Mbunge wa Jimbo la Kisesa,Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina.
MCHANGO WA MBUNGE WA JIMBO LA KISESA, MHE. LUHAGA JOELSON MPINA (MB) AKICHANGIA KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA NISHATI KWA MWAKA 2023/2024 BUNGENI DODOMA TAREHE 1 JUNI 2023
1: UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kukushukuru sana kwa nafasi hii uliyonipa nami niweze kuchangia hotuba hii muhimu ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati kwa mwaka wa fedha 2023/2024 na awali ya yote niseme kwamba nimepitia hotuba ya Waziri na nimetembelea mabanda ya maonyesho ya wiki ya nishati kwenye viwanja vya Bunge ambapo nimepata maelezo mengi ya ziada kutoka kwa watalaamu wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati nawashukuru sana kwa ushirikiano wao na nimevutiwa sana na ubunifu huu.
Pili naomba nipongeze hatua zinazochukuliwa na Serikali kwenye mradi wa Bomba la Mafuta kutoka Uganda hadi Tanga East African Cruide Oil Pipelines Project (EACOP), bomba la mafuta lenye urefu wa kilomita 1,443 na 80% ya urefu huo iko Tanzania.
Nchi yetu kupitia TPDC ina hisa za 15% za umiliki na tayari tumeshachangia kiasi cha Tsh. Bilioni 354 katika gharama za uwekezaji ambayo ni 50% ya gharama zote zinazohitajika katika uwekezaji huo.
Kukamilika kwa upanuzi wa mradi wa Kinyerezi II na TPDC na kuanza kushiriki katika biashara ya kuagiza mafuta kutoka nje kupitia utaratibu wa Petroleum Bulk Procurement Agency (PBPA), Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere kufikia 87%, kazi nzuri iliyofanywa na REA ambapo vijiji 10,127 nchini vimefikishiwa umeme vikiwemo vijiji vya Jimbo la Kisesa haya ni mageuzi makubwa sana katika sekta ya nishati na nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kazi hii nzuri, Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba na watumishi wote wa Wizara ya Nishati kwa hayo mafanikio makubwa.
2. MRADI WA LIQUIFIED NATURAL GAS (LNG PROJECT)
Taarifa ya Waziri inaeleza kuwa majadiliano yanayohusu Mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia baina ya Serikali ya Tanzania na wawekezaji Kampuni ya Shell ya Uingereza na Equinor ya Norway na washirika wao yamekamilika na kwamba sasa wataalam wapo katika kazi ya kuandika mikataba ya mradi huo.
Mkataba mmoja ni wa Nchi Hodhi (HGA) na mwingine ni mkataba uliounganishwa wa vitalu vya Gesi Asilia Namba I, II na IV ambavyo gesi yake itatumika kwenye mradi wa LNG ili kuliwezesha taifa letu kuanza kunufaika na rasilmali ya gesi asilia tuliyobarikiwa na Mwenyezi Mungu ambapo akiba ya gesi asili iliyopo nchini mwetu ni futi za ujazo (cubic feet) Trilioni 57.
Pamoja na kazi nzuri inayoendelea changamoto ninazoziona ni kama ifuatavyo:-
(i) Hakuna taarifa ya kufanyiwa mapitio ya PSA katika vitalu na 1,2 na 4 vinavyokwenda kutumika katika mradi wa LNG licha ya Serikali kusimamisha mazungumzo hayo mwaka 2019 baada ya kubaini kuwa Country’s Gas Production Sharing Agreement zilikuwa na kasoro na kulifanya taifa lisinufaike vya kutosha na akiba ya gesi asilia iliyopo. PSA hizo zilikuwa zinawanufaisha makampuni ya kigeni yanayokuja kuwekeza.
