NA DIRAMAKINI
RAIA wa Malawi wamesema, changamoto ndogondogo zinajitokeza kutokana na utekelezaji wa baadhi ya sheria nchini ikiwemo utekelezaji wa sheria inayoumiza pale lori la mafuta linapopata ajali au kugongwa na kumwaga mafuta huku likitozwa kiasi kikubwa cha fedha zikiweza kupatiwa ufumbuzi, Tanzania itaendelea kuwa kimbilio kwa wafanyabiashara wengi kutoka nchini humo katika kutumia bandari na kuja kuchukua bidhaa mbalimbali.
Hayo yamesemwa na mwakilishi wa Kampuni ya International Haulage Brokers iliyopo Chichiri jijini Blantyre nchini Malawi, Leyneck Manjandimo wakati akiwa na mfanyabiashara na Mwinjilisti wa Kimataifa, Alphonce Temba ambaye alifika katika bandari kavu ya Kwala iliyopo mkoani Pwani ili kujionea fursa na kuona namna ya kuwahamasisha Wamalawi kuleta magari yao kuja kuchukua bidhaa na mafuta nchini.
"Uongozi wa Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu ni thabiti sana, pia ni uongozi sikivu, tunaamini changamoto ndogondogo zilizopo zitafanyiwa kazi, na kwa vile rafiki yetu ndugu Alphonce Temba ameendelea kutupa imani kuwa, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia na uongozi wake watafanyia kazi changamoto hiyo, basi tutaendelea kuwa na imani.
"Awali, tulikata tamaa kabisa tukawa tunafikiria kuhamishia magari yetu yote katika Bandari ya Beira nchini Msumbiji, lakini wito wa mtumishi wa Mungu na maombi yake kwetu kuwa tuendelee kuwa na imani na Serikali ya Tanzania, basi tunavuta subira ili tuendelee kufanya biashara na Tanzania, Taifa lenye watu wenye upendo, mshikamano na amani imetawala kila kona."
Awali, mfanyabiasha na Mwinjilisti wa Kimataifa, Alponce Temba amesema, jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuboresha miundombinu mbalimbali na kuweka mazingira ya kuvutia katika uwekezaji zinaendelea kuwapa mwanga wafanyabiashara wengi kuona kuwa, Tanzania ni chaguo sahihi kwa ajili ya kufanya biashara na hata kutumia miundombinu ikiwemo bandari kwa ajili ya kupata huduma.
"Nimefika na rafiki yangu huyu kutoka nchini Malawi ambaye amekuja kutembelea Bandari ya Kwala na kuangalia viwanda ambavyo zaidi ya 200 vinajengwa karibu na Kwala.
"Wamalawi wapo tayari kufanya kazi na Tanzania, kuleta magari yao na anasema amefurahi kufika hapa Kwala, DP World anawajua pia, kwa sababu wapo nao kule Beira (Msumbiji) na wanafanya kazi nzuri sana, yapo magari zaidi ya 400 na kuna magari 200 yanakuja huku, nimejaribu kumbembeleza sana, yale magari 400 yaje huku Tanzania na 200 yaende kule Beira na nimewaomba waifanye Tanzania kuwa chaguo la kwanza.
"Kwa hiyo, ninaamini baadhi ya changamoto ambazo alizisema awali kuhusu sheria ya kodi kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inayotozwa kwa magari ya mafuta yanayopata ajali na kumwaga mafuta barabarani ikipatiwa ufumbuzi tutawavutia zaidi."