NA MWANDISHI WETU
MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), umewahimiza wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam na waliotoka katika maeneo mbalimbali nchini kufika katika Banda la NHIF katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere ili kupata huduma ya kusajili kuwa wanachama.
Rai hiyo imetolewa na Meneja Uhusiano wa Mfuko huo, Bi. Anjela Mziray ambaye ameeleza kuwa, kupitia Maonesho ya 47 yanayoendelea sasa katika viwanja hivyo, Mfuko unatoa huduma ya usajili wa wanachama kupitia mpango wa Vifurushi ambao unamwezesha kila mwananchi kujiunga na kunufaika kwa kuwa na uhakika wa matibabu.
Amesema kuwa, mbali na usajili wa wanachama, Mfuko pia unatumia fursa hiyo kutoa elimu ya dhana ya bima ya afya na umuhimu wa kujiunga kabla ya changamoto za afya, kupokea mrejesho wa huduma na maoni ya uboreshaji wa huduma na kushughulikia changamoto mbalimbali walizokutana nazo wanachama.
“Tuko hapa Sabasaba katika Jengo la NHIF na mwaka huu tumekuja na huduma ya usajili wa wanachama kupitia Mpango wa Vifurushi, mpango huu ni rahisi kwa mwananchi mmoja mmoja au na familia kujiunga na kuwa na uhakika wa kupata matibabu wakati wowote bila kikwazo cha fedha, hivyo nitumie fursa hii kuwaomba wananchi wachukue maamuzi sahihi ya kujiunga,” amesema Bi.Mziray.
Amesema kuwa, moja ya faida kubwa kwa mwanachama wa NHIF ni kuwa na uhakika wa kupata huduma za matibabu popote nchini na hii inawezekana kutokana na Mfuko kuwa na mtandao mkubwa wa vituo vya kutolea huduma.
Mpango wa Vifurushi unampa fursa mwananchi kuchangua kifurushi kutokana na mahitaji yake ikiwemo ya idadi ya wanufaika wake. Aidha, Vifurushi hivyo vyenye huduma zote za msingi kuanzia kumwona daktari, vipimo, dawa, kulazwa na upasuaji vinajulikana kwa majina ya Najali Afya, Wekeza Afya na Timiza Afya.