Mheshimiwa Mpina: Waziri Dkt.Mwigulu amepotosha maudhui ya hoja zangu bungeni

"Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dk. Mwigulu Nchemba leo tarehe 26 Juni 2023 wakati akihitimisha hoja yake Bungeni ametumia muda mwingi kupotosha maudhui ya hoja zangu nilizowasilisha Bungeni katika Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2023/2024 jambo ambalo haliruhusiwi na Kanuni za Bunge.

Mbunge wa Jimbo la Kisesa,Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina ametoa taarifa kwa umma kuhusu ufafanuzi ambao anadai ni upotoshaji uliofanywa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt.Mwigulu Lameck Nchemba kuhusu mchango wake alioutoa bungeni kuhusu Bajeti Kuu ya Serikali 2023/2024 tarehe 26 Juni 2023.

Ilitarajiwa Waziri wa Fedha angetumia muda mwingi kujibu hoja za wabunge badala yake alitumia zaidi dakika 12 kuzungumzia personalities bila kujibu hoja mahsusi za watanzania zilizohitaji majibu ya Waziri wa Fedha.

Waziri wa Fedha anasema Mpina anataka biashara ziendelee kufungwa na anataka Serikali iendelee kushikilia mizigo na kwamba mimi napingana na maono ya Mhe. Rais aliyeagiza biashara zisifungwe maneno ambayo sio ya kweli na sio sehemu mchango wangu.

Wakati najenga hoja ndani na nje ya Bunge na mchango wangu wa maandishi wa kuhusu Bajeti Kuu ya Serikali ya Mwaka 2023/2024 nilieleza bayana kupinga Kauli ya Waziri wa Fedha ya kuzuia Mamlaka za udhibiti kutokufunga biashara kwa sababu zozote zile kuanzia Tarehe 1 Julai 2023, neno KWA SABABU ZOZOTE ZILE ndilo ambalo ninalopinga mimi kwa sababu yapo mazingira yanayolazimu biashara ifungwe lakini pia kuna Biashara halali na Biashara haramu. Nakukuu sehemu ya mchango wangu.

“Kupiga marufuku ufungaji wa biashara kwa sababu zozote zile Waziri wa Fedha katika Ibara ya 126 ya hotuba anapendekeza kutofunga biashara kwa sababu zozote zile kuanzia tarehe 1 Julai 2023 huku akijua kuwa kufunga biashara ni sehemu ya takwa la kisheria inapobidi kufanya hivyo.

Mfano mgodi au kiwanda kinapokutwa kinatiririsha maji machafu na yenye kemikali za sumu kwenda kwenye makazi ya wananchi na kwenye vyanzo vya maji na kuhatarisha maisha ya watu na viumbe hai wengine, Je mamlaka za udhibiti zifanye nini, ziache watu wafe ili kulinda biashara?,

Mfanyabiashara anakutwa hana vibali, hana leseni, hana nyaraka yoyote, anauza bidhaa feki, bandia na zilizokwisha muda wa matumizi zenye athari za kiuchumi na kiafya kwa binadamu na viumbe hai wengine, ashtakiwe yeye halafu bidhaa zake ziendelee kuuzwa kwa wananchi?

Hata wafanyabishara wa dawa za kulevya, fedha haramu na biashara haramu zingine nao waachwe waendelee na biashara zao wasifungiwe?."

Kauli hii ya Waziri wa Fedha Dk. Mwigulu Nchemba inaleta mkanganyiko mkubwa wa kisheria na mifumo ya udhibiti nchini, lakini pia inarudisha nyuma jitihada za Serikali zinazofanywa na Mamlaka za Udhibiti katika kusimamia ustawi wa taifa na wananchi kwa upande mwingine wataelewa kwamba Serikali imekuwa ikiwaonea.

Aidha, ifahamike kuwa ada na tozo zinazotozwa na mamlaka za udhibiti zipo kwa mujibu wa Sheria na zilikubalika kwa Waziri mwenye dhamana ya fedha hivyo sio sahihi kusema kwamba usimamizi wao makini unasukumwa na kuongeza mapato ya taasisi husika.

