Prof.Bisanda: Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kujenga makao makuu Dodoma

NA MWANDISHI WETU

CHUO Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kinatarajia kujenga Makao Makuu yake katika Makao Makuu ya nchi Dodoma katika eneo la ekari 60 Msalato jijini Dodoma.
Hayo yamesemwa na Makamu Mkuu wa OUT, Prof.Elifas Tozo Bisanda katika ziara ya wajumbe wa Baraza la Chuo walipotembelea eneo hilo leo Juni 22, 2023. 

Prof.Bisanda amesema,"kutolewa kwa eneo hilo la ujenzi wa Makao Makuu ya OUT ni kufuatia maelekezo ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango aliyoyatoa kwa Mkurugenzi wa jiji la Dodoma kutoa ardhi ya kutosha kwa OUT kujenga Makao Makuu yake.
"Hatua za mwisho za OUT kumilikishwa eneo hili zinaendelea na baada ya hapo ujenzi utaanza kwa fedha kutoka serikalini, wadau wa elimu na OUT kufanya jitihada za kujiongeza."

Aidha, Prof. Bisanda ameishukuru ofisi ya Mkurugenzi wa jiji la Dodoma kwa kutekeleza ahadi na maelekezo ya Makamu wa Rais Mhe.Dkt. Mpango aliyoyatoa tarehe 12/12/2022 katika ziara yake aliyoifanya OUT.
Nao wajumbe wa baraza kwa umoja wao, wamefurahia sana kufika na kuliona eneo hilo na kuuelekeza uongozi wa chuo kuhakikisha hatua za umilikishwaji zinakamilika mapema iwezekanavyo. 

Vile vile wajumbe wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia OUT eneo la kujenga Makao Makuu yake Dodoma na kwamba hili ni jambo kubwa sana kwa maendeleo ya nchi yetu.
Akizungumza kwa niaba ya wajumbe wa Baraza Prof. Suleiman Ngware amesema: "Tunaishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutupatia eneo hili la ujenzi wa Makao Makuu ya Chuo chetu hapa Dodoma. 

"Ni heshima kwa OUT kuwa na Makao Makuu Dodoma kwa sababu hiki ndicho Chuo ambacho kina vituo nchi nzima na hapa Dodoma ndipo Makao Makuu ya Nchi. 
"Pia, OUT ni chuo cha kimkakati ambapo kuanzishwa kwake ni kwa ajili ya kuwafikia watu wengi kule walipo wakiwa kazini na katika biashara na shughuli zao, kikiwa na Makao Makuu Dodoma kinajenga taswira hiyo kwa ukamilifu wake."
Wajumbe wa Baraza la Chuo wapo jijini Dodoma kwa ajili ya kikao cha Baraza cha 116 kitakachofanyika tarehe 23/06/2023 katika kituo cha OUT Dodoma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news