JAKARTA-Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefungua rasmi Ubalozi wake jijini Jakarta nchini Indonesia.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Ubalozi huo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) amesema kufunguliwa kwa Ubalozi huo kutaziwezesha Serikali ya Tanzania na Serikali ya Indonesia kukuza na kuimarisha uhusiano wake wa kidiplomasia na kukuza uchumi.
“Tanzania imekuwa ikishirikiana kwa karibu na Indonesia hivyo tunaamini kuwa kufunguliwa rasmi kwa ubalozi wetu Jijini hapa kutaongeza ushirikiano zaidi baina ya mataifa yetu mawili hususan katika sekta ya uchumi,” alisema Dkt. Tax.
Waziri Tax ameongeza kuwa Indonesia imefika mbali kiuchumi, hivyo ushirikiano wake na Tanzania utatoa fursa kwa Tanzania kupiga hatua na kuhakikisha bidhaa za mazao ya kilimo na madini zinaongezwa thamani na kuuzwa katika masoko mbalimbali ya kimataifa na kuiwezesha Tanzania kukuza uchumi wake.
Pamoja na mambo mengine, Dkt. Tax ameishukuru Serikali ya Indonesia kwa ushirikiano mkubwa ambao imekua ikiupatia Ubalozi wa Tanzania, Jakarta tangu ubalozi huo ulipoanzishwa nchini humo mwaka 2022 hadi ulipozinduliwa rasmi leo tarehe 22 Juni, 2023.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Indonesia Mhe. Retno Marsudi amesema, Indonesia na Tanzania zimekuwa na ushirikiano mzuri wa muda mrefu na imara ulioanzishwa na waasisi wa mataifa hayo mawili (Mwl. Julius Nyerere na Rais Sukarno) tangu mkutano wa Bandung uliofanyika mwaka 1955.
Waziri Marsudi alisema kuwa muda wote huo, Serikali hizo mbili zimekuwa zikifanya kazi kwa pamoja na kwa karibu katika maeneno mbalimbali…“Leo najisikia faraja sana kwa Tanzania kufungua rasmi ubalozi wake hapa Jakarta. Hii ni ishara ya kuimarisha zaidi ushirikiano baina ya Indeonesia na Tanzania,” amesema Mhe. Marsudi.
Alisema kufunguliwa kwa ubalozi huo kunaonesha kuimarishwa zaidi kwa uhusiano wa kidiplomasia uliopo kati ya Tanzania na Indonesia na kuahidi kuwa yeye na timu yake wataendelea kushirikiana na Tanzania kukuza na kuimarisha uhusiano uliopo kati ya nchi hizo.
“Kufunguliwa rasmi kwa ubalozi huu leo ni ishara ya kuimarisha zaidi uhusiano wetu wa kidiplomasia kati ya Indonesia na Tanzania, mimi pamoja na timu yangu tunaahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kukuza na kuimarisha uhusiano wetu,” ameongeza Mhe. Marsudi.
Hafla ya uzinduzi wa Ubalozi huo imehudhuriwa na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa waliopo Jakarta, Indonesia.
Tanzania na Indonesia zilianzisha rasmi uhusiano wa kidiplomasia mwaka 1964, ambapo mwaka huo Ubalozi wa Indonesia ulifunguliwa rasmi nchini Tanzania. Aidha, kabla ya kufunguliwa kwa ubalozi wa Tanzania nchini Indonesia, Tanzania imekuwa ikiwakilishwa kutoka ubalozi wa Tanzania uliopo Kuala Lumpur, Malaysia.