TANZANIA, BORA KUISHANGILIA-33: MARAIS WA TANZANIA

NA LWAGA MWAMBANDE

UTAWALA wa Jamhuri ya Muungano unaundwa na viongozi wakuu ambao ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Rais, Rais wa Zanzibar, Waziri Mkuu na Baraza la Mawaziri.
Rais wa Jamhuri la Muungano ndiye Mkuu wa nchi, Mkuu wa Serikali, Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama.

Pia, Rais ndiye kiongozi wa Utawala wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Makamu wa Rais ndiye msaidizi mkuu wa Rais kwa mambo yote ya Jamhuri ya Muungano kwa ujumla na hasa ana wajibu wa kumsaidia Rais katika;

i. Kufuatilia utelekezaji wa kila siku wa mambo ya Muungano

ii. Kufanya kazi zote atakazopewa na Rais

iii. Kufanya kazi zote na majukumu ya ofisi ya Rais, wakati Rais asipokuwepo au anapokuwa nje ya nchi.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano ndiye Kiongozi wa shughuli za Serikali Bungeni na ana mamlaka ya kuthibitisha, kusimamia na kutelekeza kazi za kila siku na mambo ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha anatekeleza jambo lolote ambalo Rais atamwelekeza kuwa lifanywe.

Rais wa Zanzibar ndiye Kiongozi wa Utawala wa Zanzibar, Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi la Zanzibar.

Baraza la Mawaziri ni pamoja na Waziri Mkuu, anayeteuliwa na Rais kutokana na Wabunge wa Bunge la Taifa. Serikali inatekeleza kazi zake kupitia kwa Wizara zinazoongozwa na Mawaziri. Kila wizara ina dhmana ya kazi na sekta yake.

Mwalimu Nyerere (1964 hadi 1985)

Tangu Uhuru, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hadi sasa imeongozwa na marais sita, aliyeanza kuliongoza jahazi hilo ni Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais wa Kwanza wa Tanzania alizaliwa Aprili 13, mwaka 1922 katika Kijiji cha Butiama, Wilaya ya Musoma katika Mkoa wa Mara. Alikuwa mtoto wa Chifu Nyerere Burito na Bibi Christina Mugaya Wanyang’ombe. 

Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na viongozi wenzake wa awamu ya kwanza walielekeza juhudi zao katika kuwaunganisha Watanzania na kuweka misingi imara ya kuijenga taifa, kudumisha uhuru na amani na kuweka itikadi na sera za kukabili ujinga, umaskini na maradhi. 

Aidha, awamu hiyo iliweka misingi madhubuti ya uhusiano wa nje ikiwa ni pamoja na sera ya kutofungamana na siasa za upande wowote, msisitizo katika ukombozi wa Bara la Afrika na mapambano dhidi ya ubeberu na vibaraka wao.

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Azimio la Arusha lililosisitiza siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, na kuundwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni matunda ya uongozi wa awamu ya kwanza. 

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alifariki dunia katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas iliyoko jijini London, Uingereza tarehe 14 Oktoba, 1999. Kutokana na mchango wake mkubwa kama muasisi wa Taifa hili, Mwalimu Nyerere ataendelea kukumbukwa kuwa Baba wa Taifa.

Ali Hassan Mwinyi (1985 hadi 1995)

Mheshimiwa Alhaj Ali Hassan Mwinyi aliyeongoza Serikali ya Awamu ya Pili aliingia madarakani rasmi Novemba 5, 1985. Mheshimiwa Alhaj Ali Hassan Mwinyi alizaliwa Kivule, Mkuranga Mkoa wa Pwani tarehe 5 Mei, 1925. 

Alikuwa mwalimu wa shule za msingi za Mangapwani na Bumbwini, Zanzibar. Kisiasa, Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi alijiunga na Chama cha Afro Shiraz (ASP) mwaka 1964 na kushika nyadhifa mbalimbali za Serikali ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Miongoni mwa nyadhifa hizo ni Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu Zanzibar 1963, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1970 na kati ya mwaka 1982 hadi 1983 alikuwa Waziri wa Afya, Wizara ya Mambo ya Ndani, Maliasili na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Misri. Mwaka 1984 alichaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Benjamin William Mkapa (1995 hadi 2005)

Hayati Benjamin William Mkapa aliongoza Serikali ya Awamu ya Tatu na ni Rais wa kwanza aliyechaguliwa katika uchaguzi ulioshirikisha vyama vingi vya siasa tangu mfumo huo uliporejeshwa mwaka 1992. 

