NA GODFREY NNKO
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan ameipongeza Klabu ya Yanga ya jijini Dar es Salaam kwa kulipa Taifa heshima kubwa kupitia michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika (CAF Confederation Cup).
Pongezi hizo zinakuja baada ya saa chache kupita huku Yanga SC ikionesha soka la aina yake usiku wa Juni 3, 2023 kuamkia leo Juni 4, 2023 katika fainali za kombe hilo huko Uwanja wa du 5 Juillet, Algiers nchini Algeria.
"Hongereni sana Yanga kwa hitimisho la mchezo wa Fainali ya Kombe la Shirikisho (CAF Confederation Cup). Historia mliyoandika katika safari yenu ya michuano hii ni kubwa na ya heshima kwa Taifa letu. Nawatakia kheri katika mipango yenu ya siku zijazo,"ameeleza Rais Dkt.Samia kupitia mitandao yake rasmi ya kijamii.
Licha ya juhudi kubwa zilizofanywa na Yanga SC katika michuano hiyo, hawakufanikiwa kutwaa taji hilo badala yake USM Alger ya Algeria ndio walitawazwa kuwa mabingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika 2022/23.
Ni kwa faida ya goli la ugenini licha ya kupoteza kwa goli 1-0 dhidi ya Yanga katika mchezo wa fainali ya pili iliyopigwa unjani hapo, ukitanguliwa na ule wa awali katika Dimba la Bejamini Mkapa jijini Dar es Salaam.
Goli pekee la beki Djuma Shabani akifunga kwa penati halikutosha kuipa ubingwa, Yanga ambayo ilipoteza kwa magoli 2-1 katika mchezo wa kwanza uliochezwa hapa nchini.
Aidha, licha ya matokeo hayo, Yanga imetoa mfungaji bora wa michuano hiyo ambaye ni Fiston Mayele aliyefunga magoli saba.
Katika hatua nyingine Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kesho tarehe 5 Juni, 2023 ameialika timu ya Dar es Salaam Young Africans (Yanga) kwa chakula cha jioni Ikulu, Jijini Dar es Salaam kwa lengo kuipongeza kwa kufanya vizuri katika michuano ya soka ya kugombea Kombe la Shirikisho Barani Afrika iliyohitishwa jana Jijini Algers, Algeria.
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema Rais Samia amewapongeza Yanga kwa kucheza vizuri katika mchezo wa pili wa fainali hapo jana kwa kuwafunga wenyeji wa mchezo huo bao 1-0 na hivyo kuwa na matokeo ya jumla ya mabao 2-2 japokuwa hawakufanikiwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika kutokana na kuruhusu kufungwa mabao 2-1 katika mchezo wa kwanza wa fainali uliofanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam Tarehe 28 Mei, 2023.
Msigwa amebainisha kuwa, pamoja na kutotwaa ubingwa, Mhe. Rais Samia anatambua kuwa Yanga wameipa heshima kubwa Tanzania na anawapongeza Wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wa timu hiyo ambao ni Mabingwa wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara.
Timu ya Yanga, viongozi na mashabiki wanatarajiwa kurejea hapa nchini baadaye leo kwa ndege iliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono timu hiyo iliyokuwa ikiiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Kimataifa.
Kombe la Shirikisho la CAF ni mashindano ya kila mwaka ya vilabu vya soka yaliyoanzishwa mwaka 2004 kwa muunganisho wa Kombe la CAF na Kombe la Washindi wa Kombe la Afrika na kuandaliwa na CAF.
Timu iliyofanikiwa zaidi katika mashindano hayo ni Club Sportif Sfaxien kutoka nchini Tunisia ikiwa na mataji matatu.