NA DIRAMAKINI
SERIKAL ya Jamahuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula imewaongezea muda wa miezi minne wapangaji wa nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam kufuatia notisi waliyopewa Juni 2, 2023 ya kuhama katika majengo wanayopanga ambayoo yatahusika kwenye uwekezaji wa ubia kati ya NHC na makampuni binafsi.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula (wa kwanza kulia) akiongoza kikao hicho.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika kikao kilichowakutanisha Uongozi wa Shirika la Nyumba la Taifa na Uongozi wa wapangaji hao, Waziri Dkt. Mabula amesema kuwa, baada ya kusikiliza maoni na mapendekezo ya wapangaji hao Serikali imeona ni vyema kuwaongezea muda wa miezi mingine minne mbali ya ile mitatu ya notisi waliyopewa na NHC hapo awali.
“Serikali yenu ya Awamu ya Sita imesikiliza maoni na mapendekezo yenu ambayo mmeyawasilisha kwa lengo la kutaka kufikia muafaka juu ya muda mliopewa wa kupisha uwekezaji utakaofanyika katika baadhi ya maeneo, pamoja na mambo mengine tunafahamu kuwa baadhi yenu mna mikopo Benki na bidhaa zilizopo ghalani na zingine mmekwishaagiza, kwa kuzingatia hili mmeongezewa miezi minne ili muweze kujipanga vizuri zaidi ili kupisha maendeleo ya majengo makubwa yanayotarajiwa kufanywa,” amesema Dkt. Mabula.
Dkt. Mabula amesisitiza kuwa, ubia utakaofanywa katika maeneo yaliyoanishwa una lengo la kuboresha zaidi maeneo ya biashara pamoja na makazi, hivyo wapangaji hao wanapaswa kufahamu kuwa hawajatelekezwa bali ni kupisha uwekezaji ufanyike na baada ya kukamilika kwa ujenzi biashara zitaendelea kama kawaida.
Baadhi ya wafanyabiashara wakimsikiliza kwa makini, Mhe. Waziri (hayupo pichani).
“Niwaombe ninyi viongozi kuwa mabalozi kwa wafanyabiashara wenzenu kwanza acheni kusikiliza upotoshaji unaoendelea kuwa kuna muhindi mmoja amepewa maghorofa 19 kwa ajili ya kujenga huo ni uzushi mkubwa sana hakuna kitu kama hicho kwanza kitendo hicho ni kibaya kwani kinaonesha ubaguzi wa waziwazi, kwanini apewe muhindi peke yake wakati kuna wabia wengine tena Watanzania wenye nia ya kuwekeza, achaneni na taarifa hizo kwani hazina ukweli wowote,” alisema Dkt. Mabula.
Kuhusu kuwepo taarifa za mtu anayekusanya fedha kiasi cha shilingi milioni mbili kama kodi ya mwezi na kwamba wapo waliotoa fedha hizo kwa kulipa kodi ya miezi sita ili kuzingatiwa kupewa upangaji hapo baadae, alisisitiza kuwa watu hao wamedhulumiwa kwani mchakato wenyewe bado haujakamilika, hivyo mtu huyo ni tapeli tena anapaswa kuripotiwa kwenye vyombo vya sheria na kuchukuliwa hatua.
Waziri huyo wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi amewataka wafanyabiashara hao kuwa waangalifu katika kipindi hiki kwani wanaweza wakajitokeza kila aina ya watu wenye nia ovu kwa kuwadanganya kuwa walipe kodi mapema ili kuwahi nafasi za fremu. Ikiwa wafanyabiashara hao wanataka kuujua ukweli wa uwekezaji huo wasisite kufika NHC ili kupata ukweli wa jambo.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhandisi Athony Sanga ambaye alishiriki katika kikao hicho amewapongeza wafanyabiashara hao kwa kukubali nia ya dhati ya shirika ya kutaka kuboresha baadhi ya majengo yake.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa,Bw. Hamad Abdallah amesema kuwa mpaka sasa Shirika la Nyumba la Taifa halijaingia makubaliano ya mkataba na mtu yoyote, hivyo taarifa zinazosambaa kuwa tayari kuna mtu ameingia makubaliano na NHC ni uongo na kwamba kwa sasa Shirika liko katika mchakato mkubwa wa kufanya upembuzi wa maombi yaliyowasilishwa kwa ajili ya uwekezaji huo.
Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa,Bw. Hamad Abdallah (wa pili kushoto) akijadiliana jambo na viongozi wa wafanyabiashara wa Kariakoo waliopanga kwenye majengo ya NHC.
“Katika eneo la Kariakoo majengo yatakayohusika na uwekezaji ni 14 tu na si 19 kama ambavyo inasemekana, niwatoe wasiwasi ndugu zangu juu ya suala hili tumejipanga kuhakikisha wale wenye vigezo ndiyo watakaonufaika na uwekezaji huo wenye nia ya kuboresha mazingira yetu lakini pia kuweka mazingira hayo katika hali iliyobora zaidi tofauti na sasa,” amesema Abdallah.
Pamoja na kwamba majengo hayo yatakuwa na mbia lakini NHC tutajadiliana kwa pamoja na wabia hao ili kuona uwezekano wa kuwapatia nafasi wafanyabiashara ambao walikuwepo hapo awali kabla jengo halijaboreshwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wafanyabiashara hao, Bw. Shafiq Mohamed alianza kwa kumshukuru Mhe. Waziri na uongozi wa Shirika kwa kukaa pamoja nao ili kujadiliana mambo kadhaa yaliyojitokeza mara baada ya kutolewa notisi ya miezi mitatu ya kusitisha upangaji wao.
Shafiq amesema kuwa, kwa upande wao wanakubaliana na maboresho yanayoyokwenda kufanyika na kwamba wanaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwaongezea muda wa miezi minne ili kupisha ujenzi unaokwenda kufanyika.
Novemba 16, 2022 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa alizindua Sera ya Ubia ya NHC iliyoboreshwa.