Aliingia rasmi madarakani Oktoba 1995. Mheshimiwa Mkapa alizaliwa Masasi mkoani Mtwara tarehe 12 Novemba, 1938. 

Mwaka 1962 aliajiriwa kama Ofisa Tawala na hatimaye Ofisa Mambo ya Nje. Kati ya mwaka 1966 na 1976 alifanya kazi katika taasisi mbalimbali za umma. 

Mwaka 1976 hadi mwaka Septemba, 1995 alishika nyadhifa za Balozi wa Tanzania nchini Nigeria (1976; Mbunge wa Nanyumbu na Waziri wa Mambo ya Nje (1977-1980), Waziri wa Habari na Utamaduni (1980-1982), Balozi wa Tanzania nchini Canada (1984-1990), Waziri wa Habari na Utangazaji (1990), Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu (1992-Septemba 1995).

Dkt.Jakata Mrisho Kikwete (2005 hadi 2015)

Rais mstaafu Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete alizaliwa Oktoba 7, mwaka 1950 Msoga Mkoa wa Pwani ni mtoto wa sita katika familia ya watoto tisa. Amemuoa mama Salma Kikwete na wamebarikiwa watoto nane.

Mwaka 1976 alijiunga na Chuo Kikuu cha Maofisa wa Jeshi Monduli na kutunukiwa Cheo cha Luteni Kanali na baadaye kuwa Mkufunzi Mkuu na Kamisaa wa Siasa katika chuo hicho. 

Mheshimiwa Dkt.Kikwete amefanya kazi katika Chama Cha Mapinduzi kwa nyadhifa mbalimbali kwenye mikoa ya Singida na Tabora na wilaya za Nachingwea na Masasi.

Mwaka 1988 aliteuliwa kuwa Mbunge na Naibu Waziri wa Nishati na Madini. Mwaka 1990 alichaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo na akateuliwa kuwa Waziri wa Wizara ya Maji, Nishati na Madini. 

Nyadhifa nyingine alizoshika ni Waziri wa Fedha mwaka 1994 na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kuanzia mwaka 1995 hadi 2005.Alishika rasmi wadhifa wa urais mwaka 2005 na kuchaguliwa tena 2010 kwa muhula mwingine wa miaka mitano.

Dkt.John Magufuli (2015 hadi 2021)

Hayati Dkt.John Pombe Joseph Magufuli alizaliwa Oktoba 29, 1959 wilayani Chato Mkoa wa Kagera ambayo hivi sasa ipo Mkoa wa Geita. Dkt.Magufuli amemuoa Mwalimu Janet na wamejaliwa kupata watoto.

Harakati zake za kisiasa zilianza mwaka 1995 alipogombea kiti cha ubunge katika Jimbo la Chato na kuteuliwa kuwa Naibu Waziri katika Wizara ya Ujenzi. Mwaka 2000, Dkt.Magufuli aligombea na kushinda kwa mara ya pili na kuteuliwa kuwa Waziri wa Wizara ya Ujenzi.

Aidha, katika chaguzi za mwaka 2005 na 2010, aliendelea kuwania kiti cha ubunge katika Jimbo la Chato na kushinda uchaguzi huo na kuteuliwa kuwa Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi hadi mwaka 2008 alipohamishiwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ambayo aliiongoza hadi mwaka 2010. Mwaka 2010 alipochaguliwa tena kuwa Mbunge wa Chato aliteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi.

Dkt.Samia Suluhu Hassan (2021 hadi sasa)

Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan alizaliwa Januari 27, 1960 katika Kijiji cha Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja. Ameolewa na Bw. Hafidh Ameir na wamejaliwa watoto wanne, watatu wa kiume na mmoja wa kike.

