Mifuko ya plastiki yapigwa marufuku kuingia Hospitali ya Taifa Muhimbili

NA MWANDISHI WETU

UONGOZI wa Hospitali ya Taifa Muhimbili umepiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki kwa watoa huduma na ndugu wa wagonjwa katika mazingira ya hospitali (Upanga na Mloganzila) ikiwemo wodini na maeneo mbalimbali ya kutolea huduma.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma (MNH), Bw. Aminiel Aligaesha katazo hilo linatolewa kufuatia uwepo wa mifuko ya plastiki kwenye mazingira ya hospitali iliyopigwa marufuku na Serikali nchini.

“Mifuko hii inaletwa na baadhi ya ndugu wa wagonjwa ambao huitumia kama vibebeo vya chakula wanapokuja kutembelea ndugu zao waliolazwa wodini na baadhi ya watoa huduma hospitalini hapa,” amesema Bw. Aligaesha.

Ameongeza kuwa katazo hilo linaanza mara moja na ni kwa kampasi zote mbili za Hospitali ya Taifa Muhimbili ambazo ni Upanga na Mloganzila.

Bw. Aligaesha ameiomba jamii kutoa ushirikiano katika kukabiliana na matumizi ya mifuko ya plastiki hospitalini hapa kwa kuwa lengo ni kulinda na kutunza ustawi wa mazingira ya eno hilo na watu wake.

Ikumbukwe kuwa, kauli mbiu ya Siku ya Mazingira Duniani mwaka huu ni Pinga uchafuzi wa mazingira utokanao na mifuko ya plastiki.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news