RC Senyamule: Serikali imedhamiria kuimarisha Sekta ya Kilimo

NA MWANDISHI WETU

MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Mheshimiwa Rosemary Senyamule amesema Serikali imedhamiria kuimarisha sekta ya kilimo kwa kujenga na kuimarisha miundombinu ya skimu za umwagiliaji ili kuwa na kilimo endelevu.
Senyamule ameyasema hayo leo Juni 21, 2023 wilayani Bahi katika siku ya saba ya ziara ya Katibu Mkuu wa CCM Ndg. Daniel Chongolo Mkoani Dodoma.

"Mkoa wa Dodoma tulikuwa tunaaminishwa kama mkoa kame, lakini tatizo ni maarifa tu ya namna ya kuyapata maji na namna ya kuyahifadhi kwa matumizi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kilimo na mifugo. 
"Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Kilimo kutenga fedha nyingi kutekeleza miradi ya umwagiliaji mkoa kwetu,"Senyamule amesisitiza.

Amesema, katika skimu 16 zilizopo wilayani Bahi 15 ni za mpunga na moja ya zabibu hivyo lengo la Serikali ni kuzalisha mazao ya kutosha si kulisha Tanzania pekee bali kulisha dunia kwa ujumla wake kupitia ujenzi wa skimu za umwagiliaji zitakazowezesha kilimo mwaka mzima.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Daniel Chongolo ameiagiza Serikali kutangaza haraka zabuni za miradi ya skimu za umwagiliaji nchini.

Chongolo ametoa agizo hilo leo katika mkutano uliokutanisha wananchi katika Wilaya ya Bahi ambapo Katibu wa shina hilo, Joseph Chipule alipomueleza kuhusu changamoto ya ubovu wa miundombinu ya skimu za umwagiliaji.

Ombi hilo lilitiliwa mkazo na Mbunge wa Jimbo la Bahi, Keneth Nollo aliyesema wananchi wa eneo hilo wanaojishughulisha na kilimo cha mpunga, wanauwezo wa kulisha Mkoa wa Dodoma endapo skimu za umwagiliaji zingekarabatiwa.
“Bahi kuna mabonde mengi yanayofaa kwa kilimo cha mpunga, katika eneo hilo skimu tano ziliharibiwa na mvua za Elnino mwaka 1998 na tangu kipindi hicho kazijakarabatiwa, hivyo wakulima wanashindwa kuzalisha chakula cha kutosha,”alisema Nollo.

Kutokana na maelezo hayo Chongolo alisema ni vyema Wizara ya Kilimo kupitia Tume ya Umwagiliaji kuhakikisha kuanzia Julai Mosi mwaka huu wanatangaza tenda za ujenzi na ukarabati wa skimu za umwagiliaji nchini nzima.
“Maelekezo yetu kwa serikali kuanzia Julai Mosi mwaka huu tangazeni tenda za skimu ambazo zimetengewa fedha, ambazo zingine zinaenda kukarabatiwa na zingine zinaenda kufanyiwa upembuzi yakinifu.”

Alisema utangazaji wa zabuni mapema utaharakisha kuwapata wakandarasi wa kutekeleza miradi na kuifanya ikamilike kwa wakati na kuwanufaisha wananchi.

Aidha, Chongolo alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wananchi wa Bahi na wanaozungukwa na skimu za umwagiliaji kutouza maeneo yao.
“Wakati serikali inaweka fedha za kuboresha miundombinu ya skimu za umwagiliaji wajanja wanaotafuta fursa wengi watakimbia hapa kutafuta maeneo achene kuuza maeneo ya mashamba yenu, yamilikini endeleeni kuyasimamia mtu akitaka kulima mkodishe alime akupe chako mwaka unaofuata ulimwe mwenyewe.

“Kuuza ardhi ambayo imeshawekewa miundombinu ni kujitia umaskini na kujibadili kuwa kibarua katika ardhi yako mwenyewe uliyoimiliki kabla ya kuiuza."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news