RC Makalla atoa agizo wizi wa vifaa Buchosa

NA MWANDISHI WETU

MKUU wa Mkoa wa Mwanza, Mhe.CPA Amos Makalla amemuagiza Katibu Tawala Mkoa kuunda kamati itakayofuatilia vifaa tiba kwenye vituo vya kutolea huduma za afya Buchosa kufuatia tuhuma za kupotea na kurejeshwa kwa 'Ultrasound' kwenye hospitali ya halmashauri hiyo.
Mhe. Makala ametoa agizo hilo mapema leo Juni 5, 2023 katika nyakati tofauti wakati akizungumza na Viongozi na Watendaji wa Halmashauri za Buchosa na Sengerema akiwa ziarani kujitambulisha wilayani humo na akamtaka Mkuu wa Wilaya kuwachukulia hatua watakaobainika kuhusika na wizi wa kifaa hicho kinachogharimu takribani Milioni 80.

Aidha, CPA Makalla amekemea tabia ya watendaji kukaa na fedha za mapato bila kupeleka benki na kusababisha matumizi ya fedha mbichi jambo ambalo linaitia doa halmashauri za Wilaya hiyo hadi kupelekea kupata hoja wakati qa ukaguzi wa hesabu za Serikali kama alivyobainisha kuwa kwa mwaka 2022/23 kumekua na hoja 30 Buchosa.

"Pelekeni fedha Benki msikae nazo ndani baada ya kukusanya nami kwa kutumia mfumo wa mapato wa Tausi nitawaona mnakusanyaje kila siku na nani ana pesa hajapeleka Bank na nitalirekebisha hili hivyo ni lazima mbadilike na ndio maana kwenye ripoti ya CAG mmetajwa kwa kutopeleka Bank fedha zaidi ya milioni 30 ndani ya mwaka uliopita,"amesema.

Vilevile, amewataka watendaji kusimamia miradi ya Maendeleo vizuri kwa kushirikiana na waheshimiwa Madiwani na kuhakikisha wanajibu hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) kwa wakati na kufanya kazi kwa uadilifu ili kulinda rasilimali za nchi zisipotee.
Aidha, ametoa onyo kwa tabia ya baadhi ya viongozi wa Dini wanaowahubiria wananchi kuamini Imani kali ambazo hazina uhalisia ambapo ametolea mfano kwa tukio la hivi karibuni la vifo vya Watoto wawili pamoja na wengine 13 kutotibiwa kutokana na kutofikishwa hospitali kupata matibabu ya ugonjwa wa Surua huku wakiaminishwa kupona kwa maombi.

"Tuepuke imani kali za namna hii tutaangamia, tutumie wataalamu wetu wa afya kwenye Zahanati na vituo vya Afya vilivyo kwenye maeneo yetu tunayoishi na sio kuwasikiliza watu wengine wenye nia ya kujinufaisha kwa namna yoyote,"amesisitiza Mheshimiwa Makalla.

Kwa upande mwingine, Mhe. Makalla amebainisha kuwa ifikapo mwezi Agosti mwaka huu Serikali inakwenda kujenga barabara yenye urefu wa Kilomita 56 ya Sengerema- Buchosa kwa kiwango cha lami kwa zaidi ya Bilioni 70 ikiwa ni Muendelezo wa hatua za Mhe. Rais Samia katika kuwahudumia wananchi.

"Nataka niwahakikishie kwamba barabara ya kutoka sengerema kuja Buchosa itaanza kujengwa rasmi niwaombe viongozi wote wa kata zote mtoe ushirikiano mtakapopitiwa katika maeneo yenu ili mwezi wa nane mkandarasi aanze ujenzi rasmi." Mhe.Makalla amesema.
Akizungumzana viongozi na watendaji wa Sengerema, Mhe. Makalla ametoa wito kwa viongozi wa siasa, viongozi wengine na watendaji kushirikiana katika kufanya kazi kwani anaamini kuwa Maendeleo thabiti hupatikana pahala kwenye mahusiano thabiti.

Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Mhe. Senyi Ngaga amesema kwa Mwaka wa fedha 2022/23 Halmashauri ya Buchosa imekusanya jumla ya Bilioni 2.2 kati ya Bilioni 3.1 inayokusudiwa ambayo ni sawa na asilimia 76 na kwamba wamekuja na mikakati kabambe ya kuhakikisha wanafikia lengo katika ukusanyaji mapato. Ameongeza kuwa kwa upande wa kodi kupitia Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) wamevuka lengo kwa kukusanya kwa zaidi ya asilimia 100.

"Sisi tunamshukuru sana Mhe. Rais, tuna miradi mingi ambayo inakwenda kuifungua Sengerema kama vile mradi wa Daraja la Kigongo-Busisi ambalo kukamilika kwake kutaiweka Sengerema kwenye sehemu ya juu sana na tutahakikisha tunahimarisha makusanyo ya Mapato ya ndani ambayo hadi sasa kwa Halmashauri ya Sengerema tumekusanya kwa asilimia 85," amesema Mhe. Ngaga.
"Kwa upande wa shule za msingi, tunahitaji vyumba vya madarasa Elfu 2 na tunavyo 800 na kufanya kwa Halmashauri ya Buchosa kuwa na upungufu wa vyumba elfu 16 ila tunamshukuru Mhe. Rais kwa kutuletea fedha kujenga Miundombinu ya Madarasa, Shule Mpya pamoja na ukarabati wa madarasa na kwa upande wa Sekondari hatuna upungufu,"amesema Mhe.Ngaga.

Aidha, Mhe. Mkuu wa Wilaya amebainisha kuwa wilaya hiyo inatarajia kuvuna zaidi ya Tani 5146 za Pamba na kwamba tayari Makampuni Saba yameonesha nia ya kununua na kwenye Sekta ya Uvuvi amemhakikishia Mhe. Mkuu wa Mkoa kuwa wataendelea kukusanya Mapato kwa zaidi ya 35% ikiwa ndio tegemeo kubwa.
"Kwenye Halmashauri yetu ya Buchosa tunatekeleza miradi kwa mfumo wa 'force acct' ila kamati za ujenzi hazifanyi vema na inatoa ishara ya miradi kutekelezwa vibaya sasa tunaomba kama miongozo ya kusimamia miradi umebadirika basi tupewe taarifa ili tusimamie ipasavyo,"amesema Augustine Makoye, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Sengerema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news