Mhe. Samia Suluhu Hassan alipata elimu ya msingi katika shule mbalimbali, zikiwemo Shule ya Msingi Chwaka iliyoko Unguja kuanzia 1966 hadi 1968, Shule ya Msingi Ziwani mwaka 1970 na Shule ya Msingi Mahonda mwaka 1972. 

Baada ya hapo, alijiunga na Shule ya Sekondari ya Ng’ambo kwa ajili ya masomo ya Kidato cha Kwanza hadi cha tatu, na Shule ya Sekondari Lumumba kwa ajili ya Kidato cha Nne kati ya mwaka 1973 hadi 1976.

Mwaka 1983, alipata Astashada katika Mafunzo ya Takwimu kutoka Chuo cha Uchumi, Zanzibar. Baada ya kufanya kazi kwa kipindi kifupi kwenye Wizara ya Mipango na Maendeleo, mwaka 1983 hadi 1986, alijiunga na Chuo cha Maendeleo ya Uongozi Mzumbe (IDM) kwa ajili ya masomo ya juu katika Utawala wa Umma. 

Aidha, alipata mafunzo mbalimbali katika Taasisi ya Chuo cha Utawala wa Umma Lahore, Pakistan 1987, Taasisi ya Eastern and Southern African Management Institute (ESAMI) 1991, na Taasisi ya Uongozi ya Hyderabad India 1998 kwa ajili ya Astashahada ya Utawala. 

Baada ya hapo, alijiunga na Chuo Kikuu cha Manchester kilichopo Uingereza kwa ajili ya masomo ya Juu ya Uchumi. Vilevile, alipata Shahada ya Uzamili ya Maendeleo ya Jamii kupitia programu ya pamoja kati ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na Chuo Kikuu cha Southern New Hampshire, Marekani.

Dkt.Samia ni Rais wa Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). 

Aliapishwa Machi 19, 2021 kufuatia kifo cha ghafla cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt.John Pombe Joseph Magufuli. 

Dkt.Samia ni mwanamke wa kwanza nchini kushika nafasi za Makamu wa Rais na hatimaye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Nyadhifa nyingine alizoshika ndani ya Serikali ni Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia mambo ya Muungano 2010/2015, Waziri wa Utalii, Biashara na Uwekezaji katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar 2005/2010 na Waziri wa Kazi, Vijana, Ajira, Maendeleo ya Wanawake, na Watoto, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mwaka 2000/2005. 

Mwaka 2014, alihudumu kama Makamu Mwenyekiti wa Bunge lililojadili Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kuandaa rasimu ya Katiba mpya ya Tanzania. Mwaka 1987 hadi 1988, alikuwa Afisa Mipango Rasilimali Watu na Mwaka 1977 hadi 1983, Karani Masijala.

Mheshimiwa Dkt.Samia aliingia katika siasa kama mwanachama wa CCM Juni 10, 1987. Aliingia katika siasa za uchaguzi mwaka 2000 katika nafasi ya Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Zanzibar kama Mwakilishi wa Viti Maalum vya Wanawake hadi mwaka 2010. 

Kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, aligombea na kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwakilisha jimbo la Makunduchi, Zanzibar.

Mwaka 2002, alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi, na vile vile, kuteuliwa kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi, nyadhifa ambazo ameendelea kuzifanyia kazi hadi leo. 

Dkt.Samia ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, Mkutano Mkuu wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja; na alikuwa Mjumbe wa Kamati za Siasa Mkoa na Wilaya ya Kusini Unguja.

Kwa upande wa Jumuiya za Chama Cha Mapinduzi,Dkt.Samia ni mwanachama wa Jumuiya ya Wanawake wa Tanzania (UWT) kuanzia mwaka 1996 hadi leo. 

Aidha, ameshiriki katika kuandika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi mara nne mfululizo kuanzia 2005/2010, 2010/2015, 2015/2020 na 2020/2025.

Mwaka 2016, Mhe. Dkt.Samia aliteuliwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw.Ban Ki Moon, kuwa Mjumbe wa Jopo la Umoja wa Mataifa kuhusu Uwezeshaji wa Wanawake Kiuchumi, akiwakilisha Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika kati ya mwaka 2016 na 2017. 