Lakini pia ni muhimu kuthamini kazi nzuri inayofanywa na mamlaka zetu za udhibiti katika kulinda biashara, usalama wa afya za walaji na uchumi wa nchi, Taasisi kama TBS, NEMC, TMDA, TPRI, OSHA, Polisi, TRA, DCEA, LATRA, EWURA, BoT, TCRA, eGA, TCAA, FIU, WMA, NACTVET, FCC, BRELA, PPRA nk. zinapaswa kupongeza kwa kazi nzuri wanazofanya.

Waziri alipaswa kulieleza Bunge hatua zilizofikiwa katika utekeleza wa mpango wa kuboresha mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji nchini (Blueprint), lakini pia Waziri angeeleza hatua zilizochukuliwa dhidi ya watumishi wachache wasio waaminifu ambao wamekuwa wakikiuka Sheria na taratibu na kujihusisha na vitendo vya rushwa na kuwanyanyasa wafanyabishara badala ya kuzituhumu kiujumla taasisi za udhibiti ambazo zimekuwa zikifanya kazi nzuri kwa mujibu wa sheria na kwa ustawi wa taifa letu,”mwisho wa kunukuu.

Nimesikiliza kwa makini sana majibu ya Waziri wa Fedha wakati akihitimisha hoja yake na nilitegemea angefanya marekebisho ya hotuba yake Ibara ya 126 kwa kuondoa neno Kwa sababu zozote zile na badala yake angesema kuzuia ufungaji holela wa biashara.

Kuzuia kufunga biashara kwa sababu zozote zile kama alivyosema Waziri wa Fedha ni kuweka rehani maisha ya watanzania na viumbe hai wengine,kuua ajira, biashara na uwekezaji nchini na kuhalalisha biashara haramu na ukwepaji wa kodi.

(i) Leo hii akutwe mfanyabiashara ameingiza na kuuza mchele, ngano, mafuta, dawa, mbolea na bidhaa zingine feki, bandia na zilizokwisha muda wa matumizi aruhusiwe tu kuendelea na biashara? Hii hasara kwenye taifa inabebwa kwa gharama za nani? Matukio ya kuuzwa mchele wa plastiki na bidhaa zingine zisizo na ubora yanaripotiwa mara kwa mara nchini.

(ii) Leo hii unakuta bucha inauza nyama vibudu, samaki waliioza na wenye kemikali zenye viambata vya sumu waruhusiwe wafanye biashara? Kweli Taifa letu limefikia hapo?

(iii) Leo hii ukute mfanyabishara hana kibali wala leseni, mamlaka za udhibiti na usimamizi zitajuaje kama hiyo biashara ni halali, zitajuaje kama hiyo mali sio ya wizi na zitajuaje kama hizo bidhaa zina ubora unaotakiwa, naye asifungiwe?

(iv) Watu wanaotoka nje ya nchi na kufanya biashara ya bidhaa mbalimbali nchini bila vibali wala leseni nao waruhusiwe tu?

(v) Leo hii kwenye nchi yetu biashara haramu na za magendo nazo zimeruhusiwa na Waziri wa Fedha?

(vi) Ukwepaji wa kodi na utoroshaji wa fedha na raslimali za nchi nao umeruhusiwa?

Wakati nachangia niliamini Waziri angeelewa msingi wa hoja na mashaka niliyokuwa nayo juu ya kauli hiyo, lakini badala yake yeye akaleta upotoshaji na kumsingizia Mhe. Rais kuwa ndiye amemuagiza kufanya hivyo.

Haya ni Matumizi mabaya ya jina la Mhe. Rais. Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan mara kadhaa amewaonya mawaziri tena hadharani kuacha tabia ya kumsingizia wanapofanya maamuzi yao badala yake aliwataka kufanya maamuzi kwa kuzingatia sheria za nchi na hali ya uchumi na wawe tayari kutetea maamuzi yao bila kusema ni maelekezo kutoka juu.

