TANZANIA, BORA KUISHANGILIA-34: HARAKATI ZA UHURU

NA LWAGA MWAMBANDE

NDANI ya mwaka huu Tanzania Bara inaadhimisha miaka 62 ya Uhuru wa iliyokuwa Tanganyika ambao kupatikana kwake kulihitimisha enzi ya ukoloni wa Uingereza mnamo Desemba 9, mwaka 1961.

Tanganyika ambayo mwaka mmoja baada ya Uhuru ilitangazwa kuwa Jamhuri, ilijiunga na iliyokuwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar mwaka 1964 kuunda taifa jipya la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha, Desemba 9 mwaka 1961 mambo makubwa mawili yalifanyika kama sehemu ya maadhimisho ya Uhuru wa Tanganyika.

Mosi ilikuwa ni kushusha chini bendera ya mkoloni na kupandisha ya taifa huru na wakati huo huo kupandisha Mwenge wa Uhuru kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro mkoani Kilimanjaro.

Tukio la kupandisha bendera lilifanyika katika Uwanja wa Uhuru uliopo jijini Dar es Salaam, uwanja uliojengwa mahususi kwa ajili ya sherehe za Uhuru.

Inaelezwa kuwa, umuhimu wake ulikuwa kuonesha kuondoka kwa mkoloni na kwamba kuanzia wakati huo Watanganyika (kwa sasa Watanzania) watakuwa huru kufanya mambo yao wenyewe kwa mustakabali wao.

Pia, kushushwa kwa bendera hiyo kulikuwa ni tukio kubwa kwa waliolishuhudia, kwani kuna wazee wa zamani wamekuwa wakizungumza kuhusu vilio vya furaha vilivyosikika wakati wa tukio hilo lililofanyika saa sita usiku.

Vivyo hivyo mkoani Kilimanjaro, tukio hilo halikujulikana maana yake sana hadi pale Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipozungumza maneno yafuatayo kuhusu tukio hilo la kuwasha Mwenge wa Uhuru.

"Tunataka kuwasha Mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, umulike hata nje ya mipaka yetu; ulete tumaini pale ambapo hakuna matumaini, upendo mahali palipo na chuki na heshima palipojaa dharau."

Mwenge huo uliwekwa juu ya Mlima Kilimanjaro na shujaa Luteni Kanali Alexander Nyirenda ambaye kwa sasa ni marehemu huku baba wa Taifa akisisitiza kuwa, una umuhimu mkubwa katika kuijenga Tanzania yenye umoja, mshikamano na upendo miongoni mwa wananchi wake na kusababisha nchi kuwa miongoni mwa zinanzosifika kwa amani na utulivu duniani kote.

Aidha, ndiyo sababu, kila wakati Taifa linawajibika kujikumbusha bila ya kuchoka juu ya dhana na falsafa hiyo kupitia maneno ya busara, hekima, uzalendo na upendo yaliyotamkwa na Mwalimu Nyerere kabla na baada ya Uhuru.

Maneno ya Mwalimu yalikuwa na maana kubwa na yanaendelea kuwa na maana hata kwa sasa. Mwenge umekuwa ukikimbizwa nchi nzima ukipita kwenye vitongoji, mitaa, vijiji, wilaya na mikoa bara na visiwani na umeendelea kuwakumbusha Watanzania wajibu wa kufanya kazi kwa bidii ili kuleta maendeleo huku ukitumika kuzindua miradi mbalimbali kila mwaka kwenye maeneo unakopita.

Ingawa, Mwalimu Nyerere alikuwa Waziri Mkuu -kwa maana ya Mkuu wa Serikali, na Malkia wa Uingereza akiendelea kuwa Mkuu wa Dola katika mwaka wa kwanza wa Uhuru, Tanzania ilikuwa huru kujiamulia mambo yake.

