NA DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi ameiagiza kamati ya kuzuia udhalilishaji wa kijinsia Zanzibar, iangalie suala la matumizi na athari za mitandao kwa vijana ili serikali ijipange vyema na kwenye mwelekeo wa uhuru wa matumizi hayo kwa Zanzibar.
Dkt.Mwinyi ameyasema hayo kwenye hafla ya uzinduzi wa kamati ya kuzuia udhalilishaji wa kijinsia Zanzibar huko ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul Wakili, Kikwajuni Wilaya ya mjini.
Amesema, mitandao inapotumiwa vibaya ni kishawishi kimojawapo cha mmong’onyoko wa maadili na vitendo vya udhalilishaji.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiwa na mkewe Mama Mariam Mwinyi akiondoa pazia kuashiria kuzindua Kamati ya Kuzuia Udhalilishaji wa Kijinsia Zanzibar (kushoto ) Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar, Mhe.Mgeni Jailani Jecha na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Sheria, Katiba,Utumishi na Utawala Bora Zanzibar Mhe. Haroun Ali Suleiman. (Picha na Ikulu).
“Naiagiza kamati hii ifanye kazi ya kuchunguza athari za matumizi ya mitandao ya kijamii na ongezeko la kesi za udhalilishaji, baada ya kufanya kazi hiyo, itoe ushauri na mapendekezo serikalini ili tuwe na muelekeo bora zaidi juu ya uhuru na matumizi ya mitandao hapa Zanzibar,”aliagiza Rais Dkt.Mwinyi.
Alieleza furaha yake kuona kamati hio imeundwa ikiwa na lengo la kuzuia matukio ya udhalilishaji kabla ya kutokea, badala ya kupambana nayo yakiwa yameshaathiri jamii.
Aidha, Rais Dkt.Mwinyi aliitaka kamati hiyo iangalie mapungufu ya Kisera, Sheria na Kanuni yaliopo ili watoe mapendekezo sambamba na kuweka malengo ya kimkakati yatakayowawezesha kufanya kazi kwa kasi na haraka zaidi.
“Kwa vile ndani ya kamati hii, wamo viongozi na wajumbe kutoka taasisi za elimu ya sekula na elimu ya dini, ninayo matumaini kwamba kamati hii itakuja na mapendekezo yatakayohusisha mitaala pamoja na uendeshaji na usimamizi mzuri wa skuli, madrasa na maeneo mengine yanayotoa mafunzo ya dini,”amesisitiza Rais Dkt.Mwinyi.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt.Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inafarijika kuona jamii imesimama pamoja kuunga mkono juhudi za Serikali kivitendo.
“Sote tunasimama pamoja kupiga vita janga la udhalilishaji wa watoto na unyanyasaji wa kijinsia. Hii ni ishara kwamba sote tunaguswa na uzito wa janga hili kwa kuzingatia madhara yake. Endapo vitendo hivi tutashindwa kuwa na mbinu mwafaka za kuvikabili, jamii yetu itakuwa na idadi kubwa ya washtakiwa wa makosa ya udhalilishaji,”. amesema Rais Dkt.Mwinyi.
Ameongeza kuwepo kwa tatizo la idadi kubwa ya watu wanaofungwa kwa kesi za udhalilishaji inaifanya jamii yetu kuwa na familia zinazokosa matunzo, hali aliyoieleza kusababisha mifarakano na kusalia kuwepo kwa kundi kubwa la watoto wanaokosa usimamizi wa familia zilizo madhubuti.
Hivyo, aliwataka wazazi na walezi wajitahidi kusimamia vyema maadili, hulka na silka za vijana wao na kuhakikisha wanawalinda na kuwawekea mipaka sahihi kwa kutowapa uhuru sana pamoja na kufuatilia mabadiliko ya tabia na mienendo yao ya kila siku kwani kesi nyingi za udhalilishaji wa kijinsia zilizopo kwenye vyombo vya sheria zinawahusisha vijana.
Alisema watoto na vijana wanaofanyiwa udhalilishaji huathirika kiafya na kisaikolojia, hali aliyoieleza kuchangia kuharibu mipango na muelekeo wao wa maisha.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Zanzibar,Mheshimiwa Haroun Ali Suleiman alisema kazi ilio mbele yao kamati aliyoizundua Rais Dkt. Mwinyi ni utekelezaji wa vitendo katika juhudi za kumuungamono Rais katika mapambano dhidi ya udhalilishaji Zanzibar.
Naye Mkurugenzi wa Mashitaka Zanzibar,DPP Mgeni Jailani Jecha alisema vitendo vya udhalilishaji wa kijinsini vinazidi kuongezeka nchini badala ya kupungua.Alieleza kwamba, vinaweza kuimaliza jamii, jambo ambalo linazidi kuleta hofu na kutia dosari taifa.