Musoma Vijijini wazidi kutabasamu

NA FRSHA KINASA

SERIKALI ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan imeendelea kutoa fedha nyingi kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa shule katika Jimbo la Musoma Vijijini mkoani Mara.
Jimbo hilo ambalo linaongozwa na Mheshimiwa Prof.Sopeter Muhongo ambaye yupo mstari wa mbele kusimamia na kuchangia kwa hali na mali limeweka mkazo mkubwa katika ujenzi wa shule mbalimbali za sekondari ikiwemo maabara na maktaba.

Pia, Mheshimiwa Prof.Muhongo ametoa shukurani kwa Serikali kwa kutoa mchango wa shilingi milioni 573 ili kufanikisha ujenzi wa Sekondari ya Wanyere iliyopo jimboni hapa.Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini chini ya Prof.Muhongo leo Juni Mosi, 2023, imefafanua kuwa wameendelea kutatua matatizo yanayowakabili wanafunzi wanaosoma kwenye sekondari za kata za jimboni humo.
Miongoni mwa matatizo makuu yanayowakabili ni umbali mrefu wa kutembea kwenda masomoni,mirundikano ya wanafunzi madarasani,upungufu au ukosefu wa maabara za masomo ya sayansi,ukosefu wa maktaba na upungufu mkubwa wa walimu, hasa wa masomo ya Sayansi na Lugha.

Ujenzi wa Sekondari mpya Kijijini Wanyere

Aidha, kwa mujibu wa taarifa hiyo, Kijiji cha Wanyere ni moja ya vijiji vinne (Chirorwe, Kusenyi, Suguti na Wanyere) vya Kata ya Suguti yenye sekondari moja iliyoko kijijini Suguti
"Wanafunzi wa Kijiji cha Wanyere wanalazimika kutembea zaidi ya kilomita 30 kwenda na kurudi kutoka masomoni kwenye sekondari yao ya kata. Baadhi ya wanafunzi wamepanga vyumba (na wanajipikia) karibu na eneo la shule hiyo. 

"Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof Sospeter Muhongo alitembelea Kijiji cha Wanyere kwa malengo makuu mawili ikiwemo kupokea kero za wanakijiji na kuzitatua na kuhamasisha ujenzi wa sekondari mpya kijijini hapo."

Michango ya ujenzi wa Wanyere Sekondari

Mbunge Prof Muhongo aliendesha harambee ya kuanza ujenzi huo na michango iliyotolewa ni kama ifuatavyo:

Wanakijiji wa Wanyere wameanza kuchangia:

Nguvukazi za kusomba mchanga, mawe, maji na kuchimba msingi wa jengo moja la Madarasa 2 na Ofisi 1 ya Walimu ambapo fedha taslimu ni takribani shilingi milioni 2.5.

Wanakijiji wa Kataryo:

Aidha, kwa mujibu wa taraifa hiyo saruji mifuko 30 imetolewa na Kijiji jirani cha Kataryo cha Kata jirani ya Tegeruka. Watoto wa kijiji hiki jirani wanasoma kijijini Wanyere.

Mbunge wa Jimbo:

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof. Muhongo ameanza kutoa michango yake kwa kuchangia saruji mifuko 100.
Pia, wananchi wa Jimbo la Musoma Vijinini wameonesha matumaini makubwa kwa Halmashauri ya Musoma DC ambayo bado haijatoa mchango wowote, kwamba huenda wakafanya hivyo karibuni.


Serikali Kuu (TAMISEMI):

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) kupitia Bajeti ya Mwaka 2023/2024, Serikali itatoa shilingi Milioni 573 kupitia Mradi wake wa SEQUIP kwa ajili ya ujenzi wa Sekondari mpya Kijijini Wanyere. Hii itakuwa Sekondari ya pili ya Kata ya Suguti.

"Wananchi na Viongozi wa Jimbo la Musoma Vijijini wanaishukuru Serikali, chini ya uongozi mzuri wa Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuongeza ubora wa utoaji wa elimu jimboni mwao.
Picha zilizoambatanishwa katika habari hii zinamuonesha Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof Sospeter Muhongo akiwa na Wanakijiji kwenye Mkutano uliofanyika jana kijijini hapo kwenye eneo la ujenzi wa sekondari mpya, ambayo inajengwa ndani ya Kitongoji cha Mwikoro, Kijijini Wanyere, Kata ya Suguti, Musoma Vijijini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news