Serikali yaweka msimamo dhidi ya dawa za kulevya

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu ametoa wito kwa wazazi, walezi pamoja na jamii kuwajibika katika kufuatilia mienendo ya watoto ili kubaini mabadiliko hasi ya kitabia yanapojitokeza.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan akiwasili katika Banda la Maonesho la Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Kupiga Vita Matumizi na Biashara ya Dawa za Kulevya Duniani ambayo Kitaifa yamefanyika mkoani Arusha leo Juni 23, 2023.

Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amesema hayo leo Juni 25, 2023 wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Amesema, kutowajibika kwa wazazi husababisha watoto kuathirika na matumizi ya dawa za kulevya hivyo ni vyema kuwalinda watoto dhidi ya dawa hizo pamoja na vitendo vingine vilivyo kinyume na mila, desturi, maadili na silka
zetu.

Rais Dkt.Samia pia ameitaka jamii kuimarisha ushirikiano na viongozi wa dini pamoja na viongozi wa kijamii wakiwemo machifu kwa kuwa ndio walinzi wakuu wa maadili,utamaduni, mila na desturi.

Vile vile, Rais Dkt.Samia amesema, tatizo la biashara na matumizi ya dawa za kulevya nchini na duniani kwa ujumla limekuwa likiongezeka na madhara yake ni makubwa na wakati mwingine athari zake ni za kudumu kwa jamii.

Hali kadhalika, Rais Dkt.Samia amesema, mbali na kupoteza nguvu kazi ya uzalishaji,matumizi ya dawa za kulevya yamekuwa kichocheo cha vitendo vya uhalifu ikiwemo wizi na unyang’anyi na hata kuambukizana maradhi kama UKIMWI na TB.

Kwa mujibu wa taarifa ya hivi karibuni ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC), Tanzania ilifanikiwa kupunguza uingizaji wa dawa za kulevya kutoka nchi zinazozalisha kwa zaidi ya asilimia 90.

Onyo

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amezionya gereji zinazofanya biashara ya unga unaotoka katika masega ya gari kwa ajili ya kutengenezea dawa za kulevya nchini.

Amesema, umezuka mtindo mpya wa watu kupasua bomba linalotoa moshi wenye sumu kwenye gari na kuchukua unga uliopo ndani yake na kuchanganywa na cocaine au heroin kisha vijana wanavuta na kupata madhara ikiwemo kufariki.

“Tumepata taarifa kwamba kuna bidhaa zinaingizwa nchini, lakini zinachanganywa na dawa za kulevya na nimeona kwenye banda la maonesho wamenionesha wanasema mtu anaweza kuja na unga, lakini ule unga usiwe wa kawaida.

“Kuna bidhaa pia zinachanganywa na cocaine na heroin ambazo zinaweza kuwa sumu, siku hizi kuna mtindo wanapasua bomba linalotoa moshi kwenye gari ndani yake kule kuna unga fulani unaosababisha control ya ule moshi.

"Sasa ule unatolewa huko kwenye magereji yetu unapelekwa kwenye maunga vijana wetu wanayotumia, lakini ule moshi una sumu kubwa sasa ukichanganya na unga wanaotumia wakijidunga ndio maana unasikia mateja wanaanguka wanakufa, niombe mamlaka zinazohusika tuliangalie hili.

“Wenye gereji pia walitazame hili magari wanayopelekewa mafundi wao wanapasua wanatoa unga wanakwenda kuua,"amesema.

Aidha, Rais Dkt.Samia akizungumzia kuhusu bangi amesema,uchunguzi unaonesha ipo baadhi ya mikoa inakabiliwa na changamoto hiyo ya wananchi kujihusisha na kilimo cha bangi.

“Arusha mmejisema wenyewe hapa mkuu wa mkoa kajisema mwenyewe na kwamba hili dude la Arusha ni organic na ni kali mno, lakini mikoa mingine na naona wakuu wa mikoa wapo hapa Mara wamo kwenye hili.

"Manyara, Morogoro, Iringa , Ruvuma, Tanga na Kilimanjaro wote mmeathirika na balaa hili kwa kiasi kikubwa, kwa hiyo naomba wote mkaweke nguvu katika kuilinda jamii na balaa hili.

“Nilikuwa nanong’ona na Waziri Mkuu (Mheshimiwa Kassim Majaliwa) wazo la kwamba zile fedha tulizositisha za asilimia 10 za halmashauri kuzielekeza halmashauri vijana hawa (waraibu walioacha dawa za kulevya) waunganishwe wakapate fedha wajue kile watakachoenda kukifanya, naomba Waziri Mkuu lisimamie hilo mkalipange vizuri,”amesisitiza Mheshimiwa Rais Dkt.Samia.

RC Arusha

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Arusha,Mheshimiwa John Mongella amesema wakati Serikali ikipambana na dawa za kulevya aina ya bangi, aina hiyo ya mmea unaolimwa Arusha ambao ni maarufu kama "Cha Arusha" inatajwa kama ndio bangi kali zaidi duniani.

Bangi hiyo hulimwa na nyingine kujiotea katika marnro ya Mlima Meru na hasa katika Kijiji cha Kisimiri Juu wilayani Arumeru.

Mheshimiwa Mongella amesema, kilimo cha bangi kinafanyika katika Kijiji cha Kisimiri Juu kutokana na eneo hilo kuwa na ardhi yenye rutuba kubwa.

"Tumepewa taarifa na wataalam wa dawa za kulevya kuwa bangi ambayo inapatikana Kisimiri ndio bangi kali zaidi duniani na watumiaji wamekuwa wakitumia kwa tahadhari la sivyo inawaharibu," amesema.

Hata hivyo amesema Serikali mkoani Arusha kwa kushirikiana na viongozi wa mila na dini wanaendelea na mkakati wa kudhibiti kilimo cha bangi Kisimiri.

Pia, amesema Serikali kwa miaka imekuwa ikipambana na kilimo cha bangi, lakini bado kinaendelea na sasa ndio sababu inashirikisha viongozi wa mila, viongozi wa dini na wananchi.

"Tumeunda kamati ya watu 60 ambayo itapita kwenye mashamba kung'oa bangi kwa kushirikiana na wananchi," amesema huku akiongeza kuwa, elimu inaendelea kutolewa katika Kijiji cha Kisimiri kuachana na kilimo na bangi na kujikita na kilimo cha mazao mengine.

Mitambo

Mbali na hayo, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amesema, ana matumaini maboresho yanayoendelea kufanywa katika bandari za Tanzania yatajumuisha ufungaji wa mitambo ya kisasa itakayosaidia kubaini shehena zinazopitishwa zikiwa na dawa za kulevya ndani yake.

“Bandari zetu ni milango ya kuhudumia usafiri na usafirishaji wa bidhaa kwenda nchi jirani inawezekana baadhi ya wahalifu wakatumia usafirishaji wa shehena hizo kupitisha dawa za kulevya.

"Na ndio sababu ninasisitiza umuhimu wa kubadilishana taarifa za kiitelejensia na nchi jirani na kufanya kazi kama nchi moja baina ya Tanzania bara na Zanzibar kwa sababu milango hii Zanzibar ipo wazi sana, mtu akitoka duniani anaweza kuingia njia yoyote Zanzibar na kutoa Zanzibar kuleta Bara ni kazi rahisi.

“Tushirikiane kuongeza mapambano ya kudhibiti dawa za kulevya, ni matumaini yangu maboresho yanayoendelea kufanywa katika bandari zetu yatajumuisha ufungaji wa mitambo ya kisasa itakayosaidia kubaini shehena zinazopitishwa zikiwa na dawa za kulevya ndani yake.

“Hata hivyo kuwa na mitambo ni jambo moja, lakini kuwa na watendaji waadilifu ni jambo la pili, tukiwa na mitambo bila watendaji wenye uadilifu hatutopata matokeo tunayoyatarajia, tunahitaji watumishi wenye uzalendo wanaoweka mbele maslahi ya Taifa.

"Watumishi wa bandari, wa TMDA (Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba), wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) wote tutangulize maslahi ya Taifa mbele ndipo tutashinda vita hii,” amesisitiza Mheshimiwa Rais Dkt.Samia.

Shisha

Naye, Kamishna Jeneralin wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA),Aretas Lyimo amesema, shisha imekuwa kichochea cha matumizi ya dawa za kulevya huku tatizo hilo likiwaathiri zaidi vijana.

Kamishna Jenerali Lyimo amesema, wamebaini baadhi ya wauzaji wa shisha kuchanganya dawa za kulevya jambo ambalo limeongeza matumizi ya dawa za kulevya nchini.

"Matumizi ya shisha yameongeza matumizi ya dawa za kulevya na kuchochea matumizi ya dawa hizo,"amesema

Aidha, amesema DCEA imejipanga Kupambana na dawa za kulevya nchini hatua ambayo imefanya Tanzania kuwa mfano katika kudhibiti dawa hizo.

Diamond

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Wasafi Media, na staa wa Bongo Fleva,Naseeb Abdul Juma Issack maarufu kama Diamond Platnumz amewataka vijana nchini kuachana matumizi ya dawa za kulevya kwani hazina manufaa yoyote.

Pia amesema,matumizi ya dawa za kulevya licha ya kuharibu afya pia uvutaji unaondoa fursa kwa vijana. "Ukiwa unatumia dawa za kulevya unaitwa teja hakuna ambaye atakupa kazi, hakuna ambaye atakupokea hata katika muziki sisi tukikuona tunakuona teja tu.Leo mimi nimetoka Tandale nimefika Arusha kwa sababu ninaaminiwa,"amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news