NA MWANDISHI WETU
Nairobi Kenya
SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema kuwa imeongeza kasi ya kuboresha miundombinu, makazi na huduma za jamii kwenye maeneo ya mijini na vijijini ili kuhakikisha kuwa watu wote wanaishi katika makazi bora na salama.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa Dkt. Angeline Mabula akiwa na Mshauri wa Rais katika Masula ya Mazingira, Dkt. Robert Muyungi na Balozi wa Tanzania nchini Kenya Balozi, Dkt.John Simbachawene wakati alipotoa tamko la Serikali kwenye Mkutano wa Shirika la Makazi Duniani unaoendelea jijini Nairobi.
Hayo yamesemwa leo Juni 6, 2023 jijini Nairobi na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Mheshimiwa Dkt.Angeline Mabula kwenye Mkutano wa Shirika la Umoja wa Matifa linaloshughulikia Makazi Duniani (UN-Habitat) unaoendelea jijini humo.
Akitoa tamko la nchi kwenye Mkutano Mkuu wa Shirika la Makazi Duniani ulioanza jana jijini Nairobi, ambao kauli mbiu yake ni "hatma ya miji endelevu kupiti ushirikishwaji na uwepo wa mifumo ya mahusiano ya kimataifa", Waziri Dkt.Mabula amesema kuwa, Serikali ya Tanzania inachukua hatua madhubuti ili kukabiliana na ongezeko kubwa la watu mijini na changamoto za makazi na mabadiliko ya tabianchi, kama sehemu ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (Sustainable Development Goals) ambayo kila nchi duniani inatekeleza.
Sehemu ya wajumbe wa mkutano kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Amesema kuwa, takwimu za Sensa ya Watu na Makazi nchini iliyofanyika mwaka 2022 zinaonesha kuwa, asilimia 35 ya Watanzania wanaishi mijini huku kukiwa na ongezeko la uhamiaji mijini la asilimia 4.8 kila mwaka kati ya Watanzania wote milioni 61.7.
Dkt.Mabula pia ameueleza mkutano huo kuwa Serikali inalenga kuendelea kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba na kuhamasisha matumizi ya usafiri usioharibu mazingira, kudhibiti mafuriko, kuweka mipango ya kuifanya miji iwe salama kwa mazingira na kuweka mipango ya kudhibiti kina cha bahari kisizidi na kuingia nchi kavu.
Sambamba na mipango hiyo amesema, Serikali itaendelea kuhimiza matumizi bora ya uzalishaji nishati safi na endelevu. Aidha, aliufahamisha mkutano kuwa, serikali imerasimisha makazi kwa asilimia 61 ya makazi yasiyopangwa nchini ambayo kwa sasa yametimia 3,400.
Akasisitiza kuwa mipango yote hiyo aliyoitaja ni sehemu ya utekelezaji wa mipango ya Taifa chini ya makubaliano ya Paris na kwamba athari za mabadiliko ya tabianchi zinazochochea kwa kiasi kikubwa na idadi kubwa ya watu kuhamia mijini, gharama zake haziwezi kuondolewa na Serikali peke yake.
Amesema, ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, Tanzania inahitaji kiasi cha dola za Kimarekani bilioni 19 hadi kufikia mwaka 2030 kwa maeneo ya kutekeleza mipango mbalimbali ya kukabili mabadiliko ya tabianchi.
Alitumia fursa hiyo kuwakaribisha Wajumbe wa Mkutano huo kwa niaba ya Mheshimiwa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano Mkuu wa Mifumo ya Chakula barani Afrika (Africa Food Systems Summit), AGRAF unaotarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Septemba 4 mpaka 6, mwaka huu.
Wakati huo huo, Waziri Dkt.Angeline Mabula amekutana na Ujumbe kutoka nchi ya Venezuela ambao katika kikao hicho kilichoitishwa na Waziri wa Nyumba na Makazi wa nchi hiyo, Mhe.Ildemaro Moises Arismandi wamejadili masuala mbalimbali yanayohusiana na nyumba, makazi na mipango miji.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa Dkt. Angelina Mabula akiwa katika kikao cha mashauriano na Waziri wa Nyumba na Makazi wa Venezuela, Bw. Ildemaro Arismande jijini Nairobi leo.
Waziri huyo wa Venezuela alikumbushia maombi ya nchi yake waliyowasilisha nchini Tanzania ya kufungua Ubalozi jijini Dodoma.
Akijibu maombi yao, Mheshimiwa Waziri Mabula aliuambia ujumbe huo kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anakaribisha mahusiano ya kimataifa ili kusaidia maendeleo ya watu na kwamba Serikali ya Tanzania imetenga eneo jijini Dodoma kwa ajili ya kujenga ofisi za Balozi mbalimbali katika eneo la mji wa Serikali.
Amesema kuwa, serikali ya Tanzania inakaribisha wawekezaji katika sekta ya nyumba na makazi ambao watasaidia kuharakisha upatikanaji wa nyumba bora kwa watanzania na kuboresha namna miji yetu.