NA ADELADIUS MAKWEGA
WAKRISTO wameambiwa kuwa wasibababaike juu ya fumbo la imani la Utatu Mtakatifu, kwani Mungu Baba ni Muumbaji, Mungu Mwana ni Mkombozi na Mungu Roho Mtakatifu ni Mfariji.
Huku nafsi zote tatu zinafanya kazi katika umoja usiogawanyika, ndiyo maana Waraka wa Mtume Paulo kwa Wakorinto, Jumapili hii Wakristo wote wanaagizwa wasalimiane kwa Busu Takatifu.
Hayo ameyahubiri Padri Samwel Masanja katika Misa ya Jumapili ya tisa ya Sherehe ya Utatu Mtakatifu Juni 4, 2023 iliyofanyika katika Kanisa la Bikira Maria Malikia wa Wamisionari, Parokia ya Malya, Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza.
“Je wewe unamfanyia jirani yako busu la namna gani? Mume na mke wanasalimiana kwa busu la namna gani? Busu Takatifu linamaanisha utimilifu wa upendo mkamilifu, upendo unaojidhihisha kwa nje.
"Je? Wewe unautimilifu wa upendo? Je wewe unaukamilifu wa upendo? Kwa nje kama unacheka, kwa nje kama unatabasamu lakini kwa ndani una visasi, unamasengenyo, hayo matendo siyo ya busu takatifu. Angalia mizigo hiyo haioneshi kuwa mtu unayetoa busu takataifu. Upendo uliokamilifu ni upendo tunajifunza kutoka kwa Utatu Mtakatifu.”
Misa hiyo pia iliambatana na maombi kadhaa na mojawapo lilikuwa hili, “Ulisema kwamba haukutumwa kutoa hukumu, bali kutupa uzima, utuangazie katika furaha yako ya habari njema ee Bwana.”
Hadi misa hiyo ya pili iliyoanza saa 3.30 ya asubuhi inakamilika saa 6.00 ya mchana hali ya hewa ya eneo la Malya lililopo Kwimba mkoani Mwanza ilikuwa ya jua kali, majani yakiwa bado ya kijani kibichi huku mifugo ikipata malisho yakutosha, nao wakulima na mpunga wakiendelea kuvuna mashambani.