Je Government Negotiation Team (GNT) imefika hitimisho ya vipengele vya mikataba wa HGA na vitalu na 1, 2 na 4 kwa ajili ya mradi wa LNG kwa kutumia nyaraka gani au PSA zipi ili kulinda maslahi ya taifa katika mkataba huo na kama Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan alivyoagiza na kusisitiza wakati wa kusaini makubaliano ya awali.
(ii) Usiri wa majadiliano katika vipengele vya mikataba unaondelea katika mradi wa LNG unaleta hofu kubwa kuhusu vigezo na masharti ya mikataba inayokwenda kuingiwa na ni kinyume na kifungu cha 16 (1) cha Sheria ya The Tanzania Extractive Industries (Transparency and Accountability) Act 2015 ambacho kinataka miradi leseni, vipengele na mikataba kuwekwa wazi kwenye tovuti na kutangazwa kwenye vyombo vya habari. TEITI mko wapi? Uvunjifu mkubwa wa sheria kiasi hiki unafanyika.
(iii) Majadiliano yamejikita katika kundi dogo la GNT, hadi vipengele vya mikataba vinakamilika na mikataba kuanza kuandaliwa kwa ajili ya kusainiwa hapakuwa na ushirikishwaji mpana wa wananchi, kwa mkataba mkubwa kama huu wa LNG, GNT ilitakiwa kufanya public hearing kwa kushirikisha watu wenye taaluma mbalimbali na Bunge kabla ya kufika hitimisho la majadiliano ya vipengele vya mkataba.
(iv) Kwa kuwa mkataba uko hatua za mwisho kuingiwa ni lini Bunge litashirikishwa ili kukidhi matakwa ya Kifungu cha 12 cha The Natural Wealth and Resources (Permanent Sovereignty) Act No.5 of 2017.
(v) Serikali imeingia mkataba na Kampuni ya Baker Botts LLP ya Uingereza kama mshauri elekezi katika masuala ya teknolojia,kifedha na masoko ya kimataifa ili kuuza gesi iliyogundulika kwa misingi ya ushindani na kulinda maslahi ya taifa lakini wakati huo mmoja wa wabia Kampuni ya Shell nayo inatoka Uingereza hapa tunawezaje kuzuia mgongano wa maslahi (Conflict of Interest)
Tunakwenda kuingia mkataba mkubwa wa kuvuna raslimali za taifa za gesi asilia katika Mradi wa LNG tukiwa na mambo mengi ambayo hayajawekwa wazi na pia usiri mkubwa unaondelea unaweza kupelekea kwenda kuingia
mikataba mibovu itakayoligharimu taifa letu.
Nchi yetu haina rekodi nzuri katika eneo la mikataba ya raslimali za nchi na hivyo waheshimiwa wabunge lazima tuwe makini sana tunapofanya maamuzi.
Waziri wa Nishati wakati wa kuhitimisha hoja hii awaeleze watanzania namna maslahi ya taifa yalivyozingatiwa katika vipengele vya mkataba, sababu za kutoshirikisha Bunge na wananchi katika maandalizi ya vipengele vya mikataba kama sheria zinavyotaka hususan kwa mradi mkubwa na wa maslahi makubwa ya Taifa wa LNG.
3. MKATABA BAINA YA TANESCO NA KAMPUNI YA TECH MAHINDRA YA NCHINI INDIA
Hotuba ya Waziri haijaeleza utekelezaji wa ujenzi wa Mfumo wa TEHAMA ambao unatekelezwa na Kampuni ya Tech Mahindra ya India. TANESCO na Tech Mahindra ziliingia mkataba wa Tsh. Bilioni 70 mwaka wa fedha
2021/2022 kujenga mfumo wa TEHAMA.
Hatujaelezwa mradi huu umefikia wapi na umeisaidiaje Tanesco kuboresha mifumo yake ya TEHAMA? Je TANESCO ilipata kibali cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kama hakuna uwezo wa ndani ya nchi wa kujenga mfumo huo? Fedha nyingi zimetengwa na kutumika katika mradi huu halafu Bunge halipewi taarifa
yoyote.Waziri atakapokuja awaeleze watanzania tija ya mradi huu.
