Mkurugenzi Mkuu wa NHC asisitiza uadilifu na weledi kwa wafanyakazi

NA MWANDISHI WETU

MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Bw. Hamad Abdallah amewataka wafanyakazi wa shirika kufanya kazi zao kwa uadilifu na weledi ili kuliletea shirika tija. 
Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Bw. Hamad Abdallah akikagua mradi wa nyumba za makazi unaotekelezwa na NHC eneo la Chatur wilayani Muheza leo.

Ameyasema hayo alipokuwa akiongea na wafanyakazi wa shirika hilo jijini Tanga alipofanya ziara ya siku mbili ili kukagua miradi ya ujenzi wa nyumba na kuhimiza utendaji wa kazi.

"Kuna wanaodhani nimekuja NHC kufukua makaburi, kama kuhimiza uadilifu na utendaji wa kazi ili kuiletea nchi yetu mafanikio kwenye sekta ya nyumba ndiyo kufukua makaburi hilo sintaliacha," amesema Bw. Hamad.
Amewapongeza wafanyakazi hao kwa kazi nzuri ya kukusanya kodi na kazi nzuri ya ujenzi wa nyumba katika mradi wa Chatur na akaomba mikoa mingine ifanye kazi kwa bidii ili kuliletea shirika tija.

Amesema kuwa, kila mfanyakazi atakayefanya kazi vizuri, kazi yake itatambuliwa na kuthaminiwa na akaonya wafanyakazi kutojihusisha na tabia na vitendo vibaya ikiwemo ulevi na rushwa vitakavyoharibu taswira nzuri ya shirika. 

Amehimiza wafanyakazi wa NHC kutoridhika na mafanikio yaliyofikiwa badala yake waendelee kuwa na tamaa na shauku ya kuliongezea shirika maendeleo endelevu kwa kutumia fursa zilizopo katika mikoa ya shirika. 
Akizungumzia huduma bora kwa wateja, Mkurugenzi Mkuu amesisitiza kuwa, wafanyakazi wote wa shirika wanapaswa kuwa na lugha nzuri na huduma bora kwa wateja ili biashara na huduma za NHC ziendelee kuamiwa na watanzania.

Amesema, ili hilo litokee ni lazima wafanyakazi wote kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya msingi ya shirika ambayo ni weledi, ushirikiano, uadilifu, uwazi, ufanisi na ubunifu. 
Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Bw. Hamad Abdallah akipata maelezo ya eneo linalohitaji uendelezaji lililopo Mkwakwani Jijini Tanga alipokuwa kwenye ziara yake ya kukagua miradi na majengo ya NHC jijini Tanga.

Akizungumzia maslahi ya wafanyakazi, amewahakikishia kuwa jambo hilo litazingatiwa na akaeleza kuwa muelekeo wa serikali ni kuachia Bodi za mashirika ya kibiashara kufanya maamuzi yenye tija, hivyo amewataka wafanyakazi hao kuendelea kuongeza tija katika kazi zao. 

Kadhalika, ili kuboresha utendaji wa kazi amewataka Mameneja wa Mikoa na Wakurugenzi kujenga tabia kila Jumatatu ya wiki kukutana na wafanyakazi ili kukumbushana wajibu katika kazi na kupanga mikakati ya kutatua changamoto zilizopo.
Meneja wa NHC Mkoa wa Tanga, Mhandisi Patrick Musa Kamendu akitoa taarifa kwa Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Bw. Hamad Abdallah ambaye amefanya ziara Jijini Tanga ya kukagua miradi ya shirika na kuhamasisha utendaji kazi.

Awali, akitoa taarifa ya mkoa, Meneja wa NHC Mkoa wa Tanga, Mhandisi Patrick Musa Kamendu amesema kuwa pamoja na kufanikiwa kukusanya kodi ya pango kwa kiwango cha juu, majengo mengi ya Mkoa wa Tanga yanayomilikiwa na NHC ni ya zamani hivyo yanahitaji matengenezo makubwa.

Amesema kuwa, mradi wa nyumba za makazi unaotekelezwa Chatur Muheza unakaribia kukamilika na kwamba Mkoa huo umeanza kuongea na wateja wanaozihitaji nyumba hizo. 

Naye, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa NHC, Bi. Fatuma Chillo amewahimiza wafanyakazi wa shirika kutambua kuwa Shirika lao ni Shirika la kibiashara, hivyo ni lazima wawe na utamaduni wa kutafuta masoko na kukamilisha kazi kwa wakati.

Ametaka kila mfanyakazi awe na vipaumbele vya kuliletea Shirika tija na kwamba rasilimali za shirika zitaelekezwa pale tu penye kuleta tija kubwa.

Akawataka wafanyakazi waache tabia ya kufanya kazi kwa mazoea na kwamba Kurugenzi yake imeanza kutayarisha na kuboresha namna ya kupima upimaji wa utendaji kazi wa kila mfanyakazi ili kuliletea shirika tija kubwa. 
Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Bw. Hamad Abdallah akikagua mradi wa nyumba za makazi unaotekelezwa na NHC eneo la Chatur wilayani Muheza leo.

Akizungumzia umuhimu wa kila mfanyakazi, amesema kuwa kila mfanyakazi anapaswa kutambua kuwa ana mchango na umuhimu mkubwa katika kuongeza tija kwa shirika. 

Ametolea mfano wa wafanyakazi wanaosimamia manunuzi kuwa wana dhamana kubwa ya kuhakikisha kuwa gharama za manunuzi ya vifaa vya ujenzi katika Shirika inakuwa chini ili kumudu ushindani katika soko.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news