Pamoja na onyo hilo Waziri huyu imekuwa ni utamaduni wake wa kumsingizia Mhe. Rais kwenye hoja mbalimbali ili kuuficha udhaifu wake katika kusimamia majukumu ya Serikali.

Mambo Muhimu aliyopaswa kuyazingatia Waziri wa Fedha katika kujibu hoja yangu

(i) Taasisi za Usimamizi na udhibiti ni taasisi za Serikali na zinasimamiwa na Mawaziri wenye dhamana hivyo utendaji dhaifu wa taasisi una Baraka za Waziri na haitarajiwi kama taasisi hizo zinatekeleza majukumu yake kinyume cha Sheria, zinafunga biashara kiholela, zinanyanyasa na kuonea wafanyabiashara na wawekezaji alafu Waziri mwenye dhamana anashindwa kuchukua hatua anasubiri mpaka ifike Tarehe 1 Julai 2023.

(ii) Waziri wa Fedha anazituhumu taasisi za udhibiti kiujumla na bila takwimu kuliwezesha Bunge kujua ukubwa wa tatizo, lakini taasisi zingine ni zile anazozisimamia yeye na hivyo kama kuna ubaya zimeufanya kwenye umma basi kaufanya yeye.

Hivyo tuhuma anazozitoa dhidi ya taasisi hizo ni kuwahadaa wananchi. Tunakumbuka malalamiko makubwa kwa wafanyabiashara wa soko la Kariakoo, Njombe na maeneo mengine nchini hadi kumlazimu Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa kuingilia kati na kuunda Tume ya uchunguzi.

(iii) Waziri wa Fedha kushindwa kutekeleza kwa vitendo Mpango wa kuboresha mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji nchini (Blueprint) ambao unafafanua kwa kina namna bora ya kupunguza changamoto za mwingiliano wa kitaasisi na utitiri wa ushuru, tozo na kodi.

(iv) Waziri wa Fedha ameshindwa kutekeleza agizo la Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan alilolitoa mwaka 2021 la kuzuia Task Force, kufunga biashara na akaunti bila sababu za msingi lakini badala yake wafanyabishara waliendelea kufungiwa biashara na akaunti zao na taasisi zilizo chini ya wizara yake, amekaidi agizo la Mhe. Rais la muda mrefu leo anakuja mbele ya Bunge kutumia jina Mpina kama kichaka cha kuficha udhaifu wake.

(v) Waziri wa Fedha alileta pendekezo bungeni la kusamehe wawekezaji mahiri maalum kwa kuwaondolea Kodi ya VAT na Kodi ya mapato lakini pia hata wanapofanya miamala haramu ya Transfer Pricing wasitozwe faini hali iliyopelekea Serikali kupunguza wigo wa ukusanyaji mapato na kulazimika kuweka kodi na tozo kubwa kwa wananchi masikini ili kufidia mapato ya Serikali yaliyopotea.

Leo hii bila aibu anapendekeza kuongeza tozo katika mafuta ya Tsh. 100 kwa lita ya Dizeli na Petroli na ushuru wa Tsh. 20 kwa kila kilo moja ya saruji hali itakayochochea zaidi ugumu wa maisha na mfumko wa bei ambao pia kwa muda mrefu ameshindwa kuudhibiti.

Mheshimiwa Rais anathamini Mamlaka ya Bunge na michango ya wabunge wote kwa mujibu wa Katiba ya nchi na ndiyo maana kupitia mawaziri amekuwa akileta Bungeni mapendekezo ya mipango ya Serikali ili wawakilishi wa wananchi wapate nafasi ya kupitia, kujadili, kushauri na baadaye kufanya maamuzi ya kuboresha, kukubali au kukataa tena kwa kupiga kura ya wazi.

Waziri wa Fedha Dk. Mwigulu Nchemba hana mamlaka kisheria wala ya kikanuni ya kuzuia uhuru wa mawazo wa Mbunge yoyote.

Ni vigumu kuamini Mhe. Dk. Mwigulu Nchemba Waziri wa Serikali kusimama mbele ya Bunge kusema uongo na kupingana na sheria za nchi alizoapia kuzisimamia na kuzilinda na pia kuongelea mambo asiyoyajua na hana ushahidi nayo.

