NA MWANDISHI WETU
JAMHURI ya Muungano wa Tanzania imezihimiza nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuendelea kushirikiana katika utekelezaji wa Mkataba wa Biashara ya Kimataifa wa Wanyama na Mimea iliyo hatarini kutoweka (CITES) ili kulinda na kuhifadhi wanyamapori na mimea hiyo.
Kauli hiyo imetolewa leo Juni 22, 2023 na Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Khamis Hamza Chillo (Mb) katika mkutano wa Mawaziri wa SADC wanaohusika na Mazingira, Maliasili na Utalii uliofanyika kwa njia ya mtandao jijini Dodoma leo.
“Wanachama wa SADC ni vyema kuwa na sauti ya pamoja katika masuala ambayo kama ukanda wa Kusini mwa Afrika tunaona ni muhimu katika kuendeleza uhifadhi na maendeleo ya watu wake,” Mhe. Chillo amesisitiza.
Aidha, Mhe. Chillo amesema Tanzania imeridhia Itifaki ya Misitu inayosaidia usimamizi wa misitu katika nchi za SADC na kuzishauri nchi ambazo hazijaridhia itifaki hiyo kukamilisha mchakato ili kuweza kuwa na uoanishaji wa nyenzo za usimamizi wa misitu na rasilimali zake.
Katika hatua nyingine, Mawaziri wa SADC wanaoshughulikia Mazingira, Maliasili na Utalii wamepokea taarifa ya kuundwa kwa vikundi kazi vya utalii vitakavyokuwa na jukumu la kusimamia programu ya Utalii ya SADC ya mwaka 2020-2030.
Mkutano huo pia umejadili kuhusu makubaliano ya kuwepo kwa Mkakati mpya wa kukabiliana na ujangili (SADC LEAP 2022 – 2032) wenye lengo la kupunguza vitendo vya ujangili wa wanyamapori na uhifadhi kwenye nchi za SADC.