Katika miaka ya kwanza ya Uhuru, Tanzania ilijipambanua kama taifa linaloamini katika Umajumui wa Afrika (Pan-Africanism) Nyerere akielezwa kuwa tayari kusubiri Tanzania isiwe huru ili Jomo Kenyatta aachiwe kutoka jela Kenya kuja kuwa Rais wa Shirikisho la Afrika Mashariki na kushiriki katika harakati za kumkomboa mtu mweusi barani Afrika na kwingine duniani.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anabainisha kuwa, tunapoelekea kuadhimisha miaka 62 ya Uhuru, Tanzania ina mengi ya kujivunia katika nyanja mbalimbali ikiwemo elimu, afya, diplomasia, uchumi na nyingine mbalimbali huku akipeleka kongole kwa wote ambao walihusika kwa namna moja au nyingine kufanikisha kupatikana Uhuru. Endelea;

1.Majina nikipitia,
Vizuri kuwasifia,
Wale waliochangia,
Uhuru hapa nchini.

2.TAA ilikoanzia,
Hata TANU kufikia,
Kazi walishikilia,
Ya siasa sio dini.

3.Haki walipigania,
Mali zao kutumia,
Kofia kuwavulia,
Ni jambo jema jamani.

4.Majina nikianzia,
Kutaka kuwatajia,
Yote sitayafikia,
Walokuwa kileleni.

5.Itoshe kuwatajia,
Uhuru lipigania,
Heshima twajivunia,
Mchango mkubwa dini.

6.Wakristo wapo pia,
Pamoja tawatajia,
Maarufu kisikia,
Watajwa kote nchini.

7. Dossa Ali naanzia,
Babu ninakutajia,
Uhuru lipigania,
Kutokea mfukoni.

8.Gari la kwanza sikia,
TANU kujimilikia,
Pesa alinunulia,
Toka kwake mfukoni.

9.Kina Sykes pia,
Uhuru lipigania,
Majinayo kisikia,
Alwatani jijini.

10. Si kwa maneno sikia,
Jinsi walivyochangia,
Kwa vitendo nakwambia,
Kumshinda mkoloni.

11.TAA ilikoanzia,
Uongozi shikilia,
Sykes limwachia,
Ticha Nyerere kitini.

12.Bibi Titi mesikia?
Jina nimekutajia,
Dasalamu mepitia,
Usome barabarani?

13.Mwanamke nakwambia,
Siasa lishikilia,
Uhuru lipigania,
Hadi ushindi nchini.

14.Wengine nakutajia,
Maarufu Tanzania,
Mbali walikoanzia,
Wazee wa zote dini.

15.Kandoro ukisikia,
Na hata John Rupia,
Kwa kweli walichangia,
Siasa hapa nchini.

16. Majina ukisikia,
Wanao watumikia,
Mbali walikoanzia,
Toka enzi ukoloni.

17.TANU tunajivunia,
Uhuru kupigania,
Nani anayejulia,
Livyoanzishwa nchini?

18.Hapa ninakuambia,
Pitia historia,
Wale walijadilia,
Hadi ikawa kitini.

19.Nyerere wamsikia,
Dossa Mzee Rupia,
Sykes wawili pia,
Walikaa ofisini.

20.TANU kuiasisia,
Ni masanduku ya bia,
Viti walivyokalia,
Chama kuwa kitabuni.

21.Chumba walichokalia,
Cha TAA sikilizia,
Vile wanasimulia,
Likuwa duni samani.

22.TANU tunajivunia,
Huko waliasisia,
Mengine kusimulia,
Yajulikana nchini.

23.Wangapi walisikia,
Kuhusu Erika Fiah,
Kwa kutuhabarishia,
Na Ramadhani Plantani?

24.Gazeti la kwake Fiah,
Kwetu hujalisikia,
Cheche lilimiminia,
Dhidi yao wakoloni.

25.Hilo ndo lilianzia,
TANU kuitangazia,
Sera zake kufikia,
Mijini na vijijini.

26.Wengi walipigania,
Uhuru kukutajia,
Itoshe kukuambia,
Hao ni wengi nchini.

27.Tanganyika kisikia,
Wengi walipigania,
Pwani kama waanzia,
Uelekee kusini.

28.Kaskazi kianzia,
Magharibi sikizia,
Mengi walitufanyia,
Tunafaidi nchini.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news