4. BWAWA LA JULIUS NYERERE (JNHPP)
Nimefurahi sana kusikia kuwa Ujenzi wa Mradi wa Kuzalisha Umeme kwa Kutumia Maji wa Julius Nyerere (JNHPP), MW 2,115 umefikia asilimia 86.89 ambapo hadi kufikia tarehe 23 Mei, 2023 kina cha maji ya Bwawa la JNHPP kilikuwa kimefikia mita 160.51 kutoka usawa wa bahari ambapo ili kuweza kuzalisha umeme, kiwango cha chini cha maji kinatakiwa kufikia mita 163 kutoka usawa wa bahari.
Hii ni hatua nzuri sana pongezi kwa Serikali. Changamoto za usimamizi wa mkataba huu baina ya TANESCO na Kampuni ya Arab Contractors ya Misri ukiwa mradi umefikia 86.89% na ukiwa hatua za mwisho kama ifuatavyo:-
(i) Makato ya CSR bilioni 270 hadi sasa Wizara haijazidai kutoka kwa mkandarasi kama mkataba unavyotaka. Waziri katika hotuba yake ameeleza kwa kuanzia Serikali itajenga chuo kikubwa cha kisasa cha ufundi wa umeme na mafuta na gesi mkoani Lindi.
Mradi unatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2024 bila kutaja gharama za mradi huo na bila kuweka bangokitita la miradi yote ya kijamii itakayonufaika na CSR ya Mradi wa JNHPP.
Hii inathibitisha kuwa wizara haina dhamira ya dhati ya kudai fedha hizo kutoka kwa Mkandarasi na kama ilivyoelezwa na CAG kwenye ripoti yake ya mwaka 2021/2022.
(ii) Kushindwa kudai tozo ya fidia ya ucheleweshaji (5%) ya bei ya mkataba kiasi cha Tsh. Bilioni 327.93 kwa mwaka na kwa miaka miwili ni sawa na Tsh. Bilioni 655. Hotuba ya Waziri haijaeleza hatua zozote zinazochukuliwa na Serikali kudai fedha hizo licha pia ya CAG kulalamikia eneo hili.
Kitendo cha Waziri wa Nishati, kushindwa kueleza hatua zilizochukuliwa kukusanya fedha hizi kwa mujibu wa mkataba kunathibitisha kwamba hakuna nia njema na kuleta sintofahamu kubwa kwa wananchi. Leo hii Waziri wa Nishati awaeleze watanzania fedha zao ziko wapi?
Pia Wizara na TANESCO wameshindwa kuidai Kampuni ya IPTL madai halali baada ya Serikali kushinda kesi mahakamani tangu Machi 2021 bila sababu za msingi Tsh.Bilioni 342.
Waziri aueleze umma wa watanzania fedha zao Bilioni 342 ziko wapi? Wizara ya Nishati na TANESCO wameshindwa kukusanya madai haya ya kisheria zaidi ya Tsh bilioni 926 katika Bwawa la Mwalimu Nyerere na IPTL Tsh Bilioni 342 jumla ya madai yote ni Tsh Trilioni 1.268.
Waheshimiwa wabunge tumeitaka muda mrefu Serikali kukusanya madai haya halali ya watanzania yaliyopo kisheria na CAG amesema kama Waziri wa Nishati atashindwa kutoa majibu ya kujitosheleza tusipitishe bajeti yake hadi hapo Bunge hili litakapoletewa taarifa za kukusanywa kwa fedha hizi.
5. MWENENDO WA BEI ZA MAFUTA KATIKA SOKO LA NDANI
Hotuba ya Waziri imeeleza kupanda kwa bei za mafuta yaliyosafishwa katika soko la dunia kuliathiri pia bei za mafuta katika soko la ndani hapa nchini ambapo Serikali ikalazimika kuweka ruzuku kuanzia mwezi Juni hadi Desemba, 2022 ya Shilingi Bilioni 479.37 ili kukabiliana na hali hiyo.
