajitoa, kwa timu wanapambana,
Nani sasa atatoa, bora tutayemuona?
Mayele Ntibazonkiza, ndio wanaochuana.

6.Yanga sasa ndiyo bora, ubingwa wameuona,
Magoli mengi si bora, Simba hayo wayaona,
Idadi ni barabara, jinsi wanazidiana,
Mayele Ntibazonkiza, ndio wanaochuana.

7.Sasa kwa mechi za mwisho, kwa kweli watachuana,
Mashabiki ni mipasho, ile watarushiana,
Hadi kipenga cha mwisho, alo bora tutaona,
Mayele Ntibazonkiza, ndio wanaochuana.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news