NA MWANDISHI WETU
NAIBU Waziri wa Madini, Dkt.Steven Kiruswa ametoa muda wa miezi mitatu kwa Kampuni ya PMM Tanzania Limited kuanza uzalishaji katika Mgodi wa Uchimbaji wa Kati wa Madini ya Dhahabu uliopo katika Kijiji cha Nyasa wilayani Handeni Mkoa wa Tanga.
Dkt. Kiruswa amebainisha hayo baada ya kufanya ziara katika Mgodi huo ambao unalalamikiwa na wananchi wa vijiji vinavyozunguka mgodi huo kwa kuchelewa kuanza uzalishaji na kusababisha Serikali na wananchi kukosa mapato yatokanayo na shughuli za madini.
Aidha, Dkt. Kiruswa ameutaka Mgodi huo kuandaa Mpango wa Ushirikishwaji wa Wazawa katika Sekta ya Madini na Wajibu wa Mgodi kwa Jamii (CSR) ili kuhakikisha kwamba wananchi na jamii inayozunguka mgodi huo inafaidika ipasavyo na uwepo wa mgodi huo katika maeneo hayo.
Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Tanga, Zabibu Napacho amesema Mei 26, 2023 ofisi yake ilifanya ukaguzi maalum katika mgodi huo na kubaini mapungufu mbalimbali ikiwemo upungufu wa wataalamu hususani wahandisi migodi, uchakavu wa mitambo ya kuchimba na kuchenjua dhahabu na kutokuwepo kwa dalili za shughuli za uchimbaji madini mgodini hapo.
Pamoja na mambo mengine, Napacho amesema, kumekuwepo na malalamiko ya mara kwa mara ya wakandarasi, watoa huduma na baadhi ya wafanyakazi hasa walioachishwa kazi kutolipwa stahiki zao kwa wakati.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya PMM Tanzania Limited, Ulimbakisya Spendi ambaye ni mmiliki wa kampuni hiyo amesema mgodi huo umepanga kuajiri wataalamu wenye uzoefu wa uchimbaji na uchenjuaji wa madini ili kuongeza ufanisi katika shughuli za uchimbaji madini.