NA LWAGA MWAMBANDE
KWA mujibu wa chapisho la Mradi wa Tufundishe Watoto kupitia somo la 180: Wanawali Kumi (Mathayo 25:1-13) la Julai 9, 2017, Yesu alitoa mfano huo katika nyakati zake za mwisho, siku chache kabla ya sherehe ya Pasaka. Alipenda wanafunzi wake wakae tayari kumpokea tena atakaporudi kwake.
Hivyo, tunahitaji kuangalia tamaduni za harusi kwa kipindi kile cha Yesu. Katika harusi ya Wayahudi karamu ya harusi ilifanyika jioni, baada ya siku nzima ya shamrashamra.
Mwisho wa siku huyu bwana harusi alichukuliwa na marafiki zake kwa ajili ya kwenda katika maandamano mpaka nyumbani kwa wazazi wa bibi harusi.
Anafika kabisa nyumbani kwake. Bwana harusi na marafiki zake wanapokelewa na wanawali, yaani wampambe bibi harusi.
Kwa njia hii bwana harusi na kikundi chake wanatangaza harusi hii. Kutoka na tamadunii za Kiyahudi ilikuwa muhimu kabisa kutimiza wajibu wao kwa pande zote mbili.
Bwana harusi na kikundi chake na bibi harusi na wanawali. Lakini bibi harusi na wanawali hawakujua kabisa muda wa kufika bwana harusi. Wakati huo haukujulikana kabisa. Muhimu tu ni bibi harusi na wanawali wako tayari na bibi harusi ameshapambwa na wanawali.
Jioni ya kufika kwa bwana harusi ni ndani ya siku kumi ya sherehe. Ndani ya siku hizi bibi harusi na wanawali wamemjua tu bwana harusi na kikundi chake wanakuja.
Kama bibi harusi na wanawali wakisikia bwana harusi na marafiki zake wakiingia sehemu ya wazazi wa bibi harusi wanawali wanaenda nje na bwana harusi anapokelewa kwa heshima na furaha.
Wanamsindikiza mpaka nyumbani kwa bibi harusi kumchukua. Wote wanatembea sasa kwa maandamano kwenda nyumba ya bwana harusi.
Na nyumbani kwake sherehe ya harusi inaanza sasa. Katika sherehe hii wanakijiji wanakaribishwa wote wa kijijini kwa harusi hii maana ndugu, marafiki na majirani.
Ukimpokea bwana harusi nje gizani ni lazima tuwashe taa (koroboi). Kwa hiyo ni bora usafishe kamba ya koroboi kabla ya kuwasha ili ile koroboi ilete mwanga zaidi na wa kutosha.
Ndani ya mfano huu wasichana watano wanatumia mafuta yote mwanzoni wakati wa kumsubiri bwana harusi. Wasichana wengine watano wanalala kwanza na kama wakisikia bwana harusi anaingia mazingira ya bibi harusi wanaonesha wako tayari kumpokea kwa mwanga wa koroboi, furaha na utayari kutoka moyoni mwao.
Wasichana wenye busara walilala kwanza na kutumia mafuta kwa umakini. Wanaonesha wako tayari kutunza na kujenga imani yao.
Ndani ya mfano huu koroboi ni picha ya imani yetu, hasa mafuta ya koroboi. Kamba ya koroboi ni kama moyo wa mtu. Kama usingesafisha kamba ya koroboi usingefaulu kuwasha koroboi vizuri ili ing'ae na mwanga wake.
Usingesafisha moyo wako mara kwa mara usingeweza kumpokea bwana harusi kwa maana ya Bwana Yesu. Mafuta ndani ya koroboi ni imani ya watu.
Imani ya watu inawaka vizuri kama moyo uko safi. Sisi tuwe tayari kusafisha mioyo yetu kila wakati ili tuweze kumpokea Bwana Yesu.
Aidha, kitu kingine, imani huwezi kumpa mtu mwingine kwa hiyo wasichana wenye busara hawawezi kuwapa wasichana wapumbavu mafuta yao, kwa sababu kila mtu ana imani na mafuta yake.
Pia imani yetu inapungua muda fulani na inaongezeka kipindi kingine kama mafuta ndani ya koroboi.Yesu anapenda tuwe tayari, tusafishe mara kwa mara mioyo yetu, tuwe makini ndani ya imani yetu. Kwa hiyo alifurahahishwa wasichana wenye busara waliotunza mafuta yao badala kutumia ovyo ovyo.
Katika mfano huu wasichana wale waliomngojea bwana harusi ni mfano wa kanisa linalongoja kurudi kwake Bwana Yesu katika utukufu wake. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, taa kuwa na mafuta hiyo kwa Mungu ni hekima. Endelea;
1.Ufalme wa mbinguni, huo hasa wafanana,
Wanawali wa zamani, jumla kumi twaona,
Kwa hapa ulimwenguni ni wamjuao Bwana,
Taa kuwa na mafuta, hiyo kwa Mungu hekima.
2.Walikuwepo watano, ambao werevu sana,
Taa zao zile tano, mafuta kwenye hazina,
Hao ni kuwapa tano, walijiandaa sana,
Taa kuwa na mafuta, hiyo kwa Mungu hekima.
3.Ila watano wengine, walikuwa wajiona,
Akili zao zingine, mafuta taa hakuna,
Walikaa kivingine, na Mungu walipishana,
Taa kuwa na mafuta, hiyo kwa Mungu hekima.
4.Ndivyo waliookoka, jinsi wamechanganyana,
Wengi wao wamechoka, taa mafuta hazina,
Imebaki kutamka, kwamba asifiwe Bwana,
Taa kuwa na mafuta, hiyo kwa Mungu hekima.
5.Na huko wako wengine, wanapiga mbiu sana,
Hawaendi kwa mwingine, wanamngojea Bwana,
Hao vema tujuane, na wao kuandamana,
Taa kuwa na mafuta, hiyo kwa Mungu hekima.
6.Bwana harusi haraka, twaweza tukamuona,
Usingizi takatika, naye tuweze kutana,
Tusije kuhangaika, kama mafuta hatuna,
Taa kuwa na mafuta, hiyo kwa Mungu hekima.
7.Habari za wanawali, hapa tunakumbushana,
Muda ajao si mbali, tutamwona Yesu Bwana,
Ni vema kuwa kamili, naye tusijepishana,
Taa kuwa na mafuta, hiyo kwa Mungu hekima.
8.Mpendwa amka sasa, usije mkosa Bwana,
Hii twakupa hamasa, wanawali umeona,
Nenda kanunue sasa, endapo mafuta huna,
Taa kuwa na mafuta, hiyo kwa Mungu hekima.
9.Neno ukilisikia, hilo kumbatia sana,
Nyuma usijesalia, anasa zikakubana,
Utaachwa nakwambia, kibali hutakiona,
Taa kuwa na mafuta, hiyo kwa Mungu hekima.
10.Habari ya wanawali, nawe wahusika sana,
Hapo kuna pande mbili, tunavyotambulikana,
Ishi maisha ya kweli, na Mungu kuongozana,
Taa kuwa na mafuta, hiyo kwa Mungu hekima.
(Mathayo 25:1-13)
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602