Mwinjilisti Temba afunguka kuhusu uwekezaji wa DP World nchini

NA DIRAMAKINI

MWINJILISTI wa Kimataifa, Alphonce Temba amepongeza hatua iliyochukuliwa na Serikali za kuridhia ushirikiano kati ya Tanzania na Serikali ya Dubai kuhusu masuala ya kiuchumi na kijamii kwa ajili ya uendelezaji na uboreshaji wa utendaji kazi wa bandari hapa nchini.

Dhima ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuridhia hatua hiyo inalenga kuboresha Sekta ya Bandari nchini ili kuongeza ufanisi na mchango wa sekta hiyo katika mapato ya nchi, ajira na kuchagiza ukuaji wa sekta nyingine za kiuchumi, ambapo ilionekana upo umuhimu wa kuendelea kushirikisha sekta binafsi katika shughuli za bandari nchini.

Temba amefafanua kuwa, "Kwanza kabisa nina uzoefu wa kuishi nchi 13, nchi zaidi ya saba zikiwa na bandari na nimekwenda kujihusisha kwenye masuala ya umishenari na hafla ya uzinduzi mbalimbali wa bandari zao.

"Nataka nizungumzie tu leo chache kule nchi ya Namibia ambako walikodisha bandari yao kwa Falme za Kiarabu. Nataka nizungumzie pia kule Australia wana bandari kubwa sana ambako nimekaa mwaka mzima nao wamekodisha bandari yao.

"Bandari hiyo imejikita pia katika mambo mawili ya tofauti pamoja na kukodishiwa kwa ajili ya kushusha shehena mbalimbali ambazo zinaingia katika nchi ya Namibia, lakini zinaingia pia katika sehemu ya Angola na ukijua Angola imegawanyika, kwa hiyo ziko sehemu nyingine zilikuwa haziwezi kupitika, lakini inahudumia sehemu ya Zambia. Botswana, Zimbabwe na sehemu za Mafikeng South Africa.

"Bandari ambayo pia pamoja na kuhudumia mizigo mingi, hiyo imekuwa ikishughulika na mambo ya uvuvi katika kina kikuu cha bahari kuvua samaki ambako wamekuwa wakifanya biashara ya kusindika pamoja kuchakata na kwenda kuuza Ulaya na Marekani.

"Lakini pamoja na hayo biashara ya samaki katika nchi ya Namibia wana Waziri Maalum wa Masuala ya Samaki anayejulikana kama Waziri wa Samaki na Uvuvi katika nchi ya Namibia na pia pamoja na hilo suala la uvuvi katika kina cha bahari wanajihusisha pia na masuala ya uchimbaji wa Almasi.

"Nchi ya Namibia almasi nyingi inachimbwa baharini na wanazo meli zaidi ya tano mpaka saba maalumu za kisasa ambazo zinafanya kazi ya uchimbaji wa almasi katikati ya kina cha bahari.

"Kwa hiyo kwa msingi huo Namibia ni nchi iliyojijenga sana katika ikizingatiwa kwanza Waafrika na wengi wa Wajerumani wamekaa kwenye nchi kwa muda mrefu na wameweza kuboresha kwa kiasi kikubwa sana nchi hiyo na wameweza kukodisha bandari yao kwa ajili ya kuongeza kasi ya utendaji.

"Hivyo basi napenda kusema kwamba ninao mtazamo wangu binafsi kama Mtanzania na maoni yangu juu ya sakata hili na kugusa maeneo mengi ambayo pamoja na mambo mengine hayaangaliwi.

"Ni kweli kabisa mikataba ni mizuri kuingalia na huwa inarekebishika nataka niwaambie Watanzania wenzangu. Hakuna mkataba ambao unaasilimia 100 ya usahihi hata ukiwepo mkataba huo, lazima baada ya miaka mitano tutaona mkataba huo una asilimia chini ya 50 ya usahihi.

"Mfano mkubwa ni suala la kuandikwa kwa katiba mpya, kitendo kilichofanyika huko nyuma mpaka rasimu ya Warioba ikatoka maoni ya wananchi yakatoka ni hakika sasa hivi Watanzania wengi wanaona kabisa yako mambo mengi kabisa kwa sasa yanapaswa kuingizwa kipindi kile hayakuingizwa ni kama chini ya asilimia 50 vinapaswa kuongezwa kwa sababu ya hali ya sasa ya nchi, hali ya sasa ya maisha na hali ya sasa ya kisayansi na kiteknolojia.

