Papa Francisko aruhusiwa kutoka hospitali

NA PADRE RICHARD MJIGWA
C.PP.S,

TANGU alipofanyiwa upasuaji mkubwa Jumatano tarehe 7 Juni 2023 afya ya Baba Mtakatifu Francisko imeendelea kuimarika zaidi, kiasi kwamba, madaktari baada ya uchunguzi wa kina, Ijumaa tarehe 16 Juni 2023 wamempatia kibali cha kutoka katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli, iliyoko mjini Roma, ili kuendelea na maisha na utume wake kama kawaida.
▪︎Dominika tarehe 18 Juni 2023 anatarajiwa kuongoza Tafakari na Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na kwamba, ratiba ya mikutano yote iliyopangwa itatekelezwa isipokuwa Jumatano tarehe 21 Juni 2023, Baba Mtakatifu Francisko hataweza kutoa Katekesi yake kwa wageni na mahujaji mjini Roma, ili kumpatia nafasi ya kuendelea kuimarisha afya yake.

Professa Sergio Alfieri ambaye amekwisha mfanyia Baba Mtakatifu Francisko upasuaji mkubwa mara mbili amewaambia waandishi wa habari kwamba, afya ya Baba Mtakatifu inaendelea kuimarika zaidi, kuliko alipolazwa kwa mara ya kwanza mwaka 2021 na sasa hii ya tarehe 7 Juni 2023.

▪︎Baba Mtakatifu mara baada ya kutoka hospitalini, wazo lake la kwanza limewaendea wakimbizi na wahamiaji 80 waliozama na kufa maji baharini huko Pylos nchini Ugiriki, idadi ya watu waliopoteza maisha inaendelea kuongezeka na kwamba, waliokolewa ni watu 104 wakati ambapo mashua kutoka Libya ilikuwa imebeba abiria 750, wengi wao wakiwa ni wakimbizi na wahamiaji kutoka Siria, Pakistani na Misri. Hii ni ajali mbaya zaidi kutokea, ukiacha ile iliyotokea mwezi Aprili 2015. 

▪︎Mashirika ya misaada kwa wakimbizi yamezitupia lawama nchi za Ugiriki, Malta na Italia kwa kushindwa kutoa ushirikiano wa kutosha ili kuokoa maisha ya wakimbizi na wahamiaji hawa.

Kimsingi, “Global Compact 2018” yaani “Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji wa mwaka 2018” unapania pamoja na mambo mengine kukomesha ubaguzi na maamuzi mbele; kuongeza fursa za ushirikishwaji wa wahamiaji katika maisha ya nchi wahisani; kupunguza gharama za kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news