NA MWANDISHI WETU
MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Mheshimiwa Rosemary Senyamule amemtembelea na kumjulia hali,Bi. Witness Mkuvalwa (mkazi wa Iringa) anayesadikiwa kumwagiwa kimiminika chenye kemikali na kulazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kwa uangalizi na matibabu.
Senyamule amemtembelea, Bi. Witness leo Juni 30,2023 na kuahidi kushirikiana na Vyombo vya Ulinzi na Usalama vya Mkoa katika kuhakikisha anayetuhumiwa kuhusika na kitendo hicho anachukuliwa hatua na majeruhi wa tukio hilo anapata haki yake.
Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali hiyo, Dkt. Baraka Mponda amekiri kumpokea Bi.Witness Mkuvalwa jumatano ya Juni 28 mwaka huu ambapo tukio la kumwagiwa kimiminika hicho lilitokea katika Stendi kuu ya Mabasi ya Nanenane jijini Dodoma.
Katika kuhahikikisha Bi. Witness anarejea katika hali yake ya kawaida madaktari bingwa wa macho,pua, koo na ngozi wamempima mgonjwa huyo na kuthibitisha hakupata madhara makubwa hivyo ataendelea vizuri kutokana na Matibabu anayopatiwa.
Mhe.Senyamule pia alipata fursa ya kuwatembelea wagonjwa wengine katika wodi mbalimbali wakiwemo majeruhi wa ajali ya Moto waliolazwa katika Hospitali hiyo.