Rais Dkt.Samia:Serikali itajenga maghala ya chakula nchi nzima

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan amesema Serikali imepanga kununua chakula na kuweka akiba katika maghala kwa kiasi cha tani laki tano kwa mwaka huu ikilinganishwa na tani laki mbili na hamsini kwa mwaka uliopita.

Mheshimiwa Rais Samia ameyasema hayo leo katika Tamasha la Utamaduni la Bulabo ambalo ni sherehe za kumshukuru Mungu kwa mavuno lililofanyika katika uwanja wa Red Cross Ngomeni uliopo Kisesa.

Aidha, Rais Samia amesema Serikali itajenga maghala ya chakula katika kila mkoa ili kuweza kuhifadhi chakula kitakachoweza kuhudumia wananchi katika kila mkoa.

Rais Samia pia amesema Serikali imejipanga kuhakikisha nchi inakuwa na chakula cha kutosha kwa kuongeza matumizi katika sekta ya chakula ikiwemo kuongeza fedha kwenye bajeti ya kilimo ili wananchi waweze kuzalisha ziada ya chakula.

Vile vile, Rais Samia amesema Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kujenga skimu za umwagiliaji ili wakulima walime na kuvuna mara mbili kwa mwaka badala ya kutegemea mvua.

Kwa upande mwingine, Rais Samia amewataka Machifu kuhamasisha wananchi kufanya kazi na kuchangia katika shughuli za maendeleo ili kujenga taifa bora.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news