"Nina mawazo ya kusema kwamba Serikali imekuwa na mawazo ya mpango mzuri, ikumbukwe kwamba tuna mataifa zaidi ya 10 yanayotuzunguka, mataifa haya yalikuwa yakija kwa kasi kufanya biashara na Tanzania na Dar es Salaam.

"Na tumeona mfano huu kupitia mgomo wa Kariakoo wakati Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokwenda kutatua mgogoro ule walizungumza wafanyabiashara kadha wa kadhaa wakilalamika juu ya soko la Kibiashara la Kariakoo ambalo lilikuwa likiona wageni wengi kutoka nje, lakini wengi wamekata na wageni wale hawaonekani tena na masuala ya biashara yamekuwa magumu.

"Hii picha inatuonesha kwamba tuna upungufu mkubwa wa kuwapata wageni katika mataifa yanayotuzunguka kwa ajili ya kufanya manunuzi,na kufanya usafirishaji wa mali mbalimbali.

"Simaanishi kwamba wageni hawapo kabisa ila idadi imepungua kutokana na maelezo na malalamiko ya Watanzania waliyoyafikisha mbele ya Waziri Mkuu juu ya masuala ya biashara ya Tanzania somo la Kariakoo na bidhaa zinazoingia nchini.

"Hivyo basi nina uhakika kabisa suala hili la ukodishwaji wa bandari yetu ni suala muhimu sana na limekuja kwa wakati mzuri sana.

"Jambo ninalotaka kulizungumza ambalo halizungumzwi na watu wengi ni mawili, matatu ambayo ninaamini yangefanyika ama yangejulikana Watanzania wasingekuwa na mihemko mikubwa zaidi ya kuona kwamba suala hili ni zuri na kama kuna marekebisho basi yangefanyiwa kazi na sio 'kuattack' zoezi zima au mpango mzima wa ukodishwaji wa Bandari ya Dar es Salaam.

"Point yangu ya kwanza ni hii ya ukodishwaji unatakiwa kwa sababu, mkodishaji ambaye angekuja kufanya kazi pamoja na mambo mengine kuna vitu vya aina tatu au sifa anapaswa kuwa nazo.

"Namba moja,kuwezesha meli kubwa za kubeba mizigo kutoa huko iwe Uarabuni, Japan au China, iwe Uingereza iwe Ulaya iwe ni Marekani kuleta nchini.

"Namba mbili, kuwashawishi wananchi katika nchi husika ambazo zimetuzunguka kuja kufanya biashara au kushusha mizigo katika bandari yetu.

"Namba tatu, kuwa na mtaji nadhani usiopungua trilioni nne mpaka tatu kuendelea kuwekeza katika bandari zetu kwa hiyo vitu hivi vitatu kama kweli vipo Watanzania lazima tujue kwamba kwa nini Watanzania tunashindwa kwa sababu kutoa trilioni mbili au tatu katika bajeti yetu ya nchi tukaipeleka katika bandari na ikifanyika hivyo utatokea tena mgogoro mkubwa zaidi ya huo.

"Kwa hiyo Watanzania katika kuyajadili haya au kuyazungumza haya tunapaswa kuangalia sifa za ziada za kufanyika kwa ukodishwaji wa bandari yetu kwamba mtaji lazima uingizwe, wateja watafutwe na mizigo na usafiri lazima uwepo.

"Kama misingi hii au mambo haya yapo na yanatakiwa kufanyika kwa staili hii, Watanzania hatuna budi kuiunga mkono Serikali kwamba imekuja kwa wakati kufanya jambo zuri na serikali iboreshe machache yanayoonekana hayafai ili tuendelee vizuri na sio kukosoa au kuupinga mpango mzima kwamba haufai na usiwepo tutafanya kosa kubwa sana.

"Namba mbili ni juu ya suala la kibiashara katika zama za sasa hivi ambazo yanatakiwa kabisa yafanyike na sekta binafsi. Amerika yenyewe imekodisha baadhi ya bandari zake, imekodisha baadhi ya bandari zake kwa ajili ya kufanyika haya ninayoyazungunza.

