Rais Dkt.Samia, Prof.Mkenda wamlilia bosi wa Precision Air, Michael Ngaleku Shirima

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan ameeleza kupokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha mmiliki wa Kampuni ya Ndege ya Precision Air, Michael Ngaleku Shirima amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 80.

Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ameeleza hayo kupitia taarifa fupi aliyoitoa katika mitandao yake ya kijamii leo Juni 10, 2023.

"Nimepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Michael Ngaleku Shirima, mwanzilishi na Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Precision Air.

"Baada ya utumishi wake kwa umma, kwa zaidi ya miaka 30 amekuwa sehemu muhimu katika biashara ya anga na shughuli za kijamii katika nchi yetu. Natoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki. Mwenyezi Mungu amweke mahali pema. Amina,"amefafanua Mheshimiwa Rais Dkt.Samia.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Juni 10 na Shirika la Ndege la Precision Air imesema, mzee Shirima amefariki saa tatu usiku Juni 9, 2023 katika Hospitali ya Agha Khan jijini Dar es Salaam alikokuwa amelezwa tangu Juni 8, 2023 akipatiwa matibabu.

Wakati huo huo,Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,Mheshimiwa Profesa Adolf Mkenda (Mb) naye ameonesha kusikitishwa na kifo cha mzee Shirima huku akisisitiza kuwa, yapo mengi ambayo ameyaacha kwa ajili ya kujifunza kwa kizazi cha sasa na kijacho.

"Taarifa za kifo za Mzee Shirima, zimenisikitisha mno na nimeumia sana kwa kuondokewa na mzee wetu, hatuwezi kubadilisha au kufanya chochote, lakini maisha yake tuyatumie kama somo zuri sana kwa vijana na watu wote kwa bidii zake za kazi," amesema Profesa Mkenda

"Mzee Shirima ni mtu aliyefanya makubwa katika nchi hii na kuna mambo mengi ya kujifunza kutoka kwake, ukisoma historia yake na bahati nzuri hivi majuzi tu kaandika kitabu na kimezinduliwa, kinachoitwa "On my father's wings" utajifunza mambo mengi kuhusu maisha yake na kwamba alikuwa ni mtu wa aina gani,"amefafanua Prof.Mkenda.

Profesa Mkenda amesema Mzee Shirima amekuwa ni mpambanaji wa kihistoria na hata alipoacha kazi Shirika la Ndege la Air Tanzania alifanya biashara ya kuchoma nyama, baadaye aliendesha malori kwenda Mwanza na alipambana mpaka alipoanzisha shirika hilo la ndege.

"Michael Shirima alikuwa akifanya kazi shirika la ndege la Air Tanzania, alivyoona uongozi hauendi vizuri wakati ule alijiuzulu kazi mapema sana akiwa na umri mdogo.

“Baada ya kutoka hapo alifanya kazi ya kuchoma nyama, akaanza kuendesha malori kwenda Mwanza akapambana mpaka baadaye akafika mahali akaweza kuendesha shirika la ndege la mtu binafsi ambayo ni kati ya mashirika makubwa sana hapa Afrika,"Waziri Prof.Mkenda ambaye pia ni Mbunge wa Rombo mkoani Kilimanjaro amefafanua huku akisema kuna mengi mzee huyo aliyoyafanya wilayani Rombo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news