NA MWANDISHI WETU
MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Mhe.Rosemary Senyamule amewaasa viongozi na watumishi wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) Mkoa wa Dodoma kushirikiana na viongozi wa Halmashauri na Jiji la Dodoma katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato kwa asilimia 100 kabla ya kumalizika kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023.
Wito huo ameutoa leo Juni 3, 2023 katika kikao kazi kilichowahusisha watumishi na viongozi wa TRA, wakurugenzi wa halmashauri zote za Mkoa wa Dodoma, wakuu wa wilaya pamoja na wakuu wa idara mbalimbali wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa. Kikao hicho kimefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi hiyo Jengo la Mkapa.
"Lengo letu ni kufikia asilimia 100 ya mapato kama Mkoa lakini hadi Leo tumefikia asilimia 78 kwahiyo tumebakiza asilimia 22 tunajua ni kazi kubwa lakini ndani ya mwezi huu mmoja tunatakiwa kukamilisha,tusikwamishe Bajeti zetu au za Serikali kwa kutofikisha Bajeti ambazo zimeshapigiwa hesabu na Serikali.
"Tunajua Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akihimiza suala la Ukusanyaji wa Mapato lakini anahimiza kwa staili ya kuheshimu wale watu ambao wanatoa ushuru, ni watu muhimu kwahiyo tutumie lugha za staha ambazo wanaweza kuelewa, tusitumie nguvu na kuwafanya wachukie Serikali na kufanya biashara katika nchi yetu,"amesema Senyamule.
Aidha, Mhe. Senyamule amesema lengo la Mkoa wa Dodoma kwa sasa ni kupata wawekezaji wapya wa nje na ndani ya mipaka ya Tanzania ili kuimarisha na kukuza uchumi wa nchi na amewaasa sekta binafsi kuja kuwekeza jijini humo kwani fursa zipo.
Naye Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Bw. Ally Gugu amemshukuru Mkuu huyo wa Mkoa kwa kuandaa kikao kazi hicho kwani kimeongeza chachu na Ari ya viongozi na Watumishi kuwa wabunifu katika suala la Ukusanyaji mapato kwa Mkoa na anatarajia mabadiliko makubwa ya ukusanyaji mapato kwa Dodoma kama Makao ya Nchi.