Tume yatoa matokeo ya uchunguzi wa kifo cha mwanafunzi Nusura Hassan Abdallah

NA DIRAMAKINI

MWENYEKITI wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nchini (THBUB),Jaji mstaafu Mathew P. M. Mwaimu ametoa matokeo ya uchunguzi wa kifo cha mwanafunzi Nusura Hassan Abdallah.

Matokeo hayo ameyatoa leo Juni 2,2023 kupitia taarifa aliyoitoa kwa umma, "Mtakumbuka kuwa tarehe 10 Mei, 2023, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) ilitoa taarifa kwa Umma kupitia vyombo vya habari ikielezea nia yake ya kufanya uchunguzi wa kifo cha aliyekuwa Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM),

"Marehemu Nusura Hassan Abdallah, ambacho chanzo chake kilizua mkanganyiko, ambapo baadhi ya watu walikihusisha na ajali ya gari iliyomhusu Mhe.Dkt. Festo John Dugange (Mb), Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa - OR, TAMISEMI (Afya).

Tunapenda kuutaarifu Umma kuwa, THBUB imekamilisha uchunguzi iliyouanzisha yenyewe kwa mujibu wa Kifungu cha 15(1)(a) cha Sheria ya THBUB, Sura ya 391,kinachoipa uwezo wa kuanzisha uchunguzi.

Pamoja na uwezo wa kuanzisha uchunguzi yenyewe, Ibara za 130(1)(c) na 130(4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ikisomwa pamoja na Kifungu cha 6(1)(c)(f) cha Sheria ya THBUB, Sura ya 391, zinaipa mamlaka THBUB kufanya uchunguzi huru wakati wowote juu ya mambo yanayohusu uvunjaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.

Mjadala uliokuwa ukiendelea ulikuwa unaashiria kuvunjwa kwa haki za binadamu na kukiukwa kwa misingi ya utawala bora.

Katika uchunguzi huo, THBUB ilitembelea eneo ilipotokea ajali ya gari iliyomhusisha Mhe. Dkt. Dugange; nyumbani kwa Mhe. Dkt. Dugange; Kituo cha Polisi (Traffic) Mkoa wa Dodoma; Hospitali ya Benjamin Mkapa; na Chuo Kikuu cha Dodoma.

Pia, ilitembelea Kijiji cha Mandewa, Kata ya Mandewa, Wilaya ya Singida Mjini wanakoishi wazazi wa marehemu Nusura Hassan Abdallah; Kitongoji cha Mtakuja Kijiji cha Kikonge, Wilaya ya Iramba alikozikwa Nusura; Ofisi ya Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro; Hospitali ya Faraja iliyopo Himo, Mkoa wa Kilimanjaro; na maeneo mengine kwa madhumuni ya kupata maelezo ya watu mbalimbali kuhusu ajali ya Naibu Waziri na mazingira ya kifo cha Nusura Hassan Abdallah.

Katika maeneo yote Tume ilikokwenda ilipata ushirikiano wa hali ya juu kutoka kwa watu wote iliowahitaji kupata maelezo yao. Tunawashukuru wote walioiwezesha Tume kufanya na kukamilisha uchunguzi wake. Baada ya kupata maelezo katika maeneo yote ilikofika, THBUB imebaini yafuatayo:

1. Usiku wa tarehe 25 Aprili, 2023 kuamkia tarehe 26 Aprili, 2023 ilitokea ajali ya gari maeneo ya Iyumbu, karibu na Njia Panda ya Shule ya Mfano, Jijini Dodoma ambapo gari iliacha njia, kugonga mti na kupinduka;

2. Baada ya kupata majeraha kutokana na ajali hiyo, Dkt. Dugange alihangaika kutafuta msaada ili aweze kufikishwa hospitali kupata matibabu. Majira ya alfajiri ya tarehe 26 Aprili 2023, Dkt. Dugange alipata msaada wa boda boda
iliyomfikisha Hospitali ya Benjamin Mkapa;

3. Tarehe 27 Aprili, 2023, Marehemu Nusura Hassan Abdallah aliyekuwa Mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu cha Dodoma alisafiri kuelekea Moshi mkoani Kilimanjaro kwa basi la Manning Nice baada ya gari la Kapricon alilokuwa amepanga kusafiria kuchelewa.

Basi hilo la Manning Nice lilimfikisha Babati na baadaye kupanda gari aina ya Coaster mpaka Arusha na kumalizia safari yake hadi Moshi kwa basi la Ibra Line;

4. Marehemu Nusura Hassan Abdallah alipokelewa na mchumba wake Juma Mohamed Kundya, Mjini Moshi ambapo walifika nyumbani kwake saa tano usiku wa tarehe 27 Aprili, 2023.

