NA ELEUTERI MANGI-WUSM
KATIBU Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Saidi Yakubu amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Urusi nchini, Mhe. Andrey Avetisyan ambapo wamejadili namna bora ya Tanzania na Urusi kushirikiana katika sekta ya Utamaduni na Sanaa kwa manufaa wa wananchi wa pande hizo mbili.
Akiongea wakati wa kikao hicho kilichofanyika Juni 21, 2023, Katibu Mkuu Bw. Yakubu amesema Tanzania na Urusi wataendelea kushirikiana katika eneo la Utamaduni na Sanaa kwa kuzingatia uhusiano wa muda mrefu ulipo baina nchi hizo mbili katika masuala mbalimbali ikiwemo lugha ya Kiswahili.
“Tunatambua juhudi zinazofanywa nan chi ya Urusi kwa kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili, sisi tupo tayari kupitia BAKITA kutoa vitabu vya kujifunzia Kiswahili, tutatoa vitabu kwa walimu wa Kiswahili kutoka Urusi ambao watakuja hapa nchini wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani Julai 7 mwaka huu ili vitabu hivyo viwe nyenzo nzuri ya kufundishia lugha ya Kiswahili Urusi,” amesema Bw. Yakubu.
Kwa upande wake Balozi wa Urusi nchini Mhe. Andrey Avetisyan amesema nchi hiyo itaendelea kushirikiana na Tanzania katika Nyanja mbalimbali za maendeleo ambapo wataendelea kutoa nafasi kwa Watanzania kusoma nchini humo ambapo watajifunza pia lugha ya Kirusi ili kuendeleza mahusiano ya kibiashara na uchumi hatua inayoongeza nafasi kwa Watanzania kufanya kazi Urusi na Warusi kufanya kazi Tanzania.
Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) Bi. Consolata Mushi amesema watashirikiana na Ubalozi wa Urusi nchini ambapo wafundisha maafisa wa Ubalozi huo lugha ya Kiswahili kwa wageni na watashirikiana nao kufundisha wataalam wa tafsiri na ukalimani hatua itakayosaidia kueneza lugha ya Kiswahili duniani.