Hadi sasa bei ya nishati ya mafuta bado ziko juu na zinachangia kwa kiwango kikubwa kupanda kwa bei za bidhaa na kusababisha ugumu wa maisha kwa watanzania lakini hotuba ya waziri haionyeshi mipango,mikakati na hatua zinazochukuliwa na Serikali kukabiliana na hali hii.
Kwa ujumla eneo hili lina changamoto nyingi:-
(i) Serikali iliahidi kutoa Tsh Bilioni 100 kila mwezi hivyo kwa miezi 7 ni Tsh Bilioni 700 kwanini leo inaripotiwa Tsh Bilioni 479.37 tena bila kueleza hizo fedha zilitolewa kupitia kifungu gani.
(ii) Kwanini Waziri wa Nishati hakuweka mchanganuo (matrix) ya kueleza malipo ya fedha za ruzuku ya Tsh. Bilioni 479.37 walilipwa kina nani ili kuweka uwazi wa matumizi ya fedha za umma.
(iii) Hapakufanyika tathmini ya kina wakati wa kuweka Ruzuku ya mafuta kiasi cha Tsh Bilioni 100 kila mwezi na ruzuku hiyo imekuja kuondolewa bila tathmini ya kina na bila Bunge kuhusishwa.
(iv) Hakuna uhakiki na ufuatiliaji wa bei katika soko la dunia na soko la ndani (Due Diligence) ili kujiridhisha na uhalali wa bei unaotamkwa na wafanyabiashara wanaoagiza na kusambaza mafuta nchini, PBPA na EWURA huoni wapi wamedhibiti hali hiyo matokeo yake kuna udhibiti hafifu wa bei za mafuta na kusababisha bei ya mafuta kuendelea kuwa juu kwa visingizio vya soko la dunia na gharama na faida (Premium).
(v) Pamoja na Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) kushiriki zabuni za kuagiza mafuta kupitia PBPA lakini shirika hilo halina mtaji wa kutosha wa kuagiza mafuta na kuiwezesha Serikali kupata taarifa sahihi za mwenendo wa biashara ya mafuta.
Imani yangu kuwa endapo Serikali ingesimamia kikamilifu mfumo mzima wa bei za nishati ya mafuta na kujiridhisha na usahihi wa gharama zinazotamkwa na makampuni yanayoagiza mafuta, na pia kuiwezesha TPDC kimtaji ili iweze kuagiza mafuta kwa wingi bei za mafuta zitashuka kwa kiwango kikubwa.
Waziri wa Nishati atakapokuja kuhitimisha hoja yake, aeleze sababu za kushindwa kuweka program na mikakati ya kudhibiti mfumko wa bei za nishati ya mafuta hapa nchini.
6. KITUO CHA MIITO YA SIMU (UNIFIED CALL CENTRE)
Zipo taarifa za kuvunjwa kwa vituo vya miito ya simu kwa huduma kwa wateja vilivyokuwepo mikoani na kuunganishwa kuwa na kituo kimoja Mikocheni Dar es Salaam, kituo hiki nacho kuna taarifa kuwa kimebinafsishwa kwa Kampuni binafsi.
Je ni sahihi kwa eneo nyeti kama hili kulibinafsisha kwa kampuni binafsi,taarifa zote nyeti za kutokea hitilafu za umeme, majanga ya moto kuripotiwa kupitia kampuni binafsi? Hiyo kampuni iliyopewa hiyo kazi ilipatikanaje? Ajira za vijana wa kitanzania zimelindwa vipi katika mkataba huo wa ubinafsishaji?
Nawasilisha,
.......................................
Luhaga Joelson Mpina (Mb)
Mbunge wa Jimbo la Kisesa