NA JACOB KASIRI
SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limeungana na timu ya Mkoa wa Iringa kushiriki katika doria ya kuwasaka wanyama aina ya simba ambao hivi karibuni walizua taharuki katika vijiji jirani na hifadhi.

Akizungumzia kuhusiana na tukio hilo, Kamishna Mwakilema amefafanua kuwa, "Nilipata taarifa ya uvamizi wa wanyama hao katika vijiji vilivyoko mbali kabisa na hifadhi zaidi ya kilomita 25.

"Baada ya uvamizi wa wanyama hao,timu ya askari 17 kutoka Hifadhi ya Taifa Ruaha na maafisa kutoka Kanda ya Kusini walifika kwa haraka kushirikiana na wenzetu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, TAWA (Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzani) na KDU (Jeshi la Uhifadhi wa Wanyamapori na Misitu) kuwasaka simba hao wasilete madhara zaidi," amesema Kamishna Makilema.

"Na jana wasaidizi wangu wameruka nayo ila kutokana na hali halisi ya milima na makorongo marefu hawakuweza kuwaona.
"Pia nimeongea na mtu wa AWF pale Manyara Ranch ili kuweza kupata mbwa wa kunusa watusaidie kutambua harufu za simba hao,"amesema Kamishna huyo.

"Kwa haraka niliwasiliana na wenzetu wa TANAPA na TAWA kuja kuwaondoa simba hao.Hata hivyo, Simba hao waliendelea kusonga mbele wakiua mifugo na hatimae kufika eneo la Kiponzelya karibia na mji wa Iringa.

Mkazi wa kijiji cha Tanangozi, Grayson Laurent Mtende amesema, "baada ya kupata taarifa za simba kijijini kwetu tuliogopa kwa sababu simba hawazoeleki na ni mnyama anayeogopwa hivyo tumesitisha kufanya kazi zetu mashambani kwa muda mpaka pale mamlaka zinazohusika na uhifadhi zitakapotuambia hali ni shwari."

Pia wananchi wanaendelea kuelimishwa njia salama za kujilinda na wanyama kwa kutokuwaruhusu watoto na watu wazima kwenda vichakani kuokota kuni, na wanapotoka nje nyakati za usiku watoke na tochi.