Tanzania yasaini Hati ya Makubaliano na UN-Habitat, kuanzisha ofisi hapa nchini

NA MWANDISHI WETU
Nairobi Kenya

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesaini hati ya makubaliano kati yake na Shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi Duniani (UN-Habitat) jijini Nairobi leo. 
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula na Mkurugenzi Mtendaji wa UN- Habitat, Bi. Maimunah Sharif wakisaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano jijini Nairobi leo.

Makubaliano hayo yamesainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Bi. Maimunah Mohd Sharif na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Angeline Mabula.

Hati ya makubaliano hayo imelenga kuboresha ushirikiano baina ya Serikali kupitia Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Shirika la Makazi Duniani katika maeneo mbalimbali. 
Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Kenya, Dkt. John Simbachawene aliposhuhudia utiaji saini makubaliano hayo leo.

Maeneo hayo ni pamoja na kutoa utaalam maalum kwa kuzingatia viwango vya Shirika la Makazi Duniani, kuchangia na kuweke vipaumbele vya Serikali katika kuwezesha uboreshaji wa makazi holela na kuwezesha ujenzi wa nyumba za gharama nafuu. 

Maeneo mengine ya makubaliano ya hati hiyo ni kusaidia matumizi jadidifu ya nishati katika majengo, kupitia na kuandaa sera mpya za miji, kuanzisha kituo cha taarifa ya Makazi na kuboresha mifumo ya kitaasisi na uendelezaji wa miji midogo. 
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula na Mkurugenzi Mtendaji wa UN- Habitat, Bi. Maimunah Sharif wakionesha Hati ya Makubaliano ya ushirikiano baada ya kusaini jijini Nairobi leo.

Aidha, makubaliano hayo yataliwezesha shirika hilo kuisaidia Tanzania kujenga uwezo katika ngazi ya Taifa, Mikoa na Serikali za Mitaa katika utekelezaji wa ajenda mpya ya miji, kuwezesha upatikanaji wa wadau wa maendeleo, mifumo ya Umoja wa Mataifa na wadau muhimu katika kuchainga utekelezaji wa ajenda mpya ya miji na kutengeneza njia na mfumo wa ufuatiliaji wa utekelezaji wa ajenda mpya ya miji na Maendeleo Endelevu hasa lengo la 11 na kutoa taarifa ya mafanikio ya utekelezaji wake.

Kadhalika, hati hiyo imeweka makubaliano ya kuwezesha Shirika la Makazi Duniani kuanzisha ofisi yake nchini Tanzania ili kurqhisisha utekelezaji wa makubaliano hayo.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa UN- Habitat, Bi. Maimunah Sharif alipoingia katika ofisi za shirika hilo jijini Nairobi kusaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano leo.

Akizungumza kabla ya kusaini makubaliano hayo, Waziri Dkt.Angeline Mabula amelishukuru shirika hilo kwa misaada mbalimbali inayoipatia Tanzania na akawapongeza kwa uamuzi wake wa kuanzisha Ofisi nchini Tanzania. 

Pia amewahakikishia kuwa, Serikali ipo tayari kuwapatia jengo la kuanzisha Ofisi za UN- Habitat nchini Tanzania. 

Mheshimiwa waziri Dkt.Mabula ameliomba shirika hilo kusaidia kuwajengea uwezo watanzania kwa kuwapa mafunzo na ajira ya muda mfupi na mrefu ili kuwajengea uwezo. 
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa Dkt.Angeline Mabula na Balozi wa Tanzania nchini Kenya,Dkt. John Simbachawene wakiagana na Mkurugenzi Mtendaji wa UN- Habitat mara baada ya kusaini hati ya makubaliano ya ushirikiano jijini Nairobi leo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Bi.Maimunah Sharif amesema kuwa, malengo Endelevu ya Makazi na nyumba yatafikiwa haraka kwa kuwa na Ofisi ya Kudumu nchini Tanzania na nchi nyingine wanachama wa shirika hilo. 

Amesema kuwa, shirika hilo linafanya maandalizi kabambe ya kuanzisha ofisi zake nchini Tanzania ili kuanza utekelezaji wa makubaliano hayo na itaanza utekelezaji wa kuondoa makazi holela ili kuwa na miji salama na iliyopangwa.

Ameihakikishia Tanzania kuwa, shirika hilo lipo tayari kutoa mafunzo na ajira za muda mfupi ili kuwajengea watanzania uwezo wa kusaidia utekelezaji wa makubalino yaloyofikiwa. 
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula akiagana na Mkurugenzi Mtendaji wa UN- Habitat, Bi. Maimunah Sharif katika ofisi za shirika hilo jijini Nairobi baada ya kusaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano leo.

Kufunguliwa kwa Ofisi za Shirika la makazi la Umoja wa Mataifa nchini Tanzania kutaharakisha maendeleo endelevu ya sekta ya makazi na nyumba na kutatoa ajira kwa watanzania.

UN-Habitat ni miongoni mwa mashirika ya Umoja wa Mataifa ambalo linashughulikia makazi ya watu na maendeleo endelevu ya miji. 

Shirika hilo lilianzishwa mwaka 1977 kama matokeo ya Mkutano wa kwanza wa Umoja wa Mataifa wa Makazi ya Watu na Maendeleo Endelevu ya Miji uliofanyika Vancouver, Canada mwaka 1976.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news