"South Africa, Kenya na baadhi ya mataifa mengine yamefanya hivi kwa hiyo suala hili linaweza kuwa linatufaa sana kwa sasa kwa sababu ya kuendelea.

"Ikumbukwe Tanzania tumeanza kufanya kazi kubwa ya kutumia fedha nyingi za ndani kupanua kina cha bandari, kujenga barabara na kadhalika, na bandari kavu ya Kwala iliyochukua zaidi ya bilioni 83 ambazo zinatakiwa zirudi zifanye kazi katika mambo mengine ya barabara, madawa, madawati ya zahanati na uboreshaji wa maisha ya Watanzania.

"Hivyo basi, fursa hii ya bandari inatakiwa ifanyike kwa kiwango kingine kikubwa ambacho Watanzania tufike mahali si kukimbilia tu kuponda na kusema kwamba haviwezekani. Inatakiwa tuingie katika chalenges na kusema pia namna gani tunarekebisha baadhi ya mambo ambayo tunafikiri yawepo.

"Kwa kuwa Serikali haikuweza kufanya mapema awareness kwa Watanzania kwa ujumla ndio mihemko imekuwa mikubwa pamoja na mimi ninaye zungumza kupata hiyo.

"Lakini kutokana na uzoefu na exposure niliyonayo kwa mataifa mengine zaidi ya nchi 13 ninao ujasiri wa kuishauri Serikali maneno haya.

"Kwamba Serikali haijafanya makosa ila irekebishe makosa yaliyoko ndani ya mchakato huu hii itasaidia. Kwa sababu yamekwisha kutokea labda serikali ifanye vitu viwili au vitatu vya kusaidia.

"Ile tripu ya kwenda Dubai ya wabunge, ilipaswa Serikali ijiongeze iweze kuwaweka na wadau Watanzania kwenda kuona walichokiona wabunge.

"Na ndio maana wako watakaofikiria wabunge wamepewa bahasha, wapo watakaofikiria kuna vitu vimeuzwa, wengine watafikiria kuna mambo ya ufamilia na kadhalika na kadhalika kwa sababu bunge lilienda kushuhudia na limepitisha sheria.

"Kama inawezekana bado, uwezo mkubwa serikali upo wanaweza wakafanya wakatoa awareness wakachagua katika taasisi za dini baadhi ya viongozi wa dini, katika taasisi mbalimbali wakapata watu wasiopungua 50 au 30 wakawachukua viongozi wa dini, kwenye vyama vya siasa sita au saba, wakachukua wazee wa vijijini watatu au wanne wakaenda Dubai.

"Wengine Namibia wengine South Africa wengine Ghana mataifa kama matatu au manne wakashuhudia ufanisi wa kampuni hizi zinazopewa ndani ya miezi mitatu au minne hiyo route ikawarudisha hao viongozi wetu.

"Hata pia wanasheria wakachukuliwa, wanaharakati, kwa sababu hii keki ya bandari ya Tanzania si kwa ajili ya chama fulani bali kwa Watanzania wote. Mimi ninaamini ushauri wangu Serikali ikiufanyia kazi watu hawa wakapelekwa wakajionea kazi inayofanyika huko Dubai, Mombasa, Marekani wakarudi watakuwa walimu wazuri na bandari yetu itatumika vizuri na maisha yetu Watanzania yataboreka zaidi na zaidi.

"Nimeyatoa mawazo yangu haya kwa sababu ya exposure niliyonayo ya mataifa mbalimbali ambayo yana bandari yamefanikiwa kwa sababu ya kuweza kuingiza nguvu ya sekta binafsi kufanya kazi katika bandari zao.

"Jambo hili sio kwenye bandari pekee tumeona serikali ina mpango wa kutengeneza barabara ya mwendo kasi kutoka Kibaha mpaka Dodoma na tayari upimaji upo, Watanzania wengi wanakaribia kulipwa fidia kwa sababu ya ule mpango wa (PPP) kwa hiyo, ninaamini kwamba suala hili la urasimishaji wa sekta binafsi kuingia kusaidiana na serikali lipo katika mataifa mengi na katika nyanja nyingi ikiwepo barabara, uvuvi bandari na kadhalika.

