UNRA yafungua daraja la Mto Katonga

NA DIRAMAKINI

MAMLAKA ya Kitaifa ya Barabara nchini Uganda (UNRA) imefungua daraja la Mto Katonga ambalo awali liliporomoka kwa ajili ya kupita magari madogo na watembea kwa miguu, na hivyo kuleta ahueni kwa watumiaji wa barabara hiyo.

Katika taarifa yake siku ya Mei 31, 2023 UNRA ilisema kufuatia matengenezo, daraja hilo sasa limefunguliwa kwa ajili ya matumizi ya magari madogo ambayo ni pamoja na pikipiki, toyota saloon, SUV, teksi, na daladala zenye viti 28 maarufu kama coasters.

“Gari lolote ambalo halijajumuishwa katika kundi lililotajwa hapo juu halitaruhusiwa kuvuka daraja,” UNRA ilisema katika taarifa yake.

Hivyo walionya kuwa madereva wa mabasi,na malori ya aina yoyote bado hawajaruhusiwa kutumia daraja hilo.

Kulingana na UNRA, kwa magari madogo ambayo sasa yameruhusiwa kutumia daraja hilo, kutakuwa na njia ya moja, hivyo wasafiri wanapaswa kutarajia ucheleweshaji fulani.

“Madereva wanatakiwa kufuata kwa makini miongozo ya askari wa usalama barabarani,na alama za barabarani kwa usalama na kuepusha ucheleweshaji.

"Tathmini zaidi za kimuundo zitafanywa ili kuamua matumizi ya daraja na magari mazito zaidi. Hatua nyingine zitaendelea kwa lengo la kuirejesha barabara itumike kikamilifu katika muda mfupi na haraka iwezekanavyo.”

Aidha, maendeleo hayo ni faraja kwa wasafiri wengi wanaotumia barabara hiyo, hasa kuelekea Masaka na maeneo mengine ya Magharibi mwa Uganda ambao walikuwa wanatumia barabara ya Ssembabule.

Kuporomoka kwa daraja la Katonga na kuchangia magari kupitia Ssembabule kumesababisha kupanda kwa nauli za usafiri barabarani kutokana na umbali mrefu na wa kuchosha huku madereva wa magari ya watu binafsi wakisema walilazimika kuingia gharama kubwa za mafuta.

Kazi zinazoendelea za ujenzi wa daraja lililoporomoka la Mto Katonga zinafanywa na Kampuni ya China Communications Construction, Ltd.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news