Katika kipindi cha ujumbe wake, aliwasilisha mambo 27 kwenye jopo hilo, ambayo Serikali ya Tanzania ilibainisha kama hatua za kimkakati kwa ajili ya kuweka mfumo endelevu wa kufikia usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake kiuchumi.

Miongoni mwa matokeo ya kazi zake ni kusimamia uanzishwaji wa majukwaa ya uchumi ya wanawake nchini kwa lengo la kuwaunganisha wanawake wafanyabiashara wadogo na wakati kwenye masoko, hasa wanawake wanaoishi mipakani, kuwaunganisha na mikopo nafuu na kuhimiza mafunzo ya ujasiriamali.

Na kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kuanzisha kampeni ya kuongeza uwajibikaji katika kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto, maarufu kama “Jiongeze Tuwavushe Salama”.

Mhe.Dkt.Samia amefanya kazi na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (World Food Programme) mwaka 1988 hadi 1997. 

Vile vile, amefanya kazi katika Kamati, Bodi na Taasisi mbalimbali kama vile Mjumbe wa Kamati ya Msamaha wa Wafungwa (Parole Committee) ya Zanzibar (2001- 2010), Mlezi wa Jumuiya ya Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi Zanzibar (1997-2000), 

Mjumbe wa Bodi ya Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote – EOTF (1996-2000), Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Taasisi zisizo za Kiserikali Zanzibar (ANGOZA) 1995-2000, Mwanachama wa Lions Club Zanzibar (1991-1998), Mjumbe wa Kamati ya Uundaji wa Sera ya Elimu Zanzibar (1996) na Mwanachama Mwanzilishi wa Taasisi ya Kuchochea Maendeleo ya Wanawake Zanzibar (1991-1994). 

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, viongozi wetu wakuu wamekuwa nguzo muhimu kwa Taifa letu ikiwemo kuwaunganisha Watanzania, kuendeleza umoja, mshikamano na kudumisha amani ndani na nje ya nchi. Endelea;

1.Marais Tanzania,
Wote nimewatajia,
Nyerere liasisia,
Ukisoma vitabuni.

2.Nchi tulojipatia,
Lugha lisisitizia,
Sasa kote Tanzania,
Kiswahili mdomoni.

3.Umoja twajivunia,
Nchi yetu Tanzania,
Kwa Nyerere lianzia,
Tunaishi kwa amani.

4.Ujamaa alinia,
Azimio kumbukia,
Vijiji vikaingia,
Tukaondoka porini.

5.Jitegemee sikia,
Mwalimu lisitizia,
Lengo tuache tumia,
Omba omba ugenini.

6.Pale tulipofikia,
Mengi tulijipatia,
Ingawa tulifulia,
Changamoto duniani.

7.Shule tuliopitia,
Na jeshini kuingia,
Ukabila kusikia,
Likuwa siyo nchini.

8.Kote tulijifunzia,
Na hata kujikalia,
Kazi tulijifanyia,
Ni hadi sasa nchini.

9.Wengi wakiangalia,
Vile tunajiishia,
Makabila zidi mia,
Wanashangaa amani.

10.Nyerere kumsifia,
Alivyotusimamia,
Jema alitufanyia,
Sifa kote duniani.

11.Mwalimu lotufanyia,
Nyumbani hakusalia,
Alivuma nakwambia,
Kote kote duniani.

12.Muungano Tanzania,
Wa pekee nakwambia,
Japo kero wapitia,
Ni imara duniani.

13.Bila kuusimamia,
Nyerere ungetitia,
Bunge lilipoingia,
Kutaka upiga chini.

14.Jinsi walitingishia,
Tanganyika jidaia,
Nyerere singeingia,
Pengine ngepigwa chini.

15.Muungano pambania,
Ili usijefifia,
Hoja alozotumia,
Hamsina tano chini.

16.Wabunge lijidaia,
Wamechoka Tanzania,
Tanganyika hitajia,
Nyerere lipiga chini.

