TANZANIA, BORA KUISHANGILIA-23: KARIBU SIMIYU, PAMBA NI NYINGI

NA LWAGA MWAMBANDE

HISTORIA inaonesha kuwa, Mkoa wa Simiyu ulianzishwa kwa Tangazo la Serikali (GN) Na. 72 la Machi 2, 2012. 

Aidha, mkoa huo unapatikana Kaskazini mwa Tanzania, Kusini Mashariki mwa Ziwa Victoria. Mkoa huu upo kati ya longitudo 33°03” na 34°01” Mashariki ya mstari wa Griniwichi na latitudo 02°01” hadi 04°00” Kusini mwa Ikweta. 

Kwa upande wa Kaskazini, Mkoa wa Simiyu unapakana na Mkoa wa Mara, upande wa Mashariki mikoa ya Arusha Singida na Manyara, Kusini Mkoa wa Shinyanga na Tabora na upande wa Magharibi Mkoa wa Mwanza.

Pia, Mkoa wa Simiyu una eneo la kilomita za mraba 23,807.70. Eneo linalofaa kwa shughuli za kilimo na ufugaji ni kilomita za mraba 11,479.10 kilomita za mraba 11,723.60 ni eneo la Hifadhi ya Taifa ya Mbuga ya Serengeti, Mapori ya Akiba ya Maswa, Kijereshi na Mwiba na Hifadhi za Jumuiya za Wanyama Pori ya Makao (WMAs) iliyoko katika Wilaya ya Meatu na kilometa za mraba 605 ni eneo la maji ya Ziwa Victoria.

Vile vile, hali ya mvua kwa mwaka ni wastani wa kati ya 600mm hadi 900mm. Katika baadhi ya maeneo (Meatu) kiasi cha mvua ni 400mm. 

Hali ya joto ni kati ya 18°C hadi 31°C. Kwa ujumla, kuna misimu miwili ya mvua kwa maana ya msimu wa mvua za vuli kati ya mwezi Oktoba hadi Desemba na ule wa masika kati ya miezi ya Februari na Mei kila mwaka.
Mazao ya biashara yanayolimwa Mkoa wa Simiyu ni pamba ambayo inazalishwa kwa asilimia 47 ya pamba yote inayozalishwa nchini. 

Huku mazao mengine yakiwa ni alizeti, dengu na choroko na mazao makuu ya chakula ni mahindi, mtama, uwele, mpunga,viazi vitamu, mihogo, dengu,maharage na jamii nyingine ya mikunde.Ufugaji ni shughuli kuu ya pili ya kiuchumi katika Mkoa wa Simiyu.

Wakati huo huo, shughuli za uvuvi zinafanyika katika Wilaya ya Busega ambayo ina eneo la Ziwa Victoria lenye kilomita za mraba 605 na inatoa mchango mkubwa katika maendeleo ya wilaya, mkoa na Taifa kwa ujumla.

Mkoa wa Simiyu unaundwa na wilaya tano zenye majimbo saba ya Uchaguzi wa Ubunge ikiwemo Itilima, Bariadi, Maswa Mashariki, Maswa Magharibi, Busega, Kisesa na Meatu na halmashauri sita. Mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anasema kuwa,ukitaka kuifahamu pamba vizuri basi karibu mkoani Simiyu. Endelea; 

1. Simiyu ninaingia,
Mkoa wa Tanzania,
Ni mpya kiangalia,
Wenye makubwa lakini.

2. Nusu ya pamba sikia,
Ilimwayo Tanzania,
Simiyu watufanzia,
Tembelea mashambani.

3. Tumbaku mifugo pia,
Simiyu vimetulia,
Uchumi wanachangia,
Unatufaa nchini.

4. Viwanda ukisikia,
Pamba kutuchambulia,
Huko ndiko vyajazia,
Hizo ajira nchini.

5. Bariadi nakwambia,
Mji huo wavutia,
Walivyoupangilia,
Maendeleo nchini.

6. Nako Wasukuma pia,
Ni wengi wamejazia,
Tembelea furahia,
Utajiri Tanzania.

7. Huko watu kisikia,
Hasa ni Watanzania,
Ukarimu mwingi pia,
Ni jadi hapa nchini.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news