Wafanyakazi 15 wa Jiji la Dar es Salaam kizimbani kwa kuongoza genge la uhalifu

NA MWANDISHI WETU

WAFANYAKAZI 15 wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka 143 ikiwemo kuisababishia Halmashauri ya Jiji hasara ya zaidi ya shilingi bilioni 8.9.

Mbali na shtaka la kusababisha hasara, mashtaka mengine ni, kuongoza genge la uhalifu, matumizi mabaya ya madaraka, kuingiza taarifa za udanganyifu katika mfumo, ufujaji na ubadhirifu, kughushi, utakatishaji na kuisababishia halmashauri hiyo hasara ya shilingi 8,931,598,500.

Katika hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo na Wakili wa Serikali, Faraji Ngukah akisaidiana na Wakili Pendo Temu imewataja washtakiwa hao kuwa ni Tulusubya Kamalamo, James Bangu, Mohamedi Khais, Abdalah Mlalwe, Deogratius Lutateza, Judica Ngawo, Febronia Nangwa na Groly Eugen.

Wengine ni, Saidi Bakari, Josephina Sandewa, Doricas Gwichala, Jesca Lutagonzibwa, Patrick Chibwana, Ally Baruan na Khalid Nyakamande.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Pamela Mazengo inadaiwa kati ya Julai Mosi, 2019 na Juni 30, 2021 katika Wilaya ya Ilala ndani ya Jiji la Dar es Salaam washtakiwa waliongoza genge la uhalifu na kujipatia shilingi 8,931,598, 500 mali ya Halmashauri ya Ilala.

Ngukah aliendelea kudai kuwa katika kosa la matumizi mabaya ya madaraka washtakiwa wakiwa watumishi wa umma kwa nafasi mbalimbali katika halmashauri hiyo walishindwa kuingiza mapato katika akaunti za halmashauri hiyo zilizopo katika benki za NMB, CRDB,NBC na DCB kiasi cha shilingi 8,931,598,500.

Inadaiwa kuwa washtakiwa Ngawo, Nangwa, Mohamedi na Eugen kwa pamoja wanashtakiwa kwa makosa 53 ya kuingiza taarifa za udanganyifu katika mfumo zikionesha kuwa mapato yaliyokusanywa toka sehemu mbalimbali yameingizwa katika akaunti za halmashauri hiyo huku wakijua kuwa siyo kweli.

Aidha, washtakiwa pia wanadaiwa kughushi nyaraka mbalimbali kuonesha kuwa ni za harali huku wakijua ni kosa kisheria.

Wakili Nguka ameendelea kudai kuwa washtakiwa hao pia wanakabiliwa na shtaka la utakatishaji wa fedha shilingi bilioni 8.9 wakati wakijua fedha hizo zilitokana na kosa tangulizi la kugushi.

Hata hivyo, inadaiwa kwamba, washitakiwa hao pia wanakabiliwa na shitaka la kuisababishi halmashauri hiyo hasara ya kiasi cha shilingi bilioni 8.9.

Washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.

Aidha, kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika na kesi imeahirishwa hadi Julai 10, 2023 washtakiwa wote wamerudishwa rumande kwa kuwa kesi hiyo haina dhamana.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news