Tanzania inasonga mbele kiuchumi-Waziri Dkt.Mwigulu

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt.Mwigulu Nchemba amesema,Tanzania inaendelea kusonga mbele kiuchumi licha ya mataifa mbalimbali duniani kupitia katika kipindi kigumu kiuchumi.

Mheshimiwa Dkt.Nchemba ameyasema hayo leo Juni 15, 2023 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

"Nchi yetu inasonga mbele licha ya nchi zote duniani kupita kwenye misukosuko ya kiuchumi. Kwa mujibu wa jarida la uchumi la Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) la Aprili 2023, uchumi wa Tanzania unatarajiwa kufikia dola za Marekani bilioni 85.4 mwaka 2023 kutoka dola bilioni 69.9 mwaka 2021,"amefafanua Mheshimiwa Waziri Dkt.Nchemba.

Amebainisha kuwa, Tanzania imepanda hadi nafasi ya sita ikilinganishwa na nchi nyingine Kusini mwa Jangwa la Sahara ikiongozwa na nchi za Kenya (dola bilioni 116.0), Ethiopia (dola bilioni 120.4),Angola (dola bilioni 121.4), Afrika Kusini (dola bilioni 405.7) na Nigeria (dola bilioni 477.4).

Nchi nyingine zenye uchumi mkubwa chini ya Tanzania, Waziri Dkt.Mwigulu amesema ni Ghana (dola bilioni 72.8), Cote d'Ivoire (dola bilioni 70.0), Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (dola bilioni 62.8) na Uganda (dola bilioni 48.8).
 
"Hivyo, watanzania tunapotoa mifano ya wapi tunaelekea tuyajue mataifa yalioko mbele yetu. Na kwa programu hizi alizoanzisha Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM, za kuwekeza kwenye sekta za uzalishaji na kukuza uwekezaji na uwezeshaji wananchi kiuchumi siku sio nyingi mataifa mengi tutayavuka,"amesema.

Pia, Mheshimiwa Waziri Dkt.Nchemba amesema, Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilianza mchakato wa kufanyiwa tathmini ya uwezo wa kukopa na kulipa madeni (sovereign credit rating) mwaka 2008 ambapo zoezi hilo halikukamilika kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mdororo wa uchumi pamoja na kuyumba kwa soko la fedha duniani.

Hata hivyo, Dkt.Nchemba amesema chini ya uongozi thabiti wa Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan, Serikali imefanikiwa kukamilisha zoezi hilo ambalo lilikuwa ni kikwazo katikautafutaji fedha na mitaji katika masoko ya kimataifa.

Pia amebainisha Machi 2023,kampuni za Fitch Ratings na Moody’s Investors Service zilianza zoezi la kuifanyia nchi tathmini ya kukopesheka katika masoko ya fedha ya kimataifa.

Waziri Dkt.Nchemba amesema, zoezi hilo lilikamilika ambapo kampuni ya Moody’s Investors Service ilichapisha matokeo ya tathmini hiyo mwezi Mei 2023 na kampuni ya Fitch Ratings mwezi Juni 2023.

Kwa mujibu wa matokeo hayo, Kampuni ya Moody’s Investors Service imeipa Tanzania daraja la B2 POSITIVE na Kampuni ya Fitch Ratings daraja la B POSITIVE, ambayo yanaashiria taswira chanya kwa nchi kimataifa.

"Matokeo hayo ni bora kuliko nchi nyingine za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Pamoja na mambo mengine, matokeo hayo yamechangiwa na mwenendo mzuri wa ukuaji wa uchumi, usimamizi makini wa deni la Taifa, kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji kwa sekta binafsi, kuimarisha ushirikiano wa kimataifa pamoja na kuleta maridhiano ya kisiasa ndani ya nchi.

"Kukamilika kwa zoezi hilo, kutaiwezesha nchi kutambulika katika masoko ya fedha ya kimataifa na hivyo, kuongeza sifa za kuvutia uwekezaji na kupanua wigo wa upatikanaji wa fedha kwa miradi ya Serikali na sekta binafsi,"amefafanua Mheshimiwa Waziri Dkt.Mwigulu.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt.Mwigulu Nchemba akionesha mkoba wenye Bajeti Kuu ya Serikali 2023/24 ya shilingi trilioni 44.39 aambazo zinatarajiwa kukusanywa na kutumika. Jumla ya mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa shilingi trilioni 31.38, sawa na asilimia 70.7 ya bajeti yote. Kati ya mapato hayo, mapato yatakayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania yanakadiriwa kuwa shilingi trilioni 26.73 na mapato yasiyo ya kodi (Wizara, Idara, Taasisi na Mamlaka za Serikali za Mitaa) yanakadiriwa kuwa shilingi trilioni 4.66.(Picha na WFM).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news