MUDA NI MWALIMU MWEMA

NA LWAGA MWAMBANDE

INGAWA ni jambo ambalo limetuzunguka na wengi wetu tunalichukulia kuwa la kawaida, muda ni mojawapo ya nguvu za ajabu zaidi katika ulimwengu huu.

Kwa nini ni muhimu sana? Je, ni baadhi ya mambo gani ambayo kila mtu anapaswa kukumbuka anapofikiria kuhusu muda (wakati)?.

Ni kwa sababu,kila kitu katika ulimwengu huamuliwa au kuathiriwa na muda. Ndiyo maana mara nyingi kuna msemo ambao huwa unasisitiza kuwa, hakuna mwalimu mzuri hapa duniani kama muda.

Utafanya nini na muda uliopewa? Jibu la swali hili ni muhimu sana kwa sababu huwezi kupoteza muda hata kidogo unapotambua nafasi yako au kile ambacho unatarajia kukifanya kwa ustawi bora wa familia, jamii na Taifa kwa ujumla..

Watu mara nyingi hufikiria fedha kama rasilimali yao ya thamani zaidi, na ingawa ni kweli ni muhimu kwa sababu hukuruhusu kununua mahitaji au huduma unayohitaji,unaweza kutumia kiasi chochote na baadaye ukafanikiwa kurejesha kiasi hicho,lakini kwa upande wa muda mara tu unapopita, umekwenda na haurudi nyuma.

Kuna msemo wa kutia moyo ambao kimsingi unasema kwamba kila mtu ana saa 24 sawa kwa siku, hivyo hakuna mtu anayeweza kulalamika kwa kukosa muda wa mambo anayotaka kufanya.

Hata hivyo, ukweli ni kwamba ingawa kila mtu kiufundi ana saa 24 kwa siku, muda wa bure alionao hutofautiana sana. Ingawa mtu aliye na kazi nzuri ambayo ina saa za kawaida za kazi anaweza kutumia muda wa kutosha kufanya mazoezi ya ustadi, mtu anayehitaji kufanya kazi kwa saa nyingi zaidi ili kupata kiasi sawa hawezi.

Kwa maana hiyo, ingawa wote wawili wana saa 24 kwa siku, wanachopaswa kutambua ni kwamba muda ni mali. Sababu nyingine kwa nini muda ni muhimu sana ni kwamba hakuna mtu anayejua ni kiasi gani anacho.

Watu wanaweza kufa katika umri wowote na kwa sababu yoyote, na hakuna mtu anayeweza kutabiri wakati ujao. Kujua kutokuwa na uhakika huu kunaweza kuwa na athari kubwa juu ya jinsi unavyoishi maisha yako.

Kama wanadamu, tunafahamu hatua tatu za muda,muda (wakati) uliopita, wa sasa na ujao. Tunaweza kutumia yaliyopita kujifunza na tunaweza kujiandaa kwa ajili ya wakati ujao, lakini sasa ndiyo nafasi pekee tunayopaswa kufanya kazi.

Utafiti unaonesha kuwa, kuzingatia zaidi kinachoendelea sasa na kuishi sasa kunanufaisha kiakili na kimwili, afya na kiuchumi. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, muda ni mwalimu mwema,kwani unakuja tunasoma. Endelea;



1.Muda ni mwalimu mwema, unakuja tunasoma,
Na hauna uhasama, kuja unavyojituma,
Sawa na shamba kulima, mavuno yatasimama,
Wanasema itajenga, iache tuipe muda.

2.Kuna mahali twakwama, ni gari la kusukuma,
Badala ya kutuama, nguvu mpya twaazima,
Mengi huwa wanasema, siyo ziwa ni kisima,
Wanasema itajenga, iache tuipe muda.

3.Habari huwa zavuma, tunakosa kujituma,
Kwa jirani kunavuma, huku kwetu kwayoyoma,
Nasi hatutaki kwama, tunapenda kusimama,
Wanasema itajenga, iache tuipe muda.

4.Muda hautasimama, miaka itazizima,
Tutakuja kusimama, tuliyopata kupima,
Ama waweze kuvuma, vinginevyo kuwalima,
Wanasema itajenga, iache tuipe muda.

5.Wengine hawatahama, wanasubiri kugema,
Ikitokea kuzama, ufunguo wa kusema,
Matunda tukiyachuma, ni wa kwanza kutetema,
Wanasema itajenga, iache tuipe muda.

6.Muda wahenga wasema, hauwezi kutuama,
Tena hauna kugoma, ni jua kuchwa kuzama,
Ni ruksa kulalama, si tumepewa kusema?
Wanasema itajenga, iache tuipe muda.

7.Mipango iwekwe vyema, maandishi bila noma,
Ruvuma hadi Tunduma, waelewe wakisoma,
Ukakasi wote tema, maneno yaweza koma,
Wanasema itajenga, iache tuipe muda.

8.Wakati mwingine vema, taarifa kuzituma,
Kule ilifanya vema, hadi waliposimama,
Tuzidi kuwa salama, mawazo bila kukwama,
Wanasema itajenga, iache tuipe muda.

9.Maendeleo wasema, kulipia ni lazima,
Ni lazima kujituma, na kuingia gharama,
Vinginevyo tutakwama, kupanda huu mlima,
Wanasema itajenga, iache tuipe muda.

10.Muda nasi utasema, kama yetu ni salama,
Huo cheche utatema, endapo watatufuma,
Sijui hadi kiama, ndipo tutacheza ngoma?
Wanasema itajenga, iache tuipe muda.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

1 Comments

Previous Post Next Post

International news