Mbunge aipa saluti DCEA kwa kukamata shehena ya dawa za kulevya

NA GODFREY NNKO

MBUNGE wa Viti Maalum kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM),Mheshimiwa Lucy Thomas Mayenga ameipa kongole Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) chini ya Kamishna Jenerali, Aretas Lyimo kwa kazi kubwa na nzuri ambayo inaendelea kufanya katika kudhibiti dawa za kulevya nchini.
Hayo ameyabainisha leo Juni 20, 2023 wakati akichangia maoni yake katika Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/2024 nchini.

"Lakini, Mheshimiwa Mwenyekiti nimesimama hapa leo, kwa kweli ninaomba kwa nafasi ya pekee kabla sijachangia bajeti hii, niipongeze Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Tanzania (DCEA) ambayo kwa mara ya kwanza, wamekamata Cocaine pamoja na Heroin kilo 200 na nusu.

"Mheshimiwa Mwenyekiti ninaipongeza mamlaka hii kwa sababu kazi hii inataka uzalendo wa hali ya juu, lakini pia vile vile inataka mtu ambaye nikisema mzalendo unaweza kuwa mzalendo.

"Kwenye mambo mengine, lakini kwenye suala la fedha hauko vizuri, lakini kwa kweli inataka uzalendo uki-base kwenye kutokupokea rushwa, ninaipongeza sana mamlaka hii na ninampongeza kwa nafasi ya kipekee Kamishna Mkuu (Kamishna Jenerali) wa mamlaka hii,Aretas Lyimo kwa kweli ninampongeza sana.

"Wamekamata bangi magunia 978, bangi kavu ambayo ilikuwa tayari kusafirishwa, wamekamata bangi mbichi magunia 5495, wamefyeka hekari 1093, kwa kweli taasisi (mamlaka) hii ambayo ipo chini ya jemedari wetu, Mheshimiwa Jenista Joackhiam Mhagama kwa usimamizi wenu tunawapeni pongezi nyingi sana.

"Mheshimiwa Mwenyekiti wote tunafahamu tupo hapa tunazungumzia masuala ya bajeti kwa maana ya kile tunachopata pamoja na matumizi, lakini madawa (dawa za kulevya) ya kulevya athari zake ni kwamba yakizidi kwenye nchi, hata uchumi kwanza unaharibika.

"Hakuna mtu ambaye ataweza kuwekeza sehemu ambayo uhalifu upo kwa kiwango kikubwa, na wahalifu wengi ni hawa ambao wanatumia, wanavuta bangi wanatumia madawa (dawa za kulevya) ya kulevya.

"Kwa hiyo, uhalifu ukiongezeka hakuna mtu hata wawekezaji ambao leo hii tunapiga kelele kuwaita, hawataweza kuja, lakini pia vile vile mheshimiwa mwenyekiti, nijaribu kusema kwa sisi wanawake ambao hasa ndiyo walezi, imagine una mtoto wako ambaye pengine anaweza akawa mmoja au pengine ni watoto wako ambao unawapenda na hakuna mzazi ambaye hapendi mtoto wake.

"Umekaa umemzaa mtoto wako, umemlea vizuri na umemsomesha wakati unasema sasa kwamba ndiyo umefika wakati wa yeye kuwa walau akulee wewe anakuja kuangamia kwenye suala hili la madawa (dawa za kulevya) ya kulevya.

"Kwa hiyo Mheshimiwa Mwenyekiti nimpongeze sana Mheshimiwa Rais (Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan) kwa kuwateua watu makini, kwa sababu tumeona baadhi ya maeneo ambayo yalikuwa na haya madawa ya kulevya kwa maana ya hizi bangi, ni maeneo ambayo kuna watu wengi huko Arusha, kuna viongozi, kuna watu na kuna wenyeviti.
"Kwa hiyo, yataka moyo wa kijasiri wewe kutoka pale ulipo, kwa maana ya Kamishna (Kamishna Jenerali) Lyimo kutoka pale alipo kwenda kuyafeka yale madawa (dawa za kulevya), kwa hiyo nimpongeze sana,"amefafanua Mheshimiwa Lucy Thomas Mayenga.

Awali

Pongezi hizo zinakuja ikiwa ni siku moja baada ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kutoa taarifa ya matokeo ya operesheni zake katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Kilimanjaro na Arusha na kufanikiwa kukamata dawa za kulevya aina ya heroin kilogramu 200.5.

Sambamba na bangi kavu iliyokuwa tayari kusafirishwa gunia 978, bangi mbichi gunia 5,465, bangi iliyosindikwa (skanka) kilogramu 1.5 na methamphetamine gramu 531.43.

Dawa zingine za kulevya zilizokamatwa ni heroin kete 3,878, cocaine kete 138, mililita 3,840 za dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya Pethidine pamoja na kuteketeza hekari 1,093 za mashamba ya bangi.

Hayo yalibainishwa Juni 19, 2023 jijini Dar es Salaam na Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo wakati akitoa taarifa ya ukamataji wa dawa hizo mbele ya waandishi wa habari.

Kamishna Jenerali Lyimo alifafanua kuwa, pia kwa kushirikiana na Bodi ya Kimataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya (INCB) mamlaka hiyo imezuia kuingia nchini jumla ya kilogramu 1,507.46 za kemikali bashirifu ambazo zingeweza kutengeneza dawa za kulevya.

"Ukamataji huo ulifanyika kuanzia Machi 25 hadi Juni 19, 2023 ambapo unahusisha watuhumiwa 109 wakiwemo raia watatu wa kigeni.Baadhi ya watuhumiwa wamefikishwa mahakamani na wengine wanatarajiwa kufikishwa mahakamani taratibu za kisheria zitakapokamilika,"amebainisha Kamishna Jenerali Aretas Lyimo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news