Serikali yapeleka shangwe kubwa Mbarali, warejeshewa ardhi

NA JACOB KASIRI

SERIKALI ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan imerejesha hekta 74,432 kwa wananchi wa Mbarali ili waendeleze kilimo na ufugaji.
Uamuzi huo wa Serikali unalenga kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi tofauti na awali ambapo maeneo hayo yalikuwa chini ya Hifadhi ya Taifa Ruaha.
Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Mbeya, Syabumi Mwaipopo ameyabainisha hayo Juni 22, 2023 alipokuwa akiwasilisha ripoti kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii ilipotembelea Shamba la Kapunga lililoko wilayani Mbarali kufanya tathmini ya utekelezaji wa uwekaji wa mpaka unaoendelea katika wilaya za Mbarali na Chunya mkoani Mbeya.
Naye Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa (MB) alisema kuwa, baada ya kamati hii kutembelea uwandani na kujionea hali halisi itawasilisha mapendekezo ya walichokiona bungeni ili kubadili GN.28 na kuja na GN. mpya ambayo itakuwa ni suluhu kwa mgogoro uliodumu zaidi ya miaka 18.
"Ndugu zangu wana Mbarali, eneo lote hili lilorudishwa kwenu lilikuwa chini ya uhifadhi,na hivyo serikali kulitoa kwenu ina dhamira ya dhati kwa wananchi wake. Niwaombe, acheni zoezi hili liendee na kukamilika kwa wakati ili muweze kufanya shughuli zenu za kilimo na ufugaji kwa manufaa yenu na taifa kwa ujumla,"alisema Waziri Mchengerwa.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Juma Homera akiwakaribisha Waziri wa Maliasili na Utalii na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii alisema kuwa ni kweli kama wananchi wanavyolalamika shamba la Kapunga halijapunguzwa. Shamba hili halikupitiwa na GN ya zamani na hata hii mpya haijapita pia kwa sababu GN mpya inapita katika maeneo yale yale yaliyopitiwa na GN.28 na wala haianzishi maeneo mapya. 

Hata, hivyo wananchi watambue kuwa Kapunga Estate ni shamba la serikali na huyu mwekezaji amepewa awekeze tu kwa muda maalum, na mkataba wake utakapoisha shamba hili litarudi serikalini.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhe.Timotheo Paul Mnzava alisema kamati hiyo ya Bunge inasimamia shughuli za Maliasili na Ardhi kwa niaba ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivyo msingi wa safari hiyo ni kujiridhisha ili kulishauri Bunge kuona namna bora kumaliza hilo jambo. 
Aidha, mwenyekiti huyo aliongeza kuwa nchi ni yetu sote lazima tulinde wananchi wetu na pia tulinde Maliasili zetu kwa ajili ya kizazi cha sasa na kizazi kijacho.

Zoezi la uwekaji mpaka wilaya za Mbarali na Chunya limekamilika, ambapo vigingi 671 vimewekwa kwa umbali wa kilometa 344 kwa uwiano wa mita 500 kila kigingi ili kuwawezesha wananchi na wahifadhi kutambua maeneo yao ili kuepusha muingiliano.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news