"Na kadhalika kwa hiyo bado naipongeza serikali changamoto zilizopo zikatatuliwa, jambo hili halihitaji chama wala kampeni bali Watanzania wote,"amefafanua kwa kina Mwinjilisti Temba.

Bungeni

Juni 10, mwaka huu Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha azimio la kuridhia Mkataba baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kupitia Kampuni yake ya DP World kuhusu ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii ya Uendelezaji na Uboreshaji wa utendaji Kazi wa Bandari Tanzania.

Hatua hii ni baada ya kupokea mapendekezo ya Wawekezaji mbalimbali wakiwemo kampuni ya Hutchson (Hong Kong), Antewerp/Brugge(Belgium), PSA International (Singapore), DP World(Dubai), Abu Dhabi Ports(AbuDhabi), Adani Ports and Logistics(Mundra-India), Kampuni ya CMA-CGM(France) pamoja na Kampuni ya Maersk(Denmark).

Mkataba huo unatajwa kuleta manufaa katika kupunguza muda wa meli kukaa nangani kutoka siku 5 mpaka masaa 24 na kupunguza gharama za utumiaji wa Bandari na kufungua masoko ya kimkakati katika eneo la bidhaa na biashara ya usafirishaji ndani ya nchi na kanda jirani.

Akitoa maelezo ya awali kuhusu mapendekezo ya mkataba huo Waziri wa ujenzi na Uchukuzi Prof.Makame Mnyaa Mbarawa Mheshimiwa Spika,katika kupitia mawasilisho ya kampuni hizo pamoja na sifa zao kimataifa, Serikali iliamua kuanzisha majadiliano na kampuni ya DP World kwa kuzingatia uzoefu wake katika uendeshaji wa shughuli za bandari barani Afrika, Asia, Ulaya na Amerika ya Kaskazini na Kusini.

Ameeleza kuwa, kampuni hiyo ina uzoefu na utaalamu wa kuchagiza mnyororo mzima wa usafirishaji kutoka maeneo ambayo bidhaa zinatoka mpaka kufika kwa walaji na kueleza ameeleza kuwa uwekezaji huo utaongeza idadi ya meli zitakazokuja Bandari ya Dar es Salaam kutoka meli 1,569 zilizohudumiwa mwaka 2021/22 mpaka kufikia takriban meli 2,950 ifikapo mwaka 2032/33.

Hata hivyo Waziri huyo amebainisha kuwa muda wa ukomo wa mkataba utakaosainiwa haujawekwa wazi na badala yake Serikali imewaachia suala hilo wataalamu wa sheria za Uwekezaji.

“Tutaweka muda ukomo na muundo wa marejeo Kwa kupitia viashiria muhimu vya kiutendaji na ikiwa mwekezaji yeyote atashindwa kutekeleza majukumu yake tunaachana nae , hatuwezi kuwavumilia watu wasio na uwezo,”Amesema Waziri huyo.

Aidha ameeleza kuwa, muda wa ushushaji wa makontena utapungua kutoka siku 4.5 mpaka siku 2 ikiwa ni pamoja na kupunguza muda wa uondoshaji mizigo kutoka masaa 12 mpaka saa 1 kutokana na uboreshaji wamifumoya TEHAMA.

“Uwekezaji huu unatarajiwa kupunguza gharama ya usafirishaji wa mizigo kutoka nchi za nje kwenda nchi za Jirani, kwa mfano kutoka US$12,000 mpakakati ya US$6,000 na US$7,000kwa kash linalokwenda nchi ya Malawi, Zambia au DRC na kuleta watumiaji wengi kwenye Bandari ya Dar es Salaam,”amesema.

Waziri huyo ametaja manufaa mengine kuwa ni kuongezeka kwa shehena inayohudumiwa kutoka tani milioni 18.41 za mwaka 2021/22 hadi kufikia tani milioni 47.57 mwaka 2032/33, sawa na ongezeko la asilimia 158 na kuongezeka kwa mapato ya Serikali yatokanayo na kodi ya orodha inayokusanywa katika shehena inayopitishwa bandarini kutoka shilingi trilioni 7.76 za mwaka 2021/22 hadi shilingi trilioni 26.7 za mwaka 2032/33, sawa na ongezeko la asilimia 244.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news