Lengo la safari hiyo lilikuwa ni kuzungumzia masuala ya uchumba wao na kupanga siku ya mchumba wake kwenda kujitambulisha nyumbani kwao Singida. Aidha, alipanga kukaa hapo hadi tarehe 02 Mei, 2023 ndipo arejee Dodoma;

5. Mara ya mwisho Marehemu kuwasiliana na familia yake ilikuwa tarehe 29 Aprili, 2023 na mara ya mwisho kuwasiliana na rafiki yake aliyekuwa akisoma naye Chuo Kikuu cha Dodoma ilikuwa tarehe 1 Mei, 2023 akiwa mzima wa afya;

6. Tarehe 01 Mei, 2023, Marehemu Nusura aliandaa chakula cha jioni ambacho alikula yeye, mchumba wake na mpwa wa mchumba wake. Baada yakumaliza kula, Marehemu Nusura alijisikia vibaya na kuanza kutapika hadi kuishiwa nguvu hali iliyosababisha kufikishwa Hospitali ya Faraja kwa matibabu. Pamoja na hatua mbalimbali za kitabibu zilizochukuliwa na Madaktari wa Hospitali hiyo, Nusura Hassan Abdallah alifariki dunia majira ya
saa 5:00 usiku ya tarehe 01 Mei, 2023;

7. Vipimo vilivyofanywa na Hospitali hiyo vilionesha kuwa kifo cha Nusura Hassan Abdallah kilitokana na shambulio kali la kupanda kwa sukari na upungufu wa damu (diabetic ketoacidosis with hypovolemic shock and moderate anaemia);

8. Daktari aliyempatia huduma na ndugu wa marehemu walioutayarisha mwili kwa ajili ya mazishi na kuuona mwili huo kabla ya mazishi walithibitisha kuwa haukuwa na dalili za kupigwa, kujeruhiwa wala majeraha;

9. Mabaki ya chakula walichokula Marehemu Nusura, mchumba wake na mpwa wa mchumba wake; na matapishi yaliwasilishwa katika Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi, na baada ya kufanyiwa uchunguzi taarifa ilionesha kutoonekana kwa dalili yoyote ya kuwemo kwa sumu;

10. Gari iliyopata ajali ilikuwa ni gari binafsi aina ya Toyota Land Cruiser GXR V8 yenye namba za Usajili T454 DWV, iliyokuwa ikiendeshwa na Mhe. Dkt. Festo Dugange, Naibu Waziri, OR - TAMISEMI (Afya). Naibu Waziri alikuwa peke yake katika gari hilo;

11. Kutokana na mazingira hayo, THBUB imebaini kuwa kifo cha Marehemu Nussura Hassan Abdallah hakikuwa na uhusiano wowote na ajali ya gari aina ya Toyota Land Cruiser GXR V8 yenye namba za usajili T454 DWV iliyomhusisha Mhe. Dkt. Festo John Dugange, Naibu Waziri TAMISEMI (Afya) iliyotokea usiku wa tarehe 25 kuamkia tarehe 26 Aprili, 2023 katika eneo la Iyumbu, jijini Dodoma;

12. THBUB haikuweza kuthibitisha mtu yeyote kuhusika na kifo cha Marehemu Nusura Hassan Abdallah kutokana na vielelezo vya Hospitali ya Faraja,Mkemia Mkuu wa Serikali, na maelezo ya mengine ya mashahidi;

13. THBUB inatambua hatua zinazoendelea kuchukuliwa na vyombo vingine ikiwemo Jeshi la Polisi Tanzania na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka katika kulishughulikia suala hili kijinai.

Kutokana na uchunguzi wa vyombo hivyo, THBUB inapendekeza yafuatayo:

i) Jeshi la Polisi Tanzania na mamlaka nyingine zichukuwe hatua ili kuwabaini wale wote wanaohusika na kutoa taarifa za uongo na chonganishi zinazosababisha taharuki katika jamii;

ii) Jeshi la Polisi Tanzania kwa kushirikiana na mamlaka za usafiri barabarani liweke vifaa vya kiusalama barabarani kama vile kamera ili kubaini (detect) matukio yanayotokea barabarani;

iii) Wananchi waepuke kutoa taarifa zinazoweza kuchochea chuki na kusababisha uvunjifu wa amani;

iv) Wananchi waendelee kuwa na imani na vyombo vya dola katika kuzuia na kupambana na uhalifu na watoe ushirikiano katika kuvisaidia vyombo hivyo kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

THBUB kwa mara nyingine inatoa pole kwa familia ya Marehemu Nusura Hassan Abdallah na jumuiya ya Chuo Kikuu cha Dodoma kwa kuondokewa kwa mpendwa wao.

Mwenyezi Mungu aendelee kuwajaalia subira katika kipindi hiki. THBUB pia inazidi kumpa pole Dkt. Festo John Dugange kwa majeraha aliyopata; Mwenyezi Mungu amjaalie apone haraka ili aweze kuendelea na majukumu yake ya kulijenga Taifa,"imefafanua kwa kina taarifa hiyo ya tume.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news