NA DIRAMAKINI
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt.Mwingulu Lameck Nchemba amesema, Serikali inatambua na kuthamini mchango wa madhehebu ya dini nchini katika kuleta maendeleo.
Mheshimiwa Dkt.Nchemba ameyasema hayo Juni 4, 2023 wakati akiwa mgeni rasmi katika ibada ya harambee ya kuchangia ujenzi wa shule za sekondari za Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kati.
"Moja ya muundo wa utekelezaji wa shughuli za maendeleo wa ushirikiano kati ya sekta binafsi na Serikali, kati ya kanisa na Serikali ni miradi ya maendeleo ambayo imefanywa na kanisa, Serikali inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan inaunga mkono jitihada zote hizi ambazo taasisi za kidini zinafanya,"amesema.
Pia, Mheshimiwa Waziri Dkt.Nchemba amesema, Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri zaidi kwa kwa madhehebu ya kidini nchini kutekeleza majukumu yake.
Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kati (Singida) linatarajia kufanya ujenzi wa shule mbili za sekondari zinazotarajiwa kugharimu shilingi milioni 500 ambapo moja itajengwa Manispaa ya Singida, kwenye eneo la Mission lililopo Kititimo na ya pili itajengwa makao makuu ya Wilaya ya Iramba mjini Kiomboi.
"Baba Askofu nilikutana naye mwaka jana,mwaka juzi nikamuelezea masuala mbalimbali Mheshimiwa Rais ambayo yanahusiana na kutengeneza mazingira mazuri ya kanisa liweze kuchangia kushiriki katika shughuli za maendeleo, na Mheshimiwa Rais alinielekeza mtaona katika bajeti ya mwaka jana kuna hatua tulizichukua ambazo zinafanya kanisa kuweza kufanya shughuli zake vizuri na hasa hizo za kuchangia katika shughuli za maendeleo.
"Na hata mwaka huu tunatarajia tutakua na hatua ambazo ni mwendelezo ya maelekezo ambayo aliyatoa Mheshimiwa Rais,"amebainisha Waziri Dkt.Nchemba.
Akizungumza na waumini wa Kanisa hilo wakati wa Ibada hiyo maalumu iliyofanyika kwenye Usharika wa Emmanuel, ambao ni makao makuu ya Dayosisi hiyo Singida Mjini, Waziri Dkt. Nchemba ameitaka jamii kuwekeza kwenye shughuli za kilimo ili sekta hiyo iweze kuleta tija nchini, hasa kupitia kundi la vijana ambalo hivi sasa linapoteza mwelekeo licha ya Serikali kugharamia masomo yao hadi ngazi ya elimu ya juu.
Katika ibada hiyo, Askofu Dkt.Alex Malasusa wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani amesema, "Naomba Wakristo msikwepe kodi, hata Yesu mwenyewe alitoa kodi,Mristo aliye mwaaminifu anatoa kodi na hana matatizo na kodi, Mkristo aliye mwaminifu hafilisiki kwa sababu biashara yake ipo katika uhalali wote,"amesema Askofu Dkt.Malasusa.
Aidha, aliwataka Wakristo kujenga utamaduni wa kumtolea sadaka Mungu ili baadaye wapate baraka na hivyo kufanikiwa katika maisha yao.
Naye Askofu wa Dayosisi ya Kati,Dkt.Syprian Hillinti ameishukuru Serikali kwa kutengeneza mazingira mazuri ya taasisi za kidini ziweze kushiriki katika shughuli za maendeleo.
"Asante sana kwa ahadi ya Serikali kutengeneza mazingira mazuri ya taasisi za dini zote si Wakristo tu kuendesha mambo yake, nilisema siku ninawekwa wakifu Waislamu wakileta makontena wafikiriwe,"amesema Askofu.
Aidha, katika harambee hiyo ambayo iliwakutanisha watu mbalimbali mgeni rasmi Mheshimiwa Waziri Dkt.Mwigulu alichangia shilingi milioni tano huku zaidi ya shilingi milioni 443.63 zikikusanywa kwa ajili ya kufanikisha ujenzi huo wa shule.