17.Akawafafanulia,
Asili ya Tanzania,
Maneno kawaingia,
Presha kashuka chini.

18.Kipindi tulipitia,
Kwa kweli kilitishia,
Muungano Tanzania,
Ungeingia shidani.

19.Kitu alituachia,
Nyerere ninakwambia,
Vigumu kufikiria,
Kwa walio kileleni.

20.Madaraka liachia,
Anapendwa Tanzania,
Mshauri katulia,
Miaka mingi nchini.

21.Nje ninasimulia,
Jinsi fora alitia,
Ambayo yanabakia,
Kumuweka kileleni.

22.Ukombozi lipania,
Kwingi aliuchangia,
Wengi wanamsifia,
Kazi yake ya thamani.

23.Si Malawi na Zambia,
Angola na Namibia,
Yeye alisaidia,
Uhuru wakasaini.

24.Msumbiji kisikia,
Wanajeshi lichangia,
Uhuru kujipatia,
Na Afrika ya Kusini.

25.Mengi alitufanyia,
Kisoma tayajulia,
Mwalimu hakusalia,
Kaenda kwa Maanani.

26.Ali Mwinyi liingia,
Nchi akashikilia,
Zanzibar na Tanzania,
Kaongoza bila soni.

27.Nchi ilipofikia,
Wakati anaingia,
Sitaki kukuambia,
Tulitokea vitani.

28.Amini Nduli sikia,
Alishatuvurugia,
Kagera kushambulia,
Uchumi ukawa chini.

29.Tulimpiga kwa nia,
Nguvu tulivyojitia,
Shida zikatuingia,
Tukabaki taabani.

30.Tena hali ya dunia,
Mafuta yakaingia,
Bei tusizojulia,
Zikatuchoma nchini.

31.Mwinyi alipoingia,
Uchumi ulishavia,
Bila maamuzi nia,
Tungelienda shimoni.

32.Kitini hakutulia,
Mageuzi kufanyia,
Ujamaa kaachia,
Kuileta ahueni.

33.Mengi alitufanyia,
Machache ntawatajia,
Hapa tulipofikia,
Mwinyi yuko hesabuni.

34.Biashara lianzia,
Watu kuchangamkia,
Pesa wakazifikia,
Zikajaa mifukoni.

35.Kazi walizikimbia,
Biashara kuvamia,
Pesa walijipatia,
Ukwasi kote nchini.

36.Fagio la chuma pia,
Yeye alilitumia,
Wachafu kuwafagia,
Wasilete shida ndani.

37.Vyama vingi kuingia,
Yeye alisimamia,
Kwa busara lichangia,
Hatukufika vitani.

38.Mengi walimtupia,
Madongo livumilia,
Ruksa lituambia,
Tukaishi kwa amani.

39.Mwisho litukabidhia,
Awamu ya tatu pia,
Huyo naye liingia,
Akitokea kusini.

40.Baba Mwinyi katulia,
Akijipumzikia,
Bado anatupatia,
Hekima zake makini.

41.Salim Salim pia,
Daktari nawambia,
Maarufu Tanzania,
Hata kote duniani.

42.Bara letu nakwambia,
Kiti alikikalia,
Mengi alisimamia,
Uhuru wetu barani.

43.Kidogo angeishia,
Katibu Mkuu pia,
Figisu twakumbukia,
Ilifanya Marekani.

44.Waziri Mkuu pia,
Cheo alishikilia,
Yeye alisaidia,
Uchumi huru nchini.

45.Tunamuenzi sawia,
Kiongozi Tanzania,
Afya tunamtakia,
Na maisha ya amani.

46.Zanzibar ni Tanzania,
Ni vema kupafikia,
Mengi utajifunzia,
Elimu na burudani.

47.Mji Mkongwe sikia,
Ni urithi wa dunia,
Mitaa ukipitia,
Taburudika moyoni.

48.Mimi napafagilia,
Vile nimepafikia,
Kile ninatamania,
Nawe pawe ni nyumbani.

49.Hii ndiyo Tanzania,
Yenye mema ya dunia,
Kama hujaisikia,
Wewe huko duniani.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news