Naibu Waziri Ndejembi atoa onyo ujenzi wa shule mpya

NA JAMES MWANAMYOTO
OR-TAMISEMI

NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema ofisi yake haitomvumilia mhandisi, afisa elimu au yeyote atakayekwamisha utekelezaji wa ujenzi wa shule mpya za sekondari za bweni za wasichana kupitia Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) awamu ya kwanza na ya pili, ambao ni matokeo ya jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyedhamiria kuendelea kuboresha miundombinu ya elimu nchini. 
Sehemu ya Wakuu wa Idara za Elimu wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Deogratius Ndejembi wakati akizungumza nao kwenye kikao kazi kilicholenga kuhimiza uwajibikaji katika usimamizi wa utekelezaji wa ujenzi wa shule mpya za sekondari za bweni za wasichana kupitia mradi wa kuboresha elimu ya sekondari (SEQUIP).

Mhe. Ndejembi onyo hilo mkoani Tabora, wakati wa kikao kazi chake na Wakuu wa Idara za Elimu kilicholenga kuhimiza uwajibikaji katika usimamizi wa mradi huo wa SEQUIP unaotekelezwa kwenye halmashauri 26 ikiwa ni moja katika kila mkoa.

“Niwawahikishia kuwa, hatutamvumilia yeyote atakayecheza na fedha za utekelezaji wa mradi huu kwasasabu atakuwa anachezea fedha za Rais Samia Suluhu Hassan, na wala sitarajii kusikia REO na DEO wanavutana au REO na RAS wanavutana,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Aidha, Mhe. Ndejembi amewataka watendaji hao kuwapatia kazi watu wenye uwezo wa kutekeleza ujenzi wa mradi huu kwa wakati, ili wanafunzi wanufaike na miundombinu iliyojengwa kwa jitihada za Serikali.

“Bilioni 3 kwa kila halmashauri katika halmashauri 26 ni fedha nyingi, hivyo ni lazima mumpe kazi mtu mwenye uwezo wa kukamilisha mradi kwa wakati na si kumpatia mtu kwa upendeleo wa aina yoyote,” Mhe. Ndejembi amehimiza.

Sanjari na hilo, Mhe. Ndejembi amewasitiza watendaji hao kuzingatia sheria, kanuni, taratibu, miongozo katika mchakato wa kuwapatia kandarasi wajenzi wa mradi huu, ili kupata watu sahihi watakaojenga miundombinu imara yenye kulingana na thamani ya fedha iliyotolewa. 
Naibu Katibu Mkuu (Elimu) Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dkt. Charles Msonde akisisitiza jambo kwa Wakuu wa Idara za Elimu wakati wa kikao kazi cha Mhe. Deogratius Ndejembi na wakuu hao wa idara kilicholenga kuhimiza uwajibikaji katika usimamizi wa utekelezaji wa ujenzi wa shule mpya za sekondari za bweni za wasichana kupitia mradi wa kuboresha elimu ya sekondari (SEQUIP).

Akizungumzia idadi ya mikoa iliyonufaika na mradi huu, Naibu Katibu Mkuu (Elimu) Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dkt. Charles Msonde amesema, Mhe. Rais ameshatoa fedha za ujenzi shule hizo 26 katika halmashauri 26 ambapo awali alianza na halmashauri 10 na sasa amemalizia halmashauri 16, hivyo kupelekea mikoa yote 26 kunufaika kwa halmashauri moja kupata bilioni 4.1 ikijumuisha awamu ya kwanza na ya pili ambapo kumekuwa na nyongeza ya milioni 100 kutokana na kuongezeka kwa gharama za ujenzi.

Dkt. Msonde amesema, halmashauri zote 16 zinanufaika na fedha za mradi huu kwa kujenga shule zenye jengo la utawala, madarasa, maabara, vyoo, chumba cha jenereta, bwaro, nyumba za walimu, mabweni, chumba cha wagonjwa, mitaro ya maji, vichomea taka, uzio, chumba cha TEHAMA, maktaba, pamoja na matanki ya maji ya ardhini na ya plastiki.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news