Wakati nikiwa Waziri na Naibu Waziri Mamlaka za udhibiti zilichoma kwa moto nyavu haramu na hazikuchoma nyavu halali za Wavuvi, vile vile viwanda na migodi iliyokuwa inatiririsha maji machafu yenye kemikali za sumu kwenda kwenye vyanzo vya maji na makazi ilifungwa kwa muda ili kuzuia athari na kupisha matengenezo ya mifumo ya majitaka mfano Effluent Treatment Plant (ETP) na Tailings Storage Facilities (TSF) nk na hatua hizo zote zilitekelezwa kwa mujibu wa Sheria.

Waziri wa Fedha na Mipango amekwenda mbali zaidi na kupendekeza kufuta mfumo wa ukaguzi wa bidhaa kabla hazijasafirishwa kuja nchini (Pre-shipment Verification of Conformity-PVoC) ambapo baada ya ukaguzi huo hupewa cheti cha ubora (Certicate of Conformity-CoC), utaratibu huu ulianzishwa ili kuhakikisha kuwa kuna ubora wa bidhaa na usalama wa afya za watumiaji, kuhifadhi mazingira na kukataa Tanzania kugeuzwa kuwa dampo la bidhaa feki na bandia, au zilizokwisha muda wa matumizi, uamuzi wa Waziri wa Fedha wa kuondoa faini ya Asilimia 15 kwa bidhaa
zinazoingizwa nchini bila cheti cha CoC inamaanisha kuwa amefuta utaratibu wa PVoC ambapo sehemu mbalimbali Duniani TBS imeweka watoa huduma (Service Providers).

Mimi sina tatizo na kufutwa kwa mfumo wa PVoC lakini Serikali ilipaswa kueleza kwa kina mbadala wa PVoC ili kuepusha nchi kugeuzwa kuwa dampo la bidhaa hafifu kutoka nje ya nchi.

Waziri wa Fedha amefanya utafiti na tathmini ya kutosha kabla ya kuondoa utaratibu wa PVoC? Je Shirika la Viwango Tanzania (TBS) lina uwezo wa kutosha kusimamia jukumu hili bila Service Providers? TBS inavyo vifaa vya kutosha vya ukaguzi wa bidhaa? Na je TBS inayo raslimali watu wa kutosha kubeba jukumu hili?.

Waziri wa Fedha alishawahi kujiuliza tangu ateuliwe kushika wadhifa huo kwanini mfumko wa bei na ugumu wa maisha kwa watanzania umeongezeka mara dufu?.

Amewahi kujiuliza kwa nini Dola za Marekani zimeadimika nchini na Shilingi ya Tanzania kuporomoka thamani?, Amewahi kujiuliza kwa nini ubadhirifu na ufisadi wa kutisha wa fedha za umma umeshamiri?, amewahi kujiuliza kwa nini wafanyabiashara wanalalamikika kila kona ya nchi, kwa nini Wafanyabiashara wa Kariakoo walifanya mgomo na kufunga maduka kwa zaidi ya siku 2 jambo ambalo ni nadra kutokea tangu nchi ipate uhuru?.

Ninamshauri Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Lameck Nchemba awe msikivu na afuatilie hoja za wananchi na wabunge kwa makini na kutoa majibu sahihi badala ya kufanya upotoshaji mfano katika mchango wangu wa maandishi ambao una vipengele 13 na maswali zaidi ya 50, lakini Waziri ameweza kujibu swali 1 tu nalo kwa kupotosha maudhui yake.

Tumepewa dhamana na watanzania ni muhimu kufanya maamuzi ya haki yatakayolinda maslahi mapana ya taifa letu na kuepuka kufanya maamuzi ambayo yataliingiza taifa kwenye matatizo makubwa ya Kijamii na Kiuchumi.

Asanteni kwa kunisikiliza,
Nawasilisha,
Luhaga Joelson Mpina (Mb)
Mbunge wa Jimbo la Kisesa

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news