NA MWANDISHI WETU
NAIBU Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameufungua Mgodi wa wachimbaji wadogo wa Madini ya Dhahabu uliofungwa baada ya kuumaliza mgogoro kati ya wachimbaji wadogo wa Madini ya Dhahabu na mmiliki wa leseni ya uchimbaji mdogo Godfrey Bitesigirwe katika eneo la Kwandege Kijiji cha Mlimamzinga Wilaya ya Handeni mkoani Tanga.
Dkt. Kiruswa ameufungua mgodi huo baada ya kumaliza mgogoro uliodumu kwa muda mrefu kati ya wachimbaji hao na mmiliki wa leseni hiyo wilayani humo baada ya kutembelea eneo la machimbo hayo na kuzungumza na wachimbaji wadogo wa madini katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo la mgodi huo.
Aidha, Dkt. Kiruswa amewataka wachimbaji wadogo kufanya shughuli za uchimbaji wa madini katika eneo hilo kwa siku 90 kama alivyoagiza Mkuu wa Wilaya hiyo kabla ya kuufunga Mgodi huo na kumtaka mImiliki wa leseni hiyo kutoa ajira kwa wachimbaji wadogo wanaotarajiwa kupisha eneo la leseni hiyo ili rasilimali hiyo iweze kuwafaidisha wote.
Pamoja na mambo mengine, Dkt. Kiruswa ametoa anyo kwa wachimbaji wadogo na wafanyabishara wa madini wanaotorosha madini kwa lengo la kukwepa kodi ya Serikali ambapo amewataka kufuata Sheria na Kanuni zilizowekwa na Serikali ikiwemo kuuza madini katika Masoko na Vituo vya Ununuzi wa Madini.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Handeni Vijijini John Sallu amempongeza Dkt. Kiruswa kwa kuumaliza mgogoro uliokuwepo katika eneo hilo ili wachimbaji hao wachimbe kwa tija na wanufaike na rasilimali madini katika wilaya hiyo .
Pia, Sallu ameiomba Wizara ya Madini kutenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo hususan maeneo yenye leseni ya utafiti yaliyoisha muda wake ili waweze kufaidika na rasilimali madini zilizopo wilayani humo.