NA ELEUTERI MANGI-WUSM
KATIBU Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu amekutana na kufanya kikao cha pamoja na ujumbe kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambapo wamejadili namna bora ya kuboresha miundombinu ya michezo nchini.

Pamoja na mambo mengine, viongozi hao wamejadili kuhusu uendeshaji na usimamizi wa viwanja vya michezo vinavyomilikiwa na kusimamiwa na Serikali pamoja na CCM ambavyo vinatumika katika michezo mbalimbali nchini ikiwemo Ligi Kuu ya NBC.
Kikao hicho kimehudhuriwa wajumbe nane kutoka CCM akiwemo Mhasibu Mkuu wa CCM Taifa, Bw. Thobias Abwalo huku ujumbe wa Wizara yenye dhamana na michezo ikiwa na wajumbe saba akiwemo Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini Bw. Ally Mayayi.