Ukikutwa na dawa za kulevya, Wamasai tunakususa ukashughulikiwe-Isaac Ole Kisongo

NA DIRAMAKINI

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) imetoa elimu juu ya madhara ya dawa za kulevya hususani kilimo na matumizi ya bangi katika Kijiji cha Kisimiri Juu kilichopo wilayani Arumeru mkoani Arusha.

Elimu kwa wananchi wa Kisimiri Juu imetolewa kufuatia operesheni tokomeza bangi liyofanywa na mamlaka katika kijiji hicho ambapo kiasi kikubwa cha bangi mbichi na kavu kilikamatwa hivi karibuni ikiwemo kuharibiwa na kuteketezwa kwa mashamba ya bangi.
Akizungumza katika hafla ya utoaji elimu ambayo iliongozwa na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA), Aretas Lyimo huko Kisimiri Juu, Kiongozi Mkuu wa Jamii ya Masai Tanzania, Laigwanani Isaac Ole Kisongo ametoa onyo kali kwa Wamasai wote na kuwataka kutojihusisha na matumizi na biashara ya dawa za kulevya. 

"Makundi haya niliyoyataja, nimepiga marufuku hakuna kiongozi atakayesaidia mtu yeyote ambaye atapatikana na dawa za kulevya, kuhangaika polisi na hata kukutoa mahakamani, jamani si nimewaambia hivyo nyie?.

"Haitakiwi hata gongo, sisi jamii ya wa Masai mimi kama kiongozi wao mkuu, nilishapiga marufuku kwamba kiongozi yeyote ndani ya jamii ya Wamasai kama kundi la vijana, kama walezi wa wale watoto vijana, kama kiongozi wa hilo kundi ambaye ndiye Laigwanani mkuu wa mkoa tumepiga ni marufuku kupatikana polisi.

"Mtu amekamatwa amekutwa akijihusisha na mambo kama haya, masuala ya bangi na madawa mengine ya kulevya,lakini hata wabakaji wasijihusishe. 

"Wabakaji, watu wote ambao wanajihusisha na masuala kama hayo hata mtoto anayepewa mimba akiwa masomoni nimeshapiga marufuku kwamba, mtu yeyote, kiongozi yeyote ndani ya jamii usipatikane, ukipatikana tutakufuta nafasi yako, siyo tunakufuta ninakufuta mimi na tutakuunganisha na vyombo vya dola ambavyo ni TAKUKURU (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania) uwajibishwe kisheria,"amefafanua Laigwanani Isaac Ole Kisongo .

Kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi wa jamii hiyo ya wafugaji wameahidi kuimarisha ushirikiano ili kuhakikisha wanafanikisha udhibiti wa dawa za kulevya hususani bangi huko Kisimiri Juu.

"Wananchi wamekubali kabisa, mpaka wamechangua kamati ya kuangamiza dawa za kulevya kwa kuingia shamba hadi shamba kwa kila mwezi.

"Na mpaka na faini tumeshaweka mheshimiwa, kwamba hiyo kamati tuliyoichagua ndani ya Kijiji cha Kisimiri Juu, kamati ya watu 60 ndiyo tunaowachagua kwa sababu ndani ya kijiji chetu tuna vitongoji vitatu, kwa kila kitongoji tumechagua watu 20...ishirini,ukijumlisha ndani ya vitongoji vitatu ni watu sitini, tunajua kabisa kwamba hiyo kamati mkikuta jani kwenye shamba la mtu, faini ni laki tano akikataa tunamkamata sisi wenyewe tunampeleka mahali pa usalama.

"Ili wananchi hao waweze kukaa katika hali ya usalama, bila bughda ya aina yoyote na tumesema atakayebughudi kamati hiyo, yaani kijiji kizima kitahamia kwake, tunahamisha pamoja na familia yao waende moja kwa moja, lakini hao wengine wabaki katika hali ya usalama, kwa sababu watu hao wameteseka sana, 

"Sasa hivi tuna watoto zaidi ya 100 hospitalini, sababu ya nimonia, yaani mzazi aliyejifungua saa hiyo hiyo anakimbilia porini, korongoni na kale katoto kadogo, yaani ameshakuwa na udhaifu mkubwa sana, yaani hilo mheshimiwa tumeschukia na tumeapa, pia tunawashukuru sana kwa ushirikiano wenu mkubwa, tuwe pamoja mpaka dakika ya mwisho,"amesema Mwenyekiti wa Kijiji cha Kisimiri Juu.

Naye mwanakijiji mwingine wa Kisimiri Juu amesema, "ni aibu Masai popote duniani, kusikika analima bangi ni aibu Masai popote duniani kusikika anavuta bangi, yaani sijui nisemeje au nizungumze kwa lugha gani, lakini ni jambo kubwa la aibu sana, lakini basi tunaomba hivyo vitu vitatu tusaidiwe, hakika tunaimani kabisa tutaliacha ili, sasa tusije tukasema tunaacha kumbe kuna vitu vidogo ambavyo vinaleta ushawishi.

"Ya kwanza, barabara ya pili maji ya tatu ardhi yetu tunayo ya kutosha kwa ajili ya ufugaji. Tusimamiwe ardhi yetu ili tuweze kuwa na milki, hivi vitu vitatu tukisimamia ninaimani hatutaweza tena kufika huko."

Mwanakijiji mwingine amesema, "Tunaahidi kumaliza kabisa dawa hizi, ili ukirudi hapa uwe kama rafiki, lakini usiende kabisa ukazamia, wamama hawa wanahitaji barabara kwa ajili ya kuwafikisha kliniki, kupata zao mbadala kwani tumeshakaa muda mrefu tukatamani tupimiwe kama karanga itafaa eneo hili, maana ni eneo kubwa, kuna sehemu ambayo mahindi yamelimwa yanastawi kama mwaka huu kuna njaa sana,"ameongeza mwanakijiji huyo.

Awali Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA),Aretas Lyimo amewapa elimu wanavijiji wa Kisimiri Juu kuhusu umuhimu wa kuachana na kilimo cha bangi na kujihusisha na mazao mbadala kwa ustawi bora wa familia zao na Taifa kwa ujumla.
"Nimekuja kuwapa neno la heri, neno la busara ili sisi sote sasa tuweze kwenda na mwenendo wa Serikali wa kutii sheria bila shuruti kuhakikisha kwamba katika maeneo yetu yote hakuna zao la bangi linalolimwa tena katika maeneo yetu, mwanzoni tulipokuja kwenye operesheni, zile siku nane tulikuja kikazi, tulikuja kioperesheni si ndiyo na watu mkahama kwenye nyumba zenu.

"Lakini, ninafurahi leo tupo wote hapa, hakuna aliyehama kwenye nyumba kwa sababu tumekuja kwa amani, tumekuja kuwapa elimu ili sote tuweze kujua tatizo la dawa za kulevya, madhara ya dawa za kulevya, madhara ya kulima bangi, madhara ya kuvuta bangi.

"Ili tuhakikishe tunajenga kizazi cha kesho, kizazi cha wachapakazi, kizazi cha wazalishaji, kizazi ambacho kitajenga uchumi wa nchi, kwa sababu kwenye maeneo yetu haya athari ya bangi inaharibu zaidi vijana. 

"Athari kubwa inapoingia kwa vijana, wanashindwa kuzalisha wanaposhindwa kuzalisha, nchi haiwezi kuendelea kiuchumi kwa sababu, vijana wengi ambao ndiyo nguvu kazi ndiyo inayoharibiwa na bangi,"amefafanua Kamishna Jenerali Aretas Lyimo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news