NA DIRAMAKINI
MAMLAKA ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) pamoja na Taasisi ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) zimekutana na kufanya kikao cha jinsi ya kutoa huduma ya mawasiliano ya intaneti (Wireless Internet) kwenye Uwanja wa Maonesho wa Mwalimu J.K Nyerere ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Kikao hicho kimefanyika Juni 8, 2023 katika Ofisi za TanTrade jijini Dar es Salaaam kwa lengo la kuboresha na kurahisisha miundombinu ya mawasiliano ili kuwasaidia washiriki pamoja na watembeleaji kuweza kupata mawasiliano kwa njia rahisi na haraka zaidi katika kipindi chote cha maonesho hayo.
Akizungumza katika kikao hicho, Bw. Fortunatus Mhambe, Kaimu Mkurugenzi wa Ukuzaji Biashara, TanTrade kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, Bi. Latifa M. Khamis ameishukuru Taasisi ya UCSAF kwa kutoa huduma hiyo inayolenga kurahisisha mawasiliano na kuboresha maonesho yawe na mvuto zaidi.
