NA MWANDISHI WETU
MAMLAKA ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) wameazimia kuboresha na kukarabati miundombinu ya ndani na nje ya Uwanja wa Maonesho wa Mwalimu J.K Nyerere uliopo barabara ya Kilwa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es salaam.
Hayo yamebainishwa katika kikao kazi ambacho kimefanyika Juni 15, 2023, katika ofisi za TanTrade jijini Dar es salaam na kuhudhuliwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania, Bi.Latifa M. Khamis, na Wataalam kutoka TANROADS, Mhandisi Haruin Rashid Senkuku, Mhandisi Elisony Edward Mweladzi, Mhandisi Raymond Godfrey Maimu pamoja na wajumbe wa mkutano huo kutoka TanTrade.
Akiongea katika kikao hicho, Bi.Latifa amesema, wameamua kushirikiana na TANROADS katika kuboresha miundombinu ya viwanja ili kuchochea mabadiliko makubwa na kuyapa zaidi mvuto maonesho ya mwaka huu pamoja na kuleta urahisi wa kufanya biashara.
"Lengo ni kuendelea kuboresha miundombinu ya maonesho ili kuweka mazingira mazuri ya uoneshaji wa bidhaa kwa wafanyabiashara pamoja na watembeleaji na kuleta